Je ‘Super Tuesday’ ni nini na kwanini ni muhimu?

Donald Trump anataka tena kuwani urais wa Marekani, na msururu wa kura katika kile kinachoitwa "Super Tuesday" ndio utakaoamua iwapo atamshinda mpinzani wake, Nikki Haley, na kuwa mgombea mteule wa Chama cha Republican.

Mshindi atapambana na rais wa sasa, Joe Biden, katika uchaguzi wa Novemba 2024.

Ni vyama gani vikuu Marekani?

Chama cha Joe Biden cha Democratic kiko Ikulu ya White House, na Republican ni chama cha upinzani.

Wanademokratic kwa ujumla wanaamini katika jamii huru na huwa na imani katika matumizi makubwa ya serikali.

Republican wana mrengo wa jamii ya kihafidhina na kwa kawaida hupendelea matumizi madogo ya serikali.

Inachukua muda gani kuchagua mgombea?

Wagombea huanza kujiweka mbele katika kampeni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa urais kuanza.

Trump amekuwa kiongozi katika Chama cha Republican tangu 2016, aliposhinda urais. Lakini, alishindwa na Joe Biden katika uchaguzi wa 2020.

Katika uchaguzi ujao wa urais mwaka 2024, Warepublican wanahitaji kuchagua mgombea – katika mchakato unaoitwa kura za mchujo.

Biden hatarajiwi kukabiliwa na upinzani wowote mkali katika uteuzi wa chama chama chake cha Democrat.

Kura za mchujo ni zipi?

Uchaguzi wa mchujo ni msururu wa chaguzi za majimbo na kisha kongamano la kitaifa.

Kila jimbo huwa na uchaguzi ili kumpigia kura mgombea mteule wa chama na mshindi wa jumla anatawazwa rasmi katika Kongamano la Kitaifa la Republican (RNC) - tukio kubwa la kisiasa Julai 2024.

Je, uchaguzi wa mchujo ukojo?

Jimbo linaweza kuchagua mgombea linayempendelea katika mojawapo ya njia mbili.

Takriban majimbo yote yanafanya chaguzi zao za mchujo kupitia kura ya siri, kama katika uchaguzi mkuu.

Lakini idadi ndogo ya majimbo huamua kwa kuhesabu watu waliopo au kuonyesha mkono juu.

Majimbo yana sheria tofauti kuhusu nani anayeweza kupiga kura - mara nyingi ni wanachama wa Chama cha Republican pekee.

Kulingana na kura anazoshinda, kila mgombea hupewa idadi fulani ya wajumbe kumwakilisha katika kongamano la kitaifa la Julai.

Upigaji kura kwa kawaida unaanza lini?

Upigaji ulianza Iowa mwezi Januari. Likafuatiwa na jimbo la New Hampshire.

Pamoja na Super Tuesday, kura za mwezi Machi ni pamoja na kura za mchujo za Carolina Kusini, Michigan na kura za vikao huko Nevada na Visiwa vya Virgin.

Super Tuesday ni nini?

Super Tuesday, 5 Machi, ndiyo siku kubwa zaidi ya kupiga kura.

Uchaguzi wa chama cha Republican hufanyika katika majimbo 15, yakiwemo yenye watu wengi zaidi - California na Texas - pamoja na eneo la Marekani la Samoa.

Ni siku moja, ambayo mara nyingi mgombea mteule huibuka mshindi.

Hata hivyo, Donald Trump tayari anaongoza akiwa na wajumbe 122 dhidi ya 24 wa Nikki Haley.

Upigaji kura utaendelea hadi Juni 2024 ikiwa atachagua kusalia kwenye kinyang'anyiro hicho.

Nani atashinda mchujo wa Republican?

Donald Trump anasalia kuwa mshindi hadi sasa, baada ya kushinda katika chaguzi zote sita za ambazo zimefanyika hadi sasa.

Kila ushindi wa Trump unailetea Marekani katika hatua karibu na marudiano kati ya rais huyo wa zamani na Rais wa sasa Joe Biden.

Trump atakuwa na changamoto nyingi akiwania Ikulu ya White House - akikabiliwa na mashtaka kadhaa ya uhalifu, likiwemo la kujaribu kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Anakanusha kufanya makosa na kusema ni mashtaka ya kisiasa.

Hata kama atahukumiwa au kufungwa jela, anaweza kusalia katika kinyang'anyiro cha kuwania Ikulu.

Wapinzani wa Trump

Nikki Haley, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, ndiye mpinzani pekee wa Trump aliyesalia.

Gavana wa Florida, Ron DeSantis alijiondoa katika kinyang'anyiro hicho na kumuunga mkono rais huyo wa zamani.

Wagombea wengine wa urais, akiwemo mfanyabiashara Mmarekani mwenye asili ya India, Vivek Ramaswamy na aliyekuwa gavana wa New Jersey, Chris Christie, pia walijiondoa katika kinyang'anyiro hicho.

Akiwa amepoteza mbele ya Trump - ikiwa ni pamoja na jimbo la nyumbani la Carolina Kusini, Haley anasema anasalia kwenye kinyang'anyiro hicho kwa sababu wapiga kura "wana haki ya kuchagua, sio uchaguzi wa mtindo wa Soviet wa mgombea mmoja pekee."

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi