Vita vya Ukraine: Teknolojia ya kizamani inavyoisaidia Ukraine dhidi ya Urusi

Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vlad anasema simu za kizamani ni njia salama ya mawasiliano

Wakati Ukraine ikijiandaa kwa mashambulizi yake makubwa, itakuwa vigumu kwa wanajeshi wake kujificha dhidi ya vikosi vya Urusi. Kwa hivyo Ukraine inalazimika kutafuta njia za kuwachanganya adui.

Kwenye maficho ya mtaro huko mashariki, Ukraine inajua Urusi haijaribu tu kuwawinda kwa kutumia ndege zisizo na rubani - pia inatumia vita vya kielektroniki kujaribu kujua walipojificha.

Wanajeshi wa Brigedi ya 28 ya Ukraine wanaweza kutumia teknolojia ya Karne ya 21 - mfano satelaiti, simu mahiri na kompyuta za mkononi - ili kusaidia kuwasiliana na kutambua adui alipo. Lakini pia wanatumia mashine za kizamani.

Teknolojia ya kale ambayo inayofanana na ilemiliyotumika wakati wa Vita vya Kwanza vya dunia: simu ya zamani ya upepo.

Vlad na watu wake hutumia simu wakati wowote wanapokaribia kurusha kombora. Kwa simu zinazotoka, lazima uzungushe mpini. Ukiona ni kama unaangalia filamu za zamani enzi hata rangi hamna (black and white).

Vlad anashika nyaya zinazofika kwenye mitaro mingine iliyo karibu. Anasema ni njia salama zaidi ya mawasiliano, na kwamba "haiwezekani kusikilizwa (kuingiuliwa na adui)".

Anasema mifumo ya vita vya kielektroniki vya Kirusi inaweza kugundua na kunasa simu za mkononi au rununu na redio, lakini akionyesha simu yake ya zamani, Vlad anasema: "Teknolojia hii ni ya zamani sana - lakini inafanya kazi vizuri."

ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Kufikia sasa, vikosi vya kawaida vya Urusi vimefanya vibaya na kupata hasara kubwa, lakini bado ina mifumo ya juu zaidi ya vita vya kielektroniki ulimwenguni - njia zisizoonekana za kufuatilia adui na kuingilia au kuzuia mawasiliano.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hilo linafanya Ukraine kuwa kwenye hatari na kukutana na wakati mgumu zaidi. Rada za Zoopark za Urusi zinaweza kutambua moshi na moto wa mizinga. Magari yake ya Zhitel hutambua, kufuatilia na kuzuia masafa ya redio, huku Borisoglebsk-2 inaweza kutatiza mawasiliano ya setilaiti kama vile GPS.

Utumiaji wa Urusi wa vita vya kielektroniki pia unafanya kuwa vigumu kwa jeshi la Ukraine la ndege zisizo na rubani - vitu muhimu vya kusaidia kupata muelekeo wa ndege kwenye uwanja wa vita.

Katika eneo lingine upande wa mashariki, Oleksii na kitengo chake cha kijasusi cha ndege zisizo na rubani cha Brigade ya 59 hutumia jengo lililolipuliwa na bomu kama kinga na kurusha ndege yao ndogo ya kichina kutambua walipo warusi.

Katika hatua za mwanzo za vita, Ukraine ilionekana kuwa na ujuzi zaidi katika matumizi yao. Lakini Oleksii anasema sasa "anga imejaa ndege zisizo na rubani". Anasema Warusi, pia, wanatumia njia sawa, lakini wana ndege nyingi zaidi. Ingawa anaamini "hawajali juu ya hilo".

Oleksii anasema tayari amepoteza ndege tano ndogo zisizo na rubani zilizotengenezwa na Wachina na Brigade yake "huenda ikapoteza 'ndege tatu hadi nne kwa siku". Anasema adui wanaweza kutambua vituo vyetu vya kielektroniki na "kuingilia mawasiliano" ili kuzuia (kuzima) ndege za Ukraine zisizo na rubani.

Lakini katika mikono ya ustadi, anaongeza, ndege ndogo ya kibiashara kama Mavic inaweza kudumu "kati ya wiki mbili na tatu".

Wanajaribu wawezavyo ili kuzuia kugunduliwa - kwa kubadilisha eneo la kijiografia kwa ndege zao zisizo na rubani. Zinarushwa kwa kutumia VPN nchini Australia, ikimaanisha zinaonekana kuzunguka bara upande wa Kusini. Lakini anasema kujificha huko sio kila wakati kunafanya kazi.

Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vita vya kieletroniki vinachukua nafasi zaidi huko Ukraine

Tofauti na hilo, juhudi za Ukraine za kuangusha ndege zisizo na rubani za Urusi zinaweza kuwa za msingi zaidi.

Orlan - ndege isiyo na rubani kubwa zaidi iliyotengenezwa nchini Urusi inaweza kufanya ufuatiliaji au kunasa mawasiliano. Wakati huu inachunguza maeneo ya karibu ya ulinzi ya Ukraine ili kuelekeza eneo la kufyatua risasi.

Tunasikia sauti ya makombora kabla ya kuona athari na moshi ukifuka juu tena kwa mbali.

Majibu ya wanajeshi wa Ukraine walio karibu ni kufyatua mvua ya risasi kuelekea angani, kwa kutumia bunduki zao za kawaida. Lakini ndege isiyo na rubani ya Urusi iko juu sana. Hivyo risasi zao ni sawa na bure.

Katika kituo cha kamandi kilicho karibu, Kamanda Bohdan wa Brigedi ya 10 ya Ukraine, anaelezea kufadhaika kwake kwamba hawawezi kufanya zaidi hilo. Anasema ndege zisizo na rubani za Urusi zinaruka "kila siku, kila saa, kila sekunde. Wana rasilimali kubwa kwenye hilo. Tunapambana kuzikabili lakini si kwa namna tunavyotaka."

Skrini kubwa nyuma yake ingawa inaonyesha kuwa Ukraine bado inaweza kufanya vivyo hivyo - hata kama italazimu sasa wazingatie ndege zao zisizo na rubani kama vifaa muhimu vya kivita vinavyoweza kutumika.

Urusi inaweza kuwa na faida katika vita vya kielektroniki na ndege zisizo na rubani zaidi - zitatoa changamoto kwa mashambulizi yanayokuja ya Ukraine.

Lakini Urusi bado haijaweza kupata udhibiti wa anga, au kudhibiti upinzani na ustadi wa Kiukreni.