Nasa imethibitisha sampuli za mwamba wa Bennu zimefika duniani

Chanzo cha picha, NASA
Sampuli za vumbi kutoka katika mwamba hatari zaidi katika mfumo wa jua zimeletwa duniani. Shirika la anga za juu la Marekani Nasa lilipokea sampuli hiyo ikiwa katika chombo kidogo cha angani kilichoshuka katika Jangwa la Magharibi la jimbo la Utah.
Sampuli hizo zilichukuliwa kutoka sehemu ya juu ya mwamba uitwao Bennu mwaka 2020 kwa kutumia chombo cha anga cha Osiris-Rex.
Nasa inataka kuchunguza zaidi kuhusu mwamba huo, ambao unaweza kuigonga sayari yetu katika miaka 300 ijayo.
Sampuli hizo zinaweza kutoa taarifa mapya kuhusu muundo wa jua na sayari zake - na pengine hata jinsi maisha yalivyoanza kwenye ulimwengu wetu.
Kulikuwa na shangwe wakati chombo cha Osiris-Rex kilipoonekana katika kamera kikikaribia dunia. Hatimaye kiligusa ardhi ya jangwa linalomilikiwa na Idara ya Ulinzi saa 10:52 za Marekani (14:52 GMT).

Chanzo cha picha, NASA
Wanasayansi wana hamu ya kuichambua sampuli hiyo ambayo makadirio ya kabla ya kutua inafikia gramu 250 (9oz).
Inaweza kuonekana ni kama kiwango kidogo lakini Eileen Stansbery, mwanasayansi katika Kituo cha Nasa cha Johnson huko Texas, ameeleza, "kwa aina ya majaribio ambayo timu za NASA wanataka kufanya, ni kiwango cha kutosha sana."
Ikiwa, kama watafiti wanavyofikiria, sampuli hiyo ina kemikali za kaboni ambayo inaweza kuwa imehusika katika uumbaji wa maisha basi kuchanganya sampuli hiyo na kemia ya kisasa ya dunia kunapaswa kuepukwa.
"Usafi na kuzuia uchafu kuingia katika chombo, ndilo jambo muhimu sana katika misheni hii," anasema Mike Morrow, naibu meneja wa mradi wa Osiris-Rex.

Chanzo cha picha, NASA/KEEGAN BARBER
"Njia bora ambayo tunaweza kulinda sampuli hii ni kuipeleka katika maabara safi haraka iwezekanavyo. Na hilo limefanikiwa saa nne tu baada ya kutua duniani."
Timu ya maabara ilitenganisha chombo cha angaza za juu, na kuondoa ngao yake ya joto na kifuniko cha nyuma lakini ikaicha sampuli salama ndani ya mkebe wa ndani.
Itasafirishwa siku ya Jumatatu hadi kituo maalumu cha Johnson ambapo uchambuzi wa sampuli utaanza. Mwanasayansi wa Uingereza Ashley King atakuwa sehemu ya timu ya watu sita ambayo itafanya uchambuzi wa awali.
"Ninatarajia kuona aina ya vumbi la mwamba ambalo ni laini sana," mtaalamu huyo anasema.

Chanzo cha picha, NASA
Nasa inapanga mkutano na wanahabari tarehe 11 Oktoba kutoa tathmini ya kwanza kuhusu kile ambacho watakigundua. Sampuli ndogo ndogo zitasambazwa kwa timu za watafiti kote ulimwenguni. Nasa inatumai kupokea mrejesho ndani ya miaka miwili.
"Moja ya sehemu muhimu ya sampuli hii ni kuchukua 75% ya sampuli hiyo na kuifungia kwa ajili ya vizazi vijavyo, kwa watu ambao hata hawajazaliwa na bado hawajafanya kazi katika maabara ambazo leo hazipo kwa kutumia vifaa ambavyo hata hatujavifikiria," mkurugenzi wa Nasa wa sayansi ya sayari, Lori Glaze, aliambia BBC.












