Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Kenya 2022: Je, George Wajackoyah ana athari gani katika Uchaguzi huu?
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili
Wakati Professa George Wajackoyah aliwapowasilisha jina lake kuwania urais , hakuna aliyemtambua na kudhania kwamba angekuwa miongoni mwa watu ambao wangezua mjadala mkubwa katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka huu.
Lakini ahadi zake za kushangaza kuanzia kuunga mkono uhalalishaji wa bangi hadi ufugaji wa nyoka kwa lengo la kuuza nyama yake nchini China ni baadhi ya masuala ambayo yamemfanya kuwa maarufu katika mitandao ya kijamii na hivyobasi kuvutia uungwaji mkono katika uchaguzi huu.
Hali hiyo imemfanya mgombea huyo ambaye hakuonekana kuwa na nafasi awali , kupata motisha wa kuendeleza ajenda yake katika kampeni zake ambazo amekuwa akizifanya hadi katika klabu za burudani.
Manifesto yake ilizozua utata?
Miongoni mwa ahadi zake zilizopo ndani ya Manifesto yake ni Pamoja na ,
Kuhalalisha bangi, Kufuga nyoka, Kuuza nyama ya mbwa ugenini, kuwanyonga wafisadi, Kufunga Reli ya kisasa ya SGR, Kufanya kazi kwa siku nne kwa wiki, Kusitisha baadhi ya vipengee vya katiba , Kuhamisha mji mkuu hadi Isiolo, Kubuni majimbo manane na kuwafurusha raia wa kigeni wasio na kazi nchini.
Lakini je mgombea huyu ana athari gani katika uchaguzi huu?
Anawavutia vijana
Tangu George Wajackhoya alipoanzisha kampeni zake amekuwa akivutia idadi kubwa ya vijana katika mikutano yake huku wapinzani wake katika kinyang’anyiro hicho wakitafuta mbinu za kujaribu kukabili tishio la kupoteza kura ya vijana.
Mgombea huyo amekuwa akitembelea migahawa mingi inayotembelewa na vijana ili kujivinjari nao ambapo badala yake hugeuza maeneo hayo na kuwa kumbi za kampeni zake ambapo amekuwa akiwaahidi vijana ahadi kedekede iwapo wangempigia kura huku nao vijana wakimuona kama mmoja kati yao anayewajali zaidi. Hatua hiyo inajiri huku ikibainika kwamba kati ya wapiga kura milioni 22 katika daftari la usajili wa wapiga kura, asilimia 40 ni vijana walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 35.
Hii ina maana kwamba kuna vijana milioni 8.8 katika sajili la wapiga kura nchini. Tayari baadhi ya vijana wametumia umaarufu wa mgombea huyo anayesema atatumia uuzaji wa bangi ugenini kufuta deni la Kenya , kuchapisha tishati na hivyobasi kufanya biashara.
Kusababisha awamu ya pili ya uchaguzi
Kulingana na kura nyingi za maoni , wagombea wawili wakuu katika uchaguzi huu, raila Amolo Odinga wa Azimio na William Ruto wamekuwa wakigawanya asilimia 80 ya wapiga kura kote nchini huku asilimia 20 ya wapiga kura wakiwa bado hawajaamua ni nani watakayemuunga mkono.
Ushindi wa moja kwa moja kati ya wagombea wawili wakuu hautawezekana iwapo Bwana Wajackoyah anayeendelea kuwa maarufu miongoni mwa vijana atapata kura za kutosha ili kuwanyima William Ruto na Raila Odinga asilimia 50 na kura moja kuibuka washindi kwa raundi ya kwanza.
Vilevile iwapo mgombea huyo anaweza kuvutia baadhi ya wapiga kura ambao hawajaamua watamuunga mkono mgombea yupi, kuna uwezekano kwamba awamu ya pili ya uchaguzi huenda ikafanyika iwapo wagombea wawili wanaopigiwa upatu kuibuka washindi hawatofanikiwa kupata asilimia 50 na kura moja ili kuapishwa kuwa mshindi wa uchaguzi kulingana na katiba mpya ya 2010.
Amezua mjadala mitandaoni?
Mitandao ya kijamii imekuwa kumbi mpya za kufanya kampeni miongoni mwa wagombea. Hii ni kwasababu Wakenya wengi wanatumia mitandao hii , kujifahamisha yanayoendelea ulimwenguni, kuwasiliana, kufanya matangazo na hata kutoa maoni yao dhidi ya mambo wasioyapenda.
Hali hii imewafanya wagombea wengi kutumia mitandao ya kijami kuuza sera zao na hata kufanya matangazo. Mbali na ahadi yake ya kuhalalisha bangi nchini na kufuga nyoka ambayo imezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijami, uzinduzi wa manifesto yake hivi majuzi ulisababisha mihemko ya aina yake. Uzinduzi huo ulichukua mkondo wa ucheshi wakati neno Tingiza miti lilipotajwa.
Kila alipotoa hoja zake, msemo huo, ambao inaonekana ulitamkwa na mwanamke, ulichezwa wakati alipositisha hotuba yake. Msemo huo ulizua msisimko mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na kuibua gumzo si haba.Wakenya waliibua hisia tofauti kutokana na msemo huo huku wengine wakionekana kushangazwa.
Ameleta ucheshi katika kampeni
Kabla ya ujio wa George Wajackoyah katika uchaguzi , ni wagombea wawili tu wa urais waliokuwa kifua mbele katika uchaguzi wa mwaka huu , nao ni Raila Amolo Odinga na naibu wa rais William Samoei Ruto. Ushindani kati ya wawili hao ulisababisha hali ya wasiwasi kote nchini kenya huku kila mmoja wao akionekana kuvutia kiasi kikubwa cha wafuasi kila wanapofanya kampeni zao.
Hali hiyo iliwakumbusha Wakenya kuhusu uchaguzi wa 2007 uliozua ghasia ambapo kinyanganyiro kilikuwa kati ya Mwai kibaki na Raila Odinga. Hatahivyo kuwasili kwa George Wajackoyah katika kampeni za mwaka huu kumezua msisimuko wa aina yake sio tu katika mitandao ya kijamii bali kila makaazi nchini kenya.
Ahadi yake ya uhalalishaji wa bangi, kufanya kazi kwa siku nne, kuuza mbwa ugenini na ufugaji wa nyoka, imezua sio tu mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii bali imewasukuma baadhi ya wapiga kura kwenda mahakamani kumzuia huku nao baadhi ya viongozi wa dini wakihoji ahadi hizo. Hali hiyo imepelekea kupoa kwa hali ya wasiwasi iliokuwepo na hata kutoa fursa kwa wagombea wengine wasiojulikana kupata umaarufu.
Hali ya wasiwasi inayosababishwa na kampeni za uchaguzi nchini kenya imesababisha baadhi ya watu kutoka maeneo fulani kuhamia wanakotoka wakihofia kuzuka kwa vurugu. Hali hiyo imewanyima baadhi ya Wakenya haki yao ya kushiriki katika shughuli ya kupiga kura.