Kwa nini Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinakataa kupeleka ndege za F-16 Ukraine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Joe Biden alifutilia mbali mpango wa kutumwa kwa ndege za kivita za F-16 nchini Ukraine licha ya ombi la msaada wa haraka wa silaha za anga kutoka kwa serikali ya Kyiv.
Alipoulizwa Jumatatu kama angetuma ndege za kivita, rais alijibu kwa sauti kubwa "hapana."
Kukataliwa kunakuja wiki moja baada ya Washington kutangaza usafirishaji wa vifaru 31 aina ya Abrams kwenda Ukraine, ambavyo kwa mujibu wa Biden vinafaa zaidi, pamoja na magari mengine aina ya M88.
Hofu ya kuongezeka kwa mzozo zaidi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na mamlaka ya kijeshi ya nchi hiyo wanaamini kuwa ni muhimu kuondoa miiko ya kutumwa kwa ndege, lakini Marekani na baadhi ya washirika wake wanahofia kuwa hii itasababisha kuongezeka kwa hatari zaidi ya mzozo na Urusi, ambayo ina hazina kubwa ya silaha za nyuklia.
"Tangu kuanza kwa vita, kumekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa mzozo zaidi, ambapo inaweza kusababisha Moscow kuchukua hatua kali zaidi," Michael Desch, profesa wa uhusiano wa kimataifa na mkurugenzi, anaiambia BBC kutoka Kituo cha Usalama wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Notre Dame huko Indiana, Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Vladimir Putin mara kwa mara imekuwa ikiishutumu NATO kwa kuendesha vita vya "wakala" dhidi ya nchi yake na imeonya kama itaongezeka zaidi kunaweza kuzua mzozo zaidi wa nyuklia.
Msemaji wa Jeshi la Wana anga la Ukrain Yuriy Ihnat aliambia chombo cha ndani cha Ukrainska Pravda Jumanne kwamba Kyiv inahitaji hadi ndege 200 za kivita za aina mbalimbali (kama vile F-16s) kuweza kulinda anga yake.
Alisema kuwa kwa sasa Urusi inaizidi Ukraine mara tano hadi sita katika idadi ya ndege za kivita ilizonazo.
Hizi ni ndege maalum
Mtaalam huyo pia anaamini kwamba sababu nyingine ya Marekani kukataa kutuma ndege aina ya F-16 kwenda Ukraine ni shabaha zake za zaidi ya kilomita 4,000 , ambayo ingewafanya Waukraine kufanya kazi nje ya mipaka yao.
"Haijazungumzwa sana, lakini pia kuna wasiwasi kwamba Waukraine wanaweza kujiondoa haraka juu ya kile ambacho Marekani iko tayari kuunga mkono, na njia moja ya kuhakikisha kuwa hawatafanya hivyo ni kudhibiti mifumo ya silaha inayowahudumia," anasema.
Kwa wasomi, ikiwa Ukraine ina rasilimali zinazoiruhusu kushambulia maeneo lengwa nchini Urusi, maelfu ya kilomita kutoka mpakani, kuna uwezekano mkubwa wa mzozo huo kuongezeka zaidi kwa viwango vya hatari zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
“Mfano mzuri ni mfumo wa roketi za mbali za HiMars, ambazo zipo za aina mbalimbali na tumekuwa tukisita kuwapa zile za masafa marefu kwa sababu zingekuwa na uwezo wa kugonga shabaha ndani ya Urusi,” anasema.
F-16 ni ndege ya kivita ambayo, "hata bila ya tenki la mafuta, ina uwezo wa kutosha kushambulia ndani kabisa ya Urusi," anasema.
Kwa kuongezea, ndege hizo zilizoundwa na Marekani ni bora zaidi ya zile za enzi ya Soviet za MiG ambazo Ukraine inazitumia leo, zilizotengenezwa kabla ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa USSR mnamo 1991.
F-16 Fighting Falcon inachukuliwa kuwa mojawapo ya ndege za kivita zinazotegemewa duniani na hutumiwa pia na nchi nyingine zikiwemo Ubelgiji na Pakistan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Inaweza kupakiwa na mabomu na makombora ya kuongozwa, na ina uwezo wa kuruka kwa kasi ya 1,500 mph, kulingana na Jeshi la Anga la Merika.
Uwezo wa kulenga wa F-16 ungeruhusu Ukraine kushirikisha vikosi vya Urusi kwa usahihi zaidi katika hali zote za hali ya hewa na usiku.
Je ndege hizi zingeleta tofauti gani Ukraine?
Ukraine inadai kuwa ndege za kivita zenye uwezo wa hali ya juu zinaweza kusaidia kulinda anga yake dhidi ya mashambulizi ya Urusi, ingawa wataalam wanahoji kama inaweza kuwa kipengele muhimu katika vita hivyo.
"Kwa upande wowote hakuna ndege zinazofanya jukumu muhimu katika operesheni za ardhini. Kwa mfano, Warusi wanatumia mabomu mengi makubwa na makombora ya cruise au makombora ya hypersonic, na kwa upande wa Ukraine pia inafanya hivyo," Desch anatathmini.
Anasema kuwa "mtandao wa ulinzi wa anga katika pande zote mbili ni mkubwa sana na ni vigumu sana kwa ndege za kivita kuukwepa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika hali hii, F-16 "labda inaweza kuwa na ufanisi zaidi kuliko ndege zingine" ingawa bila kuleta mabadiliko katika kipindi cha mzozo, kulingana na mchambuzi.
Ikiwa vyovyote, Biden amekataa mara kwa mara maombi ya Ukraine ya ndege, badala yake analenga kutoa msaada wa kijeshi katika maeneo mengine.
Baadhi ya washirika wake wa Magharibi, hata hivyo, wametoa maoni tofauti.
Mgawanyiko huko Uropa
Siku ya Jumatatu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron hakukataa kutuma ndege kwa Ukraine, ingawa alihitimisha kwa kusema kwamba hii haipaswi kusababisha kuongezeka kwa mvutano au kupunguza uwezo wa ulinzi wa nchi yake mwenyewe.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov, yuko Paris, ambako anapanga kujadili suala hili na Macron na makamanda wa kijeshi wa Ufaransa.
Poland, mshirika mwingine muhimu wa Ukraine, pia haijakaa kupeleka F-16s kwa Kyiv.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alisema kwamba itawezekana tu "kwa uratibu kamili" na wanachama wengine wa NATO.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Melnyk alitoa wito kwa washirika hao kuunda "muungano wa ndege za kivita" ili kuipatia Ukraine Eurofighters, Tornados, French Rafales na Gripens za Sweden.

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Uingereza ilitangaza Jumanne kwamba haikuwa na taarifa kuhusu maombi yoyote rasmi ya ndege hizo kutoka Ukraine.
"Ndege za Typhoon na F-35 za Uingereza ni za kisasa sana na huchukua miezi kadhaa kujifunza kuzirusha," msemaji wa waziri mkuu Rishi Sunak alisema.
"Tunaamini kwamba si jambo linalowezekana kupeleka ndege hizo Ukraine", alisema.
Alihakikisha, hata hivyo, kwamba Sunak "amefanya majadiliano ya kina na washauri wa kijeshi" na "hitimisho ni kwamba, kutokana na faida ya idadi ya idadi ya ndege kwa Urusi, vita vya kudumu vya mvutano havitafaifaidisha Ukraine."
Ujerumani kwa upande wake pia imedokeza kuwa haitatuma ndege za kivita nchini Ukraine.














