Je, mkopo wa dola bilioni tatu wa IMF utatatua mgogoro wa kiuchumi wa Ghana?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ghana, mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa dhahabu na kakao duniani, inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea, huku bei ya bidhaa ikipanda kwa wastani wa asilimia 41 mwaka uliopita.

Nchi hiyo sasa imetia saini mpango mpya wa uokoaji wa thamani ya dola bilioni tatu na Shirika la Fedha Duniani (IMF) katika kipindi cha miaka mitatu ili kusaidia kupunguza matatizo hayo na inatarajiwa kupokea awamu ya kwanza ya dola milioni 600 hivi karibuni, lakini ni je, fedha hizo zitaisaidia kujikwamua kiuchumi?

Kwa nini uchumi uko katika hali mbaya hivi?

Ghana, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikionekana kuwa mojawapo ya nchi zinazoendeshwa vyema zaidi barani Afrika, imekuwa ikijitahidi kujikwamua kutokana na athari za janga la kimataifa la Covid na vita nchini Ukraine.

Upinzani pia unalaumu mzozo huo kwa kile unachokiita "usimamizi mbaya" wa uchumi - madai ambayo serikali imekanusha.

Kiwango cha kupanda kwa bei ya bidhaa, au mfumuko wa bei, kinaelekea kushuka, lakini bado kiko juu sana kwa 41% na familia nyingi zinapambana kujikimu kimaisha.

Ukubwa wa deni la Ghana sasa ni karibu sawa na jumla ya thamani ya mwaka ya uchumi wake. Serikali ilishindwa kulipa mikopo yake, na ilibidi ipange upya deni lake na wakopeshaji ili kufuzu kwa mkopo wa IMF.

Hazina ya fedha za kigeni imesalia tupu, na hivyo kufanya kuwa vigumu kulipia bidhaa kutoka nje ambazo kwa kawaida bei yake ni dola za Marekani.

Ni katika muktadha huu ambapo Waghana wengi wamekuwa wakisubiri kwa hamu mpango huu wa uokoaji wa IMF.

Lakini hii ni mara ya 17 tangu uhuru zaidi ya miongo sita iliyopita ambapo Ghana imeamua kuchukua mpango wa IMF.

Je, mkopo wa IMF utaleta mabadiliko yoyote?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa kakao duniani na mzalishaji mkuu wa dhahabu barani Afrika, tatizo la msingi la Ghana ni kwamba haipati mapato ya kutosha kupitia mauzo ya nje ili kulipia kila kitu inachoagiza kutoka nje.

Hii inajulikana kama nakisi ya salio la malipo na ndiyo kiasi ambacho mkopo wa IMF umeundwa kusaidia. Lakini si hayo tu.

Mpango huo pia unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha uthabiti wa sarafu ya ndani. Haya yote yatawanufaisha Waghana wa kawaida kupitia bei thabiti za bidhaa za kimsingi zikiwemo zinazoagizwa kutoka nje.

Imeonekana kuwa hatari kuikopesha Ghana, lakini kwa mpango mpya wa IMF kuna matumaini ya nchi hiyo kukopa tena ili kutekeleza sera zake.

Washirika wa maendeleo ikiwwa ni pamoja na Benki ya Dunia wameahidi kuisaidia nchi hiyo kujikwamua kiuchumi, huku wawekezaji sasa wakionekana kurejea bila hofu ya kupoteza fedha zao.

Hata hivyo, ukizingatia mipango iliyopita kupata mkopo wa IMF sio ishara ya kutatua matatizo ya muda mrefu ya kiuchumi ya nchi.

Ghana ilijikwamua kutoka kwa mpango wa mwisho wa IMF mwaka wa 2019 na tayari inaomba pesa zaidi.

Wachambuzi wamehusisha mtindo huu wa kawaida na usimamizi mbovu wa serikali zilizofuatana kwa miaka mingi.

Mpango huu mpya wa uokoaji ni wa muda usiozidi miaka mitatu na baada ya hapo, wengi wanauliza ikiwa mambo yatakuwa mabaya tena.

Ingawa baadhi ya Waghana wanaamini kuwa mkopo huo utashughulikia changamoto za sasa, hautachangia kupunguza umaskini, kubuni nafasi za kazi au nyongeza ya mishahara, anasema mwanauchumi Profesa Godfred Bokpin wa Chuo Kikuu cha Ghana.

Anaongeza kuwa changamoto kubwa ya kutekeleza mpango wa IMF itakuwa mwaka ujao wakati Ghana itapiga kura.

Serikali nchini Ghana zina historia ya kuongeza matumizi makubwa kabla ya uchaguzi - ili kuwaonyesha wapiga kura ni kazi gani nzuri wanayofanya, hata kama hawana pesa kila wakati.

"Serikali itataka kutumia na mpango hautawaruhusu, kwa hivyo itabidi waachane na mpango huo au wabadilishe tarehe ya uchaguzi," anasema Prof Bokpin.

"Natazamia kuona jinsi mpango wa IMF utaweza kuwazuia wanasiasa kutumia pesa kupita kiasi wakati wa uchaguzi."