Bobi avunja rekodi ya dunia ya mbwa mwenye umri mkubwa zaidi

Bobi akiwa na cheti chake cha Rekodi ya Dunia ya Guinness

Chanzo cha picha, Guinness World Records

Mbwa wa Ureno mwenye umri wa miaka 30 ametajwa kuwa ndiye mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutokea duniani na Guinness World Records - akiipiku rekodi iliyodumu kwa karne moja.

Bobi ni aina safi ya Rafeiro do Alentejo - aina ambayo ina wastani wa kuishi miaka 12 hadi 14.

Mbwa wa zamani zaidi kuwahi kutokea alikuwa Bluey wa Australia, ambaye alikufa mnamo 1939 akiwa na umri wa miaka 29 na miezi mitano.

Kufikia Februari 1, Bobi alikuwa na umri wa miaka 30 na siku 226, na inasemekana kuwa anaendelea vyema na umri wake.

Uzee wake mkubwa umethibitishwa na hifadhidata ya wanyama kipenzi ya serikali ya Ureno, ambayo inasimamiwa na Muungano wa Kitaifa wa Madaktari wa Mifugo, kwa mujibu wa Guinness World Records.

Ameishi maisha yake yote na familia ya Costa katika kijiji cha Conqueiros, karibu na pwani ya magharibi ya Ureno, baada ya kuzaliwa na ndugu watatu.

Leonel Costa, ambaye alikuwa na umri wa miaka minane wakati huo, alisema wazazi wake walikuwa na wanyama wengi na ilimbidi kuwaweka chini watoto hao, lakini Bobi alitoroka.

Mbwa akiwa na paka

Chanzo cha picha, Guinness World Records

Leonel na kaka zake walificha uwepo wa mbwa kutoka kwa wazazi wao hadi alipogunduliwa na kuwa sehemu ya familia, ambao walimlisha chakula sawa wanachokula.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kati ya kopo la chakula cha wanyama au kipande cha nyama, Bobi hasiti na kuchagua chakula chetu," alisema Bw Costa, ambaye kila mara huloweka chakula hicho majini ili kuondoa viungo vingi.

Kando na hofu ya mwaka wa 2018 alipokuwa amelazwa hospitalini baada ya kuanguka ghafla kutokana na kushindwa kupumua, Bw Costa anasema Bobi amefurahia maisha yasiyo na matatizo na anaamini kuwa siri ya maisha yake marefu ni “mazingira tulivu na yenye amani” anayoishi.

Inaweza pia kuwa kwenye damu - mamake Bobi anaishi hadi umri wa miaka 18.

Hata hivyo, muda umemkabili Bobi, ambaye sasa ana matatizo ya kutembea na macho kuwa mabaya zaidi.

Bw Costa anasema Bobi ndiye "mwisho wa kizazi kirefu cha wanyama" katika familia ya Costa na anamtaja kama "mmoja wa aina yake."

Kutawazwa kwa Bobi kama mbwa mzee zaidi kuwahi kutokea wiki mbili tu baada ya Guinness World Record kumtaja mbwa mwingine, Spike the Chihuahua, kama mbwa mwenye umri mkubwa zaidi, akiwa na umri wa miaka 23.

Guinness imesasisha rekodi zake tangu wakati huo, na kumtangaza Bobi kuwa mbwa mzee zaidi kuishi, na mbwa mzee zaidi kuwahi kutokea.