Madaktari walivyookoa maisha ya msichana wa miaka 9 aliyepigwa mshale wa moyo

Chanzo cha picha, MINISTRY OF PUBLIC HEALTH OF CAMEROON
- Author, Jean Charles Biyo'o Ella
- Nafasi, BBC
Maisha ya Roukayatou Sali hayako tena hatarini. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 9 alifanyiwa upasuaji wa mafanikio na timu ya wataalamu 15 katika hospitali kuu ya Yaoundé.
Si si mrefu Sali Adama, 57, na binti yake Roukayatou watarejea Garoua kaskazini mwa Cameroon kuendelea na matibabu huko, kabla ya kurejea nyumbani kwao kabisa.
Mwanafunzi huyo anayesoma shule ya serikali ya Adai katika wilaya ya Moulvoudaï - takribani kilomita 1,350 kutoka Yaoundé aliponea chupuchupu.
Mchana wa Oktoba 29, Roukayatou alipokuwa akikimbia kutoka nje ya nyumba yao, alikutana uso kwa uso na mshale uliolengwa na mmoja wa kaka zake.
Kaka huyo alikuwa akicheza mchezo wa kurusha mishale pamoja na ndugu wengine, kulingana na maelezo ya baba wa Roukayatou kwa BBC.
Mshale ulimpiga Roukayatou katika moyo - mshale wa sentimita 15, wanaeleza madaktari waliookoa maisha yake.
BBC iliweza kumuona msichana huyo akiwa hospitali, na kukutana na daktari wake katika Hospitali Kuu ya Yaoundé.
Operesheni ya Hatari

Chanzo cha picha, MINISTRY OF PUBLIC HEALTH OF CAMEROON
Katika hospitali kuu, kubwa na yenye vifaa bora zaidi katika mji mkuu wa Cameroon, ndipo Daktari Kobe Zephanie alipomkagua mgonjwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huku akiwa macho, daktari-mpasuaji anamuuliza maswali machache kwa lugha ya Kifulfulde. Lugha ya wenyeji inayozungumzwa sehemu ya kaskazini ya Cameroon.
Daktari anasimulia, “Mgonjwa alifika hapa mshale ukiwa bado uko kwenye moyo mwake. Mshale huu usingeweza kuondolewa kabla ya kufanyiwa upasuaji, vinginevyo angekufa."
Kwa mujibu wa Daktari Kobe, Roukayatou alifika Yaoundé, baada ya kupata huduma za awali katika hospitali ya Garoua, ambapo aliongezewa damu na kufanyiwa mambo mengine muhimu ili kuboresha hali yake kabla ya kuhamishiwa Yaoundé.
"Ilikuwa operesheni kubwa iliyohitaji vifaa maalumu na kuusimamisha moyo, kabla ya kuanza upasuaji."
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, sehemu ya chuma ya mshale iliingia kwenye moyo ilikuwa na miba pande mbili na ingeweza kupasua vyumba vya moyo ikiwa ungetolewa kwa mikono bila ujuzi.
"Kwa hivyo ilitubidi kuanza mchakato wa kuweka mzunguko wa damu nje ya mwili, kusimamisha mapigo ya moyo, kufungua vyumba vya moyo na kuondoa mshale huu wa sentimita 15, ambao karibu theluthi moja ilizama moyoni," anasimulia.
Mshikamano

Isingewezekana kumsafirisha Roukayatou kutoka Garoua hadi Yaoundé kwa kutumia barabara. Sio tu kwamba umbali kati ya mji mkuu na mkoa huo wa Kaskazini ni urefu wa kilomita 1108 tu, lakini pia barabara iko katika hali mbaya.
Siku mbili za kusafiri, msichana huyo asingefike Yaoundé akiwa hai. Kutokana na hilo, mlolongo mrefu wa mshikamano ukaanzishwa.
Wakfu wa Afya wa Cameroon ulifadhili safari ya mtoto na daktari anayeandamana naye. Watu wengine wenye mapenzi mema walilipia tiketi ya ndege ya baba wa mtoto.
“Tuliwasiliana pia na wasimamizi wa hospitali, ambao pia walikuwa wakijipanga kutafuta suluhu ya haraka. Kwa hiyo shukrani kwa mshikamano huu na asubuhi ya Jumatatu Oktoba 30, mgonjwa alipanda ndege kutoka Garoua hadi Yaoundé,” anaeleza Dkt. Kobe.
Roukayatou alivyopigwa mshale

Chanzo cha picha, MINISTRY OF PUBLIC HEALTH OF CAMEROON
Kwa mujibu wa Sali Adama, babake Roukayatou, binti yake hakuwa amelengwa makusudi.
“Kaka zake wakubwa walikuwa wanacheza na mishale uani na mimi nilikuwa najiandaa kwenda shambani. Bila kujua, Rakayatou alikuwa akikimbia nje ya nyumba na ndipo akakutana na mshale uliorushwa na kaka yake. Kwa bahati mbaya ukampiga moyoni.’’
“Nilitaka kwanza kuondoa mshale huu mwenyewe. Lakini niliogopa. Na ndipo nikaamua kumpeleka katika hospitali ya mkoa huko Garoua.’’














