Vita vya Ukraine: Makombora ya msaada ya GLSDB kwa Ukraine yenye uwezo wa kupiga umbali wa 150km kuleta mapinduzi?

Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Marekani inasema msaada wa ziada wa kijeshi kwa Ukraine wenye thamani ya $2.2bn (£1.83bn) utajumuisha makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kuongeza maradufu uwezo wake wa mashambulizi.

Nyongeza hiyo inafikisha jumla ya misaada ya kijeshi iliyotolewa kwa Ukraine kufikia zaidi ya dola $29.3bn (£24.31bn) tangu Februari 2022.

Msaada huu wa sasa unajumuisha makombora ya ardhini ya GLSDB ambayo yanaweza kulenga shabaha umbali wa kilomita 150 (maili 93).

Lakini maafisa walikataa uvumi kwamba silaha hizo zinaweza kutumika kushambulia sehemu za Crimea iliyotwaliwa na Urusi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Inapokuja kuhusu mipango ya Ukraine juu ya operesheni, ni wazi kwamba huo ni uamuzi wao," msemaji wa Pentagon Brig General Pat Ryder aliwaambia waandishi wa habari.

"Hii inawapa uwezo wa masafa marefu, uwezo wa kuzima moto wa masafa marefu, ambao utawawezesha, tena, kufanya shughuli za kulinda nchi yao na kurudisha eneo lao huru, maeneo yanayokaliwa na Urusi."

Urusi iliitwaa Peninsula ya Crimea kwa njia isiyo halali mnamo 2014 na inaiona kuwa sehemu ya eneo lake. Lakini imekuwa chini ya mapambano ya hapa na pale kutoka kwa vikosi vya Ukraine katika miezi ya hivi karibuni.

Mataifa ya Magharibi mara kwa mara yamekataa kuipatia Ukraine silaha za nguvu - kama vile ndege za kivita - ambazo inaweza kuzitumia na kushambulia ardhi ya Urusi.

Katika ujumbe wa Twitter, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliishukuru Marekani na Rais Joe Biden kwa msaada huo wa ziada.

"Kadiri silaha zetu zinavyokuwa za masafa marefu na jinsi wanajeshi wetu wanavyosonga mbele, ndivyo uchokozi wa kikatili wa Urusi utakavyokoma," Bw Zelensky aliandika. "Pamoja na [Marekani] tunasimama dhidi ya ugaidi."

Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Hapo awali, silaha ya masafa marefu zaidi ya Ukraine ilikuwa mfumo wa roketi wa Himars, ambao unaweza kulenga shabaha kwa umbali wa hadi 80km (maili 50). Kyiv ilitumia mfumo huo wakati wa uvamizi kusini na mashariki mwaka jana.

GLSDB pia inavipa vikosi vya Ukraine uwezo wa kushambulia popote katika mikoa inayokaliwa na Urusi ya Donbas, Zaporizhzhia na Kherson. Pia inaruhusu Ukraine kutishia njia za usambazaji wa silaha za Urusi katika mashariki.

Imetengenezwa na Boeing na Saab, GLSDB ni roketi ya kuruka yenye bomu ndogo, yenye uwezo wa kulenga shabaha ndani ya mita ilipo.

Na inaweza kurushwa kutoka kwa mifumo mbalimbali ya silaha, ikiwa ni pamoja na mifumo ya Himars na M270 MLRS ambayo tayari inatumika nchini Ukraine. Hata hivyo, Pentagon na Boeing walikataa kutoa maoni yao juu ya tarehe za utoaji wa mfumo huo au makombora hayo, huku baadhi ya ripoti zikipendekeza kuwa inaweza kuchukua hadi miezi tisa kabla ya kufika Ukraine.

Msaada huo mpya - ambao pia utajumuisha makombora ya ziada ya Himars na mifumo 250 ya kuzuia mashambulizi - inakuja huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kwamba mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichukua hatua za polepole sana kutoa msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine.

"GLSDB ilipaswa kuidhinishwa msimu uliopita, Mwenyekiti wa Huduma za Silaha za Baraza la Wawakilishi la Marekani Mike Rogers alisema katika ujumbe wa Twitter. "Kutoidhinishwa inacheleweshwa kufikia mikononi mwa Ukraine kumsambaratisha Mrusi."

Katika siku za hivi karibuni, ripoti zimeibuka kuwa mashambulizi ya Urusi katika eneo la mashariki la Donbas yamekuwa yakishika kasi, huku wanablogu wanaoiunga mkono Kremlin wakipendekeza kuwa mji wa Bakhmut, ambao ni kitovu cha mashambulizi ya Urusi, umezingirwa kutoka pande tatu.

Lakini Rais Zelensky alisema majeshi yake yamejikita kuzunguka mji huo na hatausalimisha kwa mashambulio ya Urusi.