Wanamichezo bora wa kuangazia Duniani mwaka 2025

.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, Lamine Yamal
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kalenda ya michezo inapozidi kupamba moto mwaka wa 2025, ulimwengu unatazamiwa kuwa uwanja wa michezo kwa wapenda michezo, huku kukiwa na msururu wa matukio ya kusisimua na burudani za kila aina.

Kuanzia mashindano ya Riadha ya Dunia , michezo ya Ndondi na ligi kuu ya Uingereza, kuna burudani kwa kila mtu.

Ifuatayo ni orodha ya wanariadha wa kuangazia mwaka 2025

Lamine Yamal

Mchezaji wa Barcelona na Uhispania Lamine Yamal ameshinda tuzo ya Golden Boy 2024.

Tuzo hiyo iliyoanzishwa na gazeti la Italia la Tuttosport, hutolewa kwa mchezaji bora wa Ulaya kwa wanaume chini ya umri wa miaka 21, huku waandishi wa habari wakipiga kura kwa kutumia mfumo wa pointi.

Yamal, 17, alijiimarisha katika kikosi cha kwanza cha Barcelona msimu uliopita kabla ya kuisaidia Uhispania kushinda Euro 2024.

Winga huyo alifunga bao moja na kusaidia mengine manne huku akitajwa kuwa mchezaji chipukizi bora wa michuano hiyo.

Mnamo Oktoba Yamal alishinda Kombe la Kopa, zawadi sawa na iliyotolewa wakati wa sherehe ya Ballon d'Or ya 2024.

Yamal amefunga mabao sita na kutoa asisti nane katika mechi 16 za mashindano yote msimu huu.

Pia unaweza kusoma

Faith Kipyegon

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Faith Kipyegon wa Kenya

Bingwa wa dunia na michezo ya Olimpiki , Faith Kipyegon alikuwa na msimu mzuri mwaka 2023 aliposhinda mbio zake zote isipokuwa moja ya mbio zake na kuweka rekodi tatu za ulimwengu.

Kipyegon alivunja rekodi za dunia katika mbio za mita 1,500, 5,000 na maili hiyo kando na kushinda mara mbili dhahabu ya mita 1,500 na 5,000 kwenye Mashindano ya Dunia.

Pia alidai Tuzo la Ligi ya Diamond katika mkondo wa mwisho wa msimu, Prefontaine Classic, mafanikio ambayo yalimpa Tuzo ya Mwanariadha Bora wa Kike wa 2023.

Kuelekea 2025, Kipyegon anapendelea zaidi kushinda medali za dhahabu katika mbio za mita 1,500 na kuna matumaini kwamba rekodi zaidi zitaporomoka.

Noah Lyles

Noah Lyles ni mwanariadha wa Marekani ambaye alijulikana kama "mtu mwenye kasi zaidi duniani" baada ya kushinda medali tatu za dhahabu-katika mita 100, mita 200, na Relay ya mita 4 × 100-kwenye mashindano ya dunia ya 2023.

Noah Lyles pia alishinda mbio za mita 100 kwa wanaume kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2024 , akimshinda Kishane Thompson wa Jamaika kwa . 005 sekunde

Kylian Mbappe

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kylian Mbappe

Mchezo wa mshambuliaji wa Real Madrid Kylian Mbappe "uko chini" lakini ana dhamira ya kuvuka kipindi kigumu, kulingana na meneja Carlo Ancelotti.

Fowadi huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 25, ambaye alijiunga na Real kwa uhamisho wa bila malipo kutoka Paris St-Germain mwezi Julai, amekuwa na wakati mgumu sana tangu alipowasili Bernabeu.

"Mbappe yuko chini kama kila mtu mwingine, lakini ana ari ya kumaliza kipindi hiki," bosi wa Real Ancelotti aliambia mkutano wa wanahabari.

"Tatizo alilo nalo ni la kila mtu. Unaweza kumwelekeza Vinicius [Junior], Rodrygo au [Jude] Bellingham. Ni wakati mgumu kwa kila mtu."

Mchezaji huyo anatarajiwa kuimarika 2025 wakati ambapo atakuwa amefahamikiana vizuri kimchezo na wachezaji wenzake Real Madrid.

Beatrice Chebet

Beatrice Chebet ni mwanariadha wa Kenya wa mbio ndefu ambaye ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 na medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya 2024 katika mbio za mita 5000 na 10,000, mbali na kuwa mwanamke wa tatu katika historia kushinda mbio mbili tofauti kwenye michezo ya Olimpiki.

Mwaka 2022, Chebet alishinda medali za dhahabu katika mbio za mita 5000 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, Mashindano ya Afrika, na Ligi ya Almasi, na medali ya fedha katika mbio za mita 5000 kwenye Mashindano ya Dunia. Chebet pia alishinda medali za dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya 2023 na 2024.

Katika mashindano ya vijana ,Chebet alishinda medali za dhahabu katika mbio za mita 5000 kwenye Mashindano ya Dunia ya U20 ya IAAF 2018 na sehemu ya Wanawake ya Vijana ya Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika za 2019.

Gervonta Davis

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Gervonta Davis

Gervonta Bryant Davis anayejulikana pia kwa jina lake la utani "Tank", ni bondia mtaalamu wa Marekani. Ameshikilia taji la Chama cha Ngumi cha Dunia (WBA) uzani mwepesi tangu 2023, akiwa ameshikilia toleo la Kawaida kutoka 2019 hadi 2023. Pia alishikilia taji la Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF) uzani wa super feather mnamo 2017, taji la WBA super featherweight mara mbili kati ya 2018 na 2020, na taji la WBA super lightweight mwaka 2021.

Kufikia Mei 2024, Davis aliorodheshwa kama mchezaji wa pili bora duniani katika uzani mwepesi na ESPN, kwanza na Bodi ya Nafasi za Ndondi za Kimataifa, na pili na jarida la The Ring.

Amethibitisha kuwa taaluma yake inakaribia mwisho. Akiwa na rekodi nzuri ya mapigano 30 bila kushindwa na 28 ya mtoano, mpiganaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ametangaza kuwa ana mpango wa kustaafu mwaka 2025, na kuacha historia ambayo imewashangaza mashabiki na wataalam wengi

Victor Wembanyama

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Nyota wa San Antonio Spurs, Victor Wembanyama ameshinda tuzo ya mchezaji bora anayechipuka wa NBA mwaka huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ndiye Mfaransa wa kwanza kushinda tuzo hiyo baada ya kuwa na wastani wa pointi 21.4

Wembanyama, alipata kura zote 99 za nafasi ya kwanza.

Yeye ndiye Rookie wa kwanza kwa kauli moja tangu Karl-Anthony Towns mnamo 2016.

"Malengo yangu siku zote yalikuwa ni kuisaidia timu yangu kadri niwezavyo na kuwa bora kadri mwaka ulivyosonga," Wembanyama aliiambia TNT Sports.

Mchezaji wa timu Oklahoma City Thunder Chet Holmgren aliibuka wa pili na Brandon Miller wa Charlotte Hornets akashikilia nafasi ya tatu.

Letsile Tebogo

Letsile Tebogo ni mwanariadha kutoka Botswana. Alishinda medali ya dhahabu katika Olimpiki ya 2024 katika mashindano ya mbio za mita 200, na ushindi wake uliipata Botswana dhahabu ya kwanza ya Olimpiki . Pia alishinda medali ya fedha katika Mashindano ya Dunia ya 2023 katika mbio za mita 100 na kufuatiwa na medali ya shaba katika mbio za mita 200 siku tano baadaye.

Tebogo alishinda katika mbio za mita 100 na kushika nafasi ya pili katika mbio za mita 200 katika Mashindano yote mawili ya Riadha ya Dunia ya 2021 na 2022. Mwaka 2021, alikua mwanariadha wa kwanza wa Botswana kushinda taji la mita 100 katika kiwango chochote cha Ubingwa wa Dunia. Yeye ndiye bingwa wa Afrika wa mita 200 2022, na kuwa mshindi mwenye umri mdogo zaidi wa taji hili katika historia ya mashindano. Alishinda tuzo ya mwanamichezo bora wa dunia upande wa wanaume 2024.

Amos Serem

Mwanariadha Mkenya Amos Serem alisitisha mfululizo wa ushindi wa miaka 2 wa bingwa mara 2 wa Olimpiki Soufiane El Bakkali na kushinda taji lake la kwanza la Ligi ya Diamond la mbio za mita 3000 kuruka viunzi kwenye Fainali ya Allianz Memorial van Damme – Wanda Diamond League mjini Brussels..

Serem alimzidi El Bakkali kwa urahisi katika awamu ya mwisho na kushinda kwa saa 8:06.90. El bakali wa Morocco alimaliza katika nafasi ya pili kwa muda wa 8:08.60 huku Mohamed Amin Jhinaoui wa Tunisia (8:09.68) akimaliza wa tatu.

Amos Serem ana hamu ya kutwaa tena utawala wa Kenya katika mbio za kuruka viunzi mwaka wa 2025, lengo kuu likiwa ni kung'ara katika Mashindano ya Dunia huko Tokyo, Japan.

Daniel Dubois

Daniel Dubois ni mwanamasumbwi mtaalamu wa Uingereza. Ameshikilia taji la uzani mzito la Shirikisho la Ndondi za Kimataifa (IBF) tangu Juni 2024. Hapo awali, aliwahi kushikilia taji la uzito wa juu la Chama cha Ngumi cha Dunia (WBA) kutoka 2022 hadi 2023.

Katika ngazi ya mkoa, amewahi kushikilia ubingwa wa uzani mzito, pamoja na mataji ya Uingereza na Jumuiya ya Madola kutoka 2019 hadi 2020.

Akiwa mwanariadha, alikuwa bingwa mara tano wa kitaifa upande wa vijana na bingwa wa Uingereza. Dubois anajulikana kwa uwezo wake wa ngumi nzito akishinda mara 21 kati ya 22 kwa njia ya knockout.

Ushindi wake mkubwa dhidi ya Bingwa wa zamani wa uzani mzito zaidi duniani Anthony Joshua uliinua nyota yake.

Faith Cherotich

.

Chanzo cha picha, World Athletics

Maelezo ya picha, Faith Cherotich

Faith Cherotich ni mwanariadha wa Kenya ambaye ni mtaalamu wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi. Akiwa na umri wa miaka 17, alishinda nishani ya shaba katika Mashindano ya Riadha ya Dunia ya walio chini ya umri wa miaka 20 ya 2021 yaliyoandaliwa Nairobi.

Cherotich aliboresha shaba yake hadi dhahabu mwaka mmoja baadaye, na kushinda taji katika Mashindano ya Dunia ya U20 huko Cali. Mshindi wa medali ya shaba katika Olimpiki, Faith Cherotich alimshangaza bingwa wa Olimpiki na Dunia wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi, Winfred Yavi na kutwaa taji la Diamond League huko Allianz Memorial Van Damme - fainali ya mzunguko wa Diamond League 2024.