Abdon Atangana: Mfahamu Mwanahesabati namba mbili bora duniani anayetaka kuondoa ukoloni wa Hisabati
Valorien Noubissi, BBC Africa

Chanzo cha picha, FREE STATE UNIVERSITY (SOUTH AFRICA)
Yeye ni mmoja wa wanahisabati maarufu zaidi duniani. Abdon Atangana, mtaalamu na gwiji wa hesabati (Applied Mathematics), mwenye ndoto za kuwa na Afrika inayotawala Sayansi.
Ilikuwa Juni 19 huko Paris. Raia huyo wa Cameroon mwenye umri wa miaka 37 alipokea Tuzo ya kwanza ya Kimataifa ya UNESCO-AI Fozan kwa kukuza wanasayansi wachanga katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Ni tuzo ya kila baada ya miaka miwili iliyoanzishwa na UNESCO mnamo 2021, kwa ushirikiano na Wakfu wa Al-Fozan wa Saudi Arabia. Tuzo ambayo, kulingana na mpokeaji, "inathibitisha bila shaka kwamba Waafrika wanaweza kusalia Afrika, kufanya kazi kwa bidii, kusonga mbele na kuendeleza bara lao bila msaada zaidi kutoka nchi za Magharibi".
Majarida ya kisayansi yanakubaliana juu ya jambo moja: Profesa katika Chuo Kikuu cha Free State huko Bloemfontein, Afrika Kusini ametoa mchango muhimu katika uwanja wa hisabati, haswa katika maeneo haya kitalaam : fractional calculus, fractional differential equations na mathematical modeling.
Mnamo mwaka wa 2019, alitajwa na Chuo Kikuu cha Stanford kama mtaalam namba mbili bora wa hesabu ulimwenguni akiwa miongoni mwa 2% ya wanasayansi wa juu ulimwenguni.

Chanzo cha picha, Free State University in South Africa
Yeye ndiye mwanahisabati wa kwanza kupata Tuzo ya TWAS Mohammad A. Hamdan iliyotolewa na World Academy of Sciences ambacho hutuza kazi bora zaidi ya hisabati inayofanywa na mwanasayansi anayefanya kazi na anayeishi Afrika au uarabuni.
Atangana, ambaye alifanya sehemu ya masomo yake nchini Cameroon, mwaka 2017 alikuwa mwanahisabati aliyetajwa zaidi duniani kupitia kazi yake ya kisayansi.
Mnamo mwaka wa 2019 na 2020 alijumuishwa katika orodha ya Wanasayansi wa Juu wa Kimataifa wa Clarivate wa Sayansi (Clarivate Web of Science Top 1% Global Scientists).
Kwa mujibu wa Atangana-Baleanu, tuzo hizi na tofauti ni dhibitisho kwamba "tunaweza kuwa na athari popote tulipo".
"Nitasalia barani Afrika, nitaweka juhudi kubwa katika kusafisha njia na, kwa msaada wa Mungu, nitajenga msingi imara kwa kizazi kijacho," aliambia BBC.

Chanzo cha picha, Andre Damons
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ili kuelewa maneno yake vizuri, lazima kwanza tuelewe kwamba profesa wa hesabu Abdon Atangana anaongoza mapambano ya kina zaidi: anataka kuondoa ukoloni wa hisabati.
Anasema anafanya kazi kwa bidii na anaamini kuwa siku moja “watoto wa Kiafrika watasoma vitabu na makala ambapo wataalamu wa hisabati wa Kiafrika wameanzisha kanuni kadhaa za hisabati, ambazo zinaweza kutumika hasa kutatua matatizo barani Afrika”.
Atananga ambaye amefunga ndoa na mwanakemia Enestine Atangana na baba wa wavulana wawili, anadhani ni muhimu kupitia upya jinsi masomo ya sayansi yanavyofundishwa kwa vijana wa Kiafrika.
“Moja ya udhaifu mkubwa ni namna hesabu inavyofundishwa katika shule za Sekondari, msisitizo sio matumizi yake, bali fomula zinawasilishwa ambazo wakati mwingine ni ngumu sana kuzielewa, jambo ambalo huwakatisha tamaa vijana walio wengi kuendelea na taaluma ya hisabati”, analaumu.
Anaongeza "mwanasoka, mwanamuziki, kwa kutaja wachache ni mfano wa kuigwa katika nchi kadhaa za Afrika. Hakika, sipingani na hilo, lakini unapaswa kuelewa kwamba hisabati ni uti wa mgongo wa sayansi, teknolojia na uhandisi wowote."
Anaamini kuwa serikali za Afrika zinapaswa kufanya zaidi katika kukuza STEM (Sayansi, Teknolojia, Elimu na Hisabati) ikiwa kweli zinataka kubadilisha mustakabali wa bara hili. Na hiyo inamaanisha "kutoa msaada mkubwa wa kifedha, kurahisisha mambo kwa watafiti".












