Profesa wa Nigeria anayepata pesa nyingi kwa kuchomelea vyuma

.

Kabir Abu Bilal sio profesa wa kawaida wa chuo kikuu cha Nigeria - ana kazi ya pili ya kuchomelea vyuma kaskazini ya jiji la Zaria.

Uchomeleaji unaonekana sana kama kazi duni kote nchini Nigeria na amewashangaza wengi - hasa wafanyakazi wenzake - kwa kufungua karakana yake ya uchomeleaji.

"Sioni aibu kuwa ninafanya kazi ya uchomeleaji licha ya kuwa profesa," anaambia BBC. "Ninapata pesa zaidi kutokana na uchomaji vyuma."

Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 50 anafundisha na kusimamia wanafunzi wa utafiti katika kitivo cha uhandisi katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello, chuo kikuu kikubwa zaidi cha Nigeria na mojawapo ya vyuo vikuu vyake vya hadhi.

Amefanya kazi huko kwa miaka 18 na kuchapisha vitabu kadhaa juu ya fizikia na uhandisi wa umeme.

Msomi mwenzake, Prof Yusuf Jubril, anaeleza kuwa wenzao huona jambo la ajabu: “Jamii inatufanya tufikirie kuwa mtu ni mkubwa sana kwa majukumu fulani na si kweli.

"Anachofanya si cha kufedhehesha bali ni cha kupongezwa, na natumai wengine watajifunza kutoka kwake."

.
Maelezo ya picha, Mapato yake kutokana na uchomeleaji yamemwezesha profesa huyo kununua gari aina ya Mercedes-Benz

Prof Abu Bilal anakubali kwamba watu, hasa wahitimu, wanahitaji kuwa wazi zaidi kuhusu jinsi wanavyoendesha maisha yao.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Elimu isimzuie mtu kufanya kazi za namna hii, nashangaa kuna watu wenye shahada za kwanza wanaona kazi kama hii ni udhalilishaji."

Maneno yake yana uzito - kwani kulingana na Ripoti ya Wahitimu ya Sutern's Nigeria, zaidi ya 40% ya wahitimu wanashindwa kupata kazi nchini Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Alifungua karakana ndogo huko Zaria karibu miongo miwili iliyopita.

Mnamo 2022, mwaka mmoja baada ya kupandishwa cheo na kuwa profesa, alihamia kwenye majengo makubwa akiwa amepata biashara nyingi katika mji wa chuo kikuu.

Hii imemwezesha kununua vifaa zaidi na kufanya kazi kubwa zaidi, huku wateja wakimtaka atengeneze vitu kama vile milango ya chuma na fremu za madirisha.

“Nafanya kazi hiyo hata iwe ndogo kiasi gani, hata ikiwa ni mlango mmoja nitauchomelea kwa furaha ili nilipwe,” anasema.

Tangu akiwa mtoto, profesa huyo anasema, amekuwa akipenda kutenganisha na kuweka pamoja vifaa na vitu kama redio, ambavyo vilimvutia kwenye kazi yake.

“Kwa bahati mbaya niligundua uhandisi hapa umejikita zaidi kinadharia na nilihitaji mahali pa kujieleza,” anasema.

"Hamu hiyo ilinisukuma kuanza karakana hii ya uchomeleaji."

Sio tu kwamba karakana imekidhi haja yake ya kuchafua mikono yake, lakini imemsaidia sana katika masuala ya kifedha.

Wasomi nchini Nigeria kwa muda mrefu wametatizika kupata mishahara ya kawaida, wengi wao wakipata kati ya naira 350,000 ($390; £305) na 500,000 ($555; £435) kwa mwezi - na mara nyingi kuna vita vya muda mrefu na serikali kupata nyongeza ya mishahara.

Prof Abu Bilal anasema kazi yake ya uchomeleaji imemwezesha kujitegemea zaidi na hata ameweza kununua gari la kutegemewa zaidi - Mercedes.

Na pia amesaidia hata wale ambao walichukia kazi yake.

"Wahadhiri wa vyuo vikuu walipogoma kwa miezi minane mwaka wa 2022 na hatukulipwa, siku zote nilikuwa na pesa kwa sababu ya kazi hii na wenzangu wachache walikuja kwangu kuomba msaada."

Prof Abu Bilal anatumai kuwatia moyo watu wengine kufanya kazi kama anazofanya.

.

Ana wanafunzi 10 - wenye umri wa kati ya miaka 12 na 20 - katika karakana yake ambapo anawafundisha ujuzi wa biashara hiyo.

Wale ambao hawako shuleni wakati wa mchana huwa kwenye karakana wakati yeye amekwenda kufundisha kikuu.

Kujifunza huwa kunachukua takriban mwaka mmoja - halafu wanapokuwa na ujuzi wanaweza kwenda kuanzisha biashara zao.

"Nimejifunza mengi sana nikiwa kwenye karakana, naweza kuunganisha vitu vingi pamoja sasa," Jibril Adam mwenye umri wa miaka 18 alisema.

"Hata kama mwanafunzi, anatupa naira 10,000 kila mwezi na matumizi ya kila siku na chakula."

Msomi huyo pia amedhamiria kwamba watoto wake watano wasiwe wabaguzi wa masomo: "Mimi huwaleta hapa wikendi nyingi ili kuona jinsi inavyofanywa. Nataka wajifunze ili siku moja waweze kuifanya."

Kwa Prof Abu Bilal taaluma yake ya pamoja inamfaa kikamilifu, kwani anaweza kukubali jukumu lake la kufundisha katika nyanja zote mbili: "Ninapenda kutoa maarifa."