Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maisha jirani na mgodi wa shaba na kobalti unaomilikiwa na China nchini DRC
- Author, Global China Unit
- Nafasi, BBC
Mapema mwaka huu, Ai Qing aliamshwa katikati ya usiku na zogo la hasira nje ya bweni lake kaskazini mwa Argentina.
Alichungulia nje ya dirisha na kuona wafanyakazi wa Argentina wakizunguka jengo na kuziba mlango kwa matairi ya moto.
"Ilikuwa inatisha kwa sababu niliona moto angani. Kulikuwa na ghasia," anasema Bi Ai, anayefanya kazi katika kampuni ya Kichina ya kuchimba lithiamu katika milima ya Andes, kwa ajili ya matumizi ya betri.
Maandamano hayo, yaliyochochewa na kufutwa kazi wafanyakazi kadhaa wa Argentina, ni moja tu ya kati ya matukio mengi ya msuguano kati ya wafanyabiashara wa China na jamii za wenyeji.
Miaka 10 iliyopita kampuni ya China ilinunua hisa za kwanza katika mradi wa uchimbaji lithiamu ya Argentina, Bolivia na Chile, nchi zenye hifadhi nyingi za lithiamu duniani.
Uwekezaji mwingine mkubwa wa China katika shughuli za uchimbaji madini wa ulifuata, kulingana na ripoti za mashirika, serikali na vyombo vya habari.
Kulingana na hisa zao, makampuni ya China sasa yanadhibiti wastani wa 33% ya lithiamu katika miradi inayozalisha madini hayo au katika miradi inayoendelea kujengwa.
Nguvu za China kwa sasa
Kitengo cha BBC Global China kimetambua miradi 62 ya uchimbaji madini duniani kote, ambapo makampuni ya China yana hisa, kuchimba lithiamu au kuchimba mojawapo ya madini mengine matatu muhimu kwa teknolojia ambayo ni rafiki kwa mazingira - cobalt, nikeli na manganese.
Zote zinatumika kutengeneza betri za lithiamu - zinazotumika katika magari ya umeme – ambapo pamoja na umeme wa jua, sasa magari hayo ni kipau mbele cha juu kwa viwanda vya China.
China imekuwa ikiongoza kwa muda mrefu katika kusafisha lithiamu na cobalt, na usambazaji wake wa kimataifa umefikia 72% na 68% mtawalia 2022, kulingana na taasisi ya Chatham House.
Uwezo wake wa kusafisha madini hayo na mengine muhimu kumeifanya China kuuza zaidi ya nusu ya magari ya umeme yaliyouzwa duniani kote mwaka 2023.
Ina asilimia 60 ya uwezo wa kimataifa kutengeneza mitambo ya umeme wa upepo, na inadhibiti 80% ya kila hatua katika mnyororo wa usambazaji wa umeme wa jua.
Jukumu la China katika sekta hiyo limezifanya bidhaa hizi kuwa nafuu na kupatikana duniani kote.
Lakini sio China pekee ambayo itahitaji kuchimba na kuchakata madini yanayohitajika kwa uchumi wa kijani. Umoja wa Mataifa unasema ikiwa dunia inataka kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kwa kiwango kikubwa hadi ifikapo 2050, matumizi ya bidhaa hizo lazima yaongezeke mara sita ifikapo 2040.
Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zote zimetengeneza mikakati, kupunguza utegemezi wao kwa vifaa vya China.
Lakini si kila kitu kiko sawa
Kadiri biashara za China zinavyozidi kupanuka, zimekabiliwa na tuhuma za unyanyasaji sawa na zile ambazo mara nyingi huelekezwa kwa wafanyabiashara wengine wa madini wa kimataifa.
Kwa Ai Qing, maandamano ya siku ile ya kuchoma matairi yalikuwa mwamko mbaya. Alitarajia maisha ya utulivu huko Argentina, lakini alijikuta akihusika katika usuluhishi wa migogoro kwa sababu ya kuzungumza Kihispania.
"Haikuwa rahisi," anasema. “Inabidi tuyaweke sawa mambo mengi, kama vile wasimamizi kuwafikiria wafanyakazi ni wavivu na wanategemea sana chama cha wafanyakazi, na jinsi wenyeji wanavyofikiri Wachina wako hapa kuwanyonya."
Shirika lisilo la serikali la Rasilimali, Biashara na Haki za Kibinadamu, liinasema shida kama hizo "sio za China pekee katika uchimbaji."
Mwaka jana lilichapisha ripoti iliyoorodhesha tuhuma 102 zilizotolewa dhidi ya kampuni za Kichina zinazohusika katika uchimbaji madini, kuanzia ukiukaji wa haki za wenyeji, kuharibu mifumo ikolojia na mazingira yasiyo salama ya kufanya kazi.
BBC imehesabu zaidi ya madai 40 ambayo yalitolewa mwaka 2023, na kuripotiwa na NGOs au kwenye vyombo vya habari.
Hali ilivyo DR Congo
Katika viunga vya mji wa Lubumbashi kusini kabisa mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Christophe Kabwita amekuwa akiongoza upinzani dhidi ya mgodi wa kobalti wa Ruashi, unaomilikiwa na Kundi la Jinchuan tangu 2011.
Anasema mgodi huo wa shimo, ulio umbali wa mita 500 kutoka juu, unaharibu maisha ya watu kwa kutumia vilipuzi kulipuka miamba mara mbili au tatu kwa wiki. Ving'ora hulia wakati ulipuaji unapokaribia kuanza, kama ishara kila mtu kuacha anachofanya na kujificha.
“Hata hali ya joto iweje, mvua inanyesha au upepo mkali unavuma, inabidi tuondoke majumbani mwetu na kwenda kwenye maeneo ya kujificha karibu na mgodi,” anasema.
‘Hilo ni kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wagonjwa na wanawake ambao wamejifungua, kwani hakuna mahali pengine salama,’’ anasema.
Mwaka 2017 msichana mdogo Katty Kabazo, aliripotiwa kufariki na jiwe lililoruka alipokuwa akirejea nyumbani kutoka shuleni, huku mawe mengine yakielezwa kutoboa mashimo kwenye kuta na paa za nyumba za wenyeji.
Msemaji kutoka mgodi wa Ruashi, Elisa Kalasa, alikiri "mtoto mmoja mdogo alikuwa katika eneo hilo - hakutakiwa kuwepo na aliathiriwa na miamba hiyo".
Alisema tangu wakati huo "tumeboresha teknolojia, na sasa tuna aina ya ulipuaji ambapo hakuna mawe yanayoruka tena".
BBC ilizungumza na meneja usindikaji katika kampuni hiyo, Patrick Tshisand, anasema:
"Tukichimba madini tunatumia vilipuzi. Vilipuzi vinaweza kusababisha mawe kuruka, yanaweza kuishia kwenye maeneo ya jamii kwa sababu jamii iko karibu sana na mgodi. Hivyo tulipata ajali sababu hiyo."
Bi Kalasa anasema kati ya 2006 na 2012 kampuni hiyo ililipa fidia zaidi ya familia 300 ili kuhama mbali na mgodi huo.
Hali nchini Indonesia
Katika kisiwa cha mbali cha Obi cha Indonesia, mgodi unaomilikiwa na kampuni ya Kichina, Lygend Resources and Technology, na kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Indonesia ya Harita Group umeharibu misitu inayozunguka kijiji cha Kawasi.
Jatam, shirika linalosimamia uchimbaji madini, linasema wanakijiji wamekuwa chini ya shinikizo kuhama na kukubali fidia ya serikali.
Makumi ya familia zimekataa kuhama, wakisema kile kinachotolewa ni kidogo. Kutokana na hali hiyo, wengine wanasema wametishiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa madai ya kuvuruga mradi wenye umuhimu wa kimkakati kwa taifa.
Jatam inasema misitu mizee imekatwa ili kutoa nafasi kwa mgodi huo na wamerikodi jinsi mito na bahari zilivyojaa takataka, na kuchafua mazingira ya baharini.
"Maji kutoka mtoni hayanyweki sasa, yamechafuliwa sana, na bahari ambayo kwa kawaida huwa na rangi ya samawati, huwa nyekundu wakati mvua inaponyesha," anasema Nur Hayati, mwalimu anayeishi katika kijiji cha Kawasi.
Wanajeshi wa Indonesia wametumwa kisiwani kulinda mgodi huo na BBC ilipotembelea hivi karibuni, kulikuwa na ongezeko kubwa la wanajeshi.
Jatam inadai askari wanatumiwa kuwatisha, na hata kuwashambulia, watu wanaozungumza kukosoa mgodi huo.
Bi Nur anasema jamii yake inahisi jeshi liko pale "kulinda masilahi ya mgodi, sio ustawi wa watu wao."
Msemaji wa jeshi huko Jakarta anasema madai ya vitisho "hayawezi kuthibitishwa na wanajeshi wako huko kulinda mgodi, hawapo kuingiliana moja kwa moja na wenyeji."
Katika taarifa yake, alidai uhamishaji wa wanakijiji ili kupisha mgodi huo umesimamiwa na polisi kwa njia ya amani na adabu.
Bi Nur alikuwa miongoni mwa kundi la wanakijiji waliosafiri hadi mji mkuu wa Indonesia, Jakarta, Juni 2018, kupinga athari za mgodi huo.
Lakini mwakilishi wa serikali ya eneo hilo, Samsu Abubakar, aliiambia BBC hakuna malalamiko yaliyopokelewa kutoka kwa umma kuhusu uharibifu wa mazingira.
Pia alituonyesha ripoti rasmi ambayo ilihitimisha kuwa Harita Group imekuwa "ikitii utunzaji wa mazingira na majukumu ya ufuatiliaji".
Harita yenyewe ilituambia "inafuata kikamilifu kanuni za maadili ya biashara na sheria za mitaa" na "inaendelea kufanya kazi kushughulikia na kupunguza athari zozote mbaya."
Ilidai haijasababisha uharibifu mkubwa wa misitu, ilifuatilia chanzo cha maji ya kunywa, na vipimo huru vimethibitisha maji yanakidhi viwango vya ubora wa serikali.
Imeongeza kuwa haijaondoa watu kwa lazima au kununua ardhi isivyo haki na haikumtisha mtu yeyote.
Jitihada za kupunguza tatizo
Mwaka mmoja uliopita, shirika la biashara ya madini la China, linalojulikana kama CCCMC, lilianza kuweka utaratibu wa malalamiko, uliokusudiwa kutatua malalamiko yaliyotolewa dhidi ya miradi ya uchimbaji madini inayomilikiwa na China.
‘Kampuni zenyewe hazina uwezo - wa kitamaduni na kilugha kuingiliana na jamii za wenyeji au mashirika ya kiraia,” anasema msemaji, Lelia Li.
Wakati uhiriki wa China katika shughuli za uchimbaji madini unaonekana dhahiri kuongezeka - utaratibu ulioanzishwa na CCCMC bado haufanyi kazi kikamilifu.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah