Nchi 7 zinazoongoza kwa kuzalisha taka nyingi za plastiki duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kila mwaka, mamilioni ya tani za taka huzalishwa duniani, nyingi zikiwa za plastiki ambazo huishia kuchafua bahari, mito, ardhi na hata anga.
Kwa sasa, dunia inazalisha takriban tani milioni 400 za taka za plastiki kila mwaka, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Kati ya tani bilioni saba za taka za plastiki zinazozalishwa kote duniani kufikia sasa, chini ya asili mia 10 huchakatwa. Mamilioni ya tani za taka za plastiki hupotelea kwa mazingira, au wakati mwingine kusafirishwa maelfu ya kilomita hadi mahali ambapo huchomwa au kutupwa.
Ripoti ya 2024 kutoka Chuo Kikuu cha Leeds inaonesha kuwa zaidi ya tani milioni 52 za taka za plastiki huingia moja kwa moja kwenye mazingira kila mwaka na asilimia 70 ya kiasi hicho kinatoka katika nchi 20 tu.
Umoja wa mataifa unasema makadirio ya hasara ya kila mwaka ya thamani ya taka za mifuko ya plastiki wakati wa kutenga na usindikaji pekee ni USD kati ya bilioni 80 na bilioni 120.
Katika kuadhimisha Siku ya dunia isiyo na taka inayofanyika kila Mei 25, tunaangalia mataifa saba yanayoongoza kwa uzalishaji wa taka za plastiki duniani, kwa takwimu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uhifadhi ya mazingira kama NHM UK ya Uingereza , Our World in Data na GroundReport.
1. China – Tani Milioni 25.4 kwa mwaka
China inaongoza kwa kuzalisha kiasi kikubwa zaidi cha taka za plastiki duniani. Viwanda vingi, idadi kubwa ya watu (zaidi ya bilioni 1.4) na matumizi ya vifungashio katika usafirishaji wa bidhaa huchochea ongezeko hili.
Ingawa serikali imeanzisha kampeni ya kupunguza plastiki, changamoto za utekelezaji bado zipo, hasa katika miji midogo na maeneo ya viwanda.
2. India – Tani Milioni 9.3 kwa mwaka

Chanzo cha picha, Getty Images
India ni taifa la pili kwa uzalishaji wa taka za plastiki. Kwa mujibu wa Ground Report , kiasi cha taka kinachozalishwa nchini humo kila mwaka ni sawa na uzito wa sanamu 75 za uhuru wa Marekani.
Takriban watu bilioni 1.2 nchini humo wanaishi bila huduma rasmi za ukusanyaji taka, hali inayosababisha plastiki nyingi kutupwa kwenye mito au kuchomwa ovyo.
3. Nigeria – Tani Milioni 3.5 kwa mwaka
Nigeria inaongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa taka. Jiji la Lagos peke yake huzalisha maelfu ya tani za taka kila siku, nyingi zikiwa za plastiki.
Ukosefu wa miundombinu ya usimamizi wa taka pamoja na ongezeko la kasi la watu mijini huwafanya wakazi kutegemea njia zisizo rasmi za kutupa taka.
4. Indonesia – Tani Milioni 3.4 kwa mwaka

Chanzo cha picha, Getty Images
Indonesia ni moja ya wachangiaji wakubwa wa taka za plastiki baharini. Zaidi ya asilimia 60 ya taka za plastiki huishia moja kwa moja kwenye mazingira au majini. Visiwa zaidi ya 17,000 na maeneo yasiyofikika kwa urahisi hufanya ukusanyaji wa taka kuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Indonesia.
5. Pakistan – Tani Milioni 2.6 kwa waka
Pakistan inakabiliwa na ongezeko la taka linaloendana na ukuaji wa miji na viwanda. Ingawa sheria kuhusu plastiki zipo, utekelezaji wake ni dhaifu. Miji mikuu kama Karachi na Lahore huchangia kiasi kikubwa cha taka ambazo huishia kwenye mifereji, maeneo wazi na mito kama Ravi.
6. Bangladesh – Tani Milioni 1.7 kwa mwaka

Chanzo cha picha, Getty Images
Bangladesh ni mojawapo ya nchi zilizo na msongamano mkubwa wa watu duniani. Kiasi kikubwa cha plastiki hutumika kwenye vifungashio vya bidhaa za kila siku, hasa sokoni na maeneo ya biashara.
Kwa mujibu wa NHM, zaidi ya nusu ya taka nchini humo hutupwa ovyo bila kuchakatwa au kudhibitiwa.
7. Brazil – Tani Milioni 1.4 kwa mwaka
Nchini Brazil, changamoto kubwa ni ukusanyaji usiofanikiwa wa taka katika vitongoji vya mijini na maeneo ya pembezoni.
Japo Brazil ina viwanda vya kuchakata taka, asilimia kubwa ya plastiki huzagaa kutokana na udhaifu wa mifumo ya manispaa na utofauti mkubwa wa kiuchumi kati ya maeneo mbalimbali.















