Ugunduzi wa zana za jiwe unaonyesha binadamu wa kwanza walikuwa wabunifu

Chanzo cha picha, David Braun
- Author, Pallab Ghosh
- Nafasi, Mwandishi wa Masuala ya Sayansi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Utafiti mpya uliofanywa kaskazini-magharibi mwa Kenya unaonyesha kuwa binadamu wa kwanza, takriban miaka 2.75 milioni iliyopita, walikuwa wabunifu.
Wanasayansi wamegundua kuwa walitumia zana za jiwe kwa mfululizo kwa kipindi cha miaka 300,000.
Hii inapingana na dhana ya awali kwamba binadamu wa kale walitumia zana kwa bahati nasibu tu.
Ugunduzi wa Namorotukunan ni wa kwanza kuonyesha kwamba ujuzi huu wa kutengeneza zana uliweza kuenezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kwa mujibu, Profesa David Braun wa Chuo Kikuu cha George Washington ugunduzi huu unaonyesha kuwa matumizi ya zana yalikuwa ya muda mrefu na thabiti, si jambo la muda mfupi kama tulivyodhani awali.
"Tulidhani kwamba utumiaji wa zana ungeweza kuwa ni bahati nasibu na kisha kutoweka. Tunapoona miaka 300,000 ya kitu kimoja, hiyo haiwezekani," alisema.
"Huu ni mwendelezo mrefu wa tabia. Utumiaji wa zana hiyo katika (binadamu na mababu za kibinadamu) pengine ni wa mapema zaidi na unaendelea kuliko tulivyofikiria."

Chanzo cha picha, David Braun
Wanaekolojia walitumia miaka kumi kugundua vipande 1,300 vya zana za jiwe, ikiwa ni pamoja na mawe ya kuchonga na misingi ya jiwe, yote yaliyochongwa kwa uangalifu kwa kutumia teknolojia ya Oldowan.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Zana hizi zilitumika kwa mfululizo, zikiwa zimegawanyika katika tabaka tatu za ardhi, zikionyesha maendeleo ya muda mrefu na ujuzi wa hali ya juu wa kutambua mawe bora. Haya ni kulingana na mwanajiosayansi mkuu katika timu ya utafiti, Dk Dan Palcu Rolier wa Chuo Kikuu cha São Paulo nchini Brazili.
"Tunachokiona hapa kwenye eneo ni kiwango cha ajabu cha hali ya juu," aliiambia BBC News.
"Watu hawa walikuwa wanajiolojia wajanja sana. Walijua jinsi ya kupata malighafi bora na zana hizi za mawe ni za kipekee. Kimsingi, tunaweza kukata vidole vyetu na baadhi yao."
Uchunguzi wa kijiolojia unaonyesha kuwa zana hizi ziliwasaidia binadamu hao kuishi wakati wa mabadiliko makali ya tabianchi, ''kutoka maeneo yenye mito na mwani mwingi hadi nyasi kavu na nusu jangwani'', alisema Rahab N. Kinyanjui, mwanasayansi mkuu katika Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.
Badala ya kubadilika kibiolojia, binadamu hawa walitumia zana kudhibiti mazingira yao na kupata chakula.

Mabadiliko haya makali ya mazingira kwa kawaida yanaweza kulazimisha idadi ya wanyama kubadilika kupitia mageuzi au kuondoka.
Lakini watengenezaji zana katika eneo hilo walifanikiwa kustawi kwa kutumia teknolojia badala ya kukabiliana na kibaolojia, kulingana na Dk Palcu Rolier.
"Teknolojia iliwawezesha wenyeji hawa wa mapema wa Turkana Mashariki kuishi katika mazingira yanayobadilika haraka - sio kwa kujirekebisha, lakini kurekebisha njia zao za kutafuta chakula."
Ushahidi wa zana za mawe kwenye tabaka tofauti unaonyesha kuwa kwa muda mrefu na endelevu, watu hawa wa zamani walivuka mbele ya mageuzi ya kibaolojia, wakitafuta njia ya kudhibiti ulimwengu unaowazunguka, badala ya kuruhusu ulimwengu kuwadhibiti.
Na hii ilitokea mwanzoni mwa kuibuka kwa ubinadamu, kulingana na Dk Palcu Rolier.
"Matumizi ya zana yalimaanisha kwamba hawakulazimika kubadilika kwa kurekebisha miili yao ili kuendana na mabadiliko haya. Badala yake, walitengeneza teknolojia waliyohitaji kupata chakula: zana za kurarua mizoga ya wanyama na kuchimba mimea."

Chanzo cha picha, David Braun
Kwa kutumia zana hizi, walichonga mifupa ya wanyama na kuchimba mimea, jambo lililowawezesha kupata chakula kwa muda mrefu na kubaki hai. Hii pia inaonyesha kuwa teknolojia ilikuwa faida kubwa kwa binadamu wa awali, ikiwasaidia kuishi kwenye mazingira yanayobadilika haraka.
"Teknolojia hiyo inawapa wakaaji hawa wa mapema faida, anasema Dk Palcu Rolier.
"Wana uwezo wa kupata aina tofauti za vyakula kadiri mazingira yanavyobadilika, chanzo chao cha kujikimu kinabadilika, lakini kwa sababu wana teknolojia hii, wanaweza kupita changamoto hizi na kupata chakula kipya."

Chanzo cha picha, David Braun
Takriban miaka 2.75 milioni iliyopita, eneo hilo lilikuwa na baadhi ya binadamu wa kwanza, ambao walikuwa na ubongo mdogo.
Binadamu hawa wa kale wanaaminika kuwa waliishi pamoja na mababu zao wa kiasili: kundi la binadamu wa awali linaloitwa australopithecines, waliokuwa na meno makubwa na mchanganyiko wa sifa za sokwe na binadamu.
Watumiaji wa zana katika Namorotukunan huenda walikuwa mmoja wa makundi haya au pengine wote wawili.
Ugunduzi huu unapingana na dhana iliyokuwa ikishikiliwa na wanasayansi wengi wa mageuzi ya binadamu kwamba matumizi endelevu ya zana yaliibuka baadaye, kati ya miaka 2.4 na 2.2 milioni iliyopita, wakati binadamu walikuwa na ubongo mkubwa zaidi, kulingana na Profesa Braun.
"Hoja ni kwamba tunayoona ni ongezeko kubwa la ukubwa wa ubongo. Mara nyingi imedhaniwa kuwa matumizi ya zana yaliruhusu binadamu kula chakula cha kutosha kwa ubongo huu mkubwa.
"Lakini kile tunachoona Namorotukunan ni kwamba zana hizi za awali zilitumika kabla ya ongezeko hilo la ukubwa wa ubongo."
"Huenda tumepunguza sana umuhimu wa binadamu hawa wa awali na mababu zao. Tunaweza kufuatilia mizizi ya uwezo wetu wa kuendana na mabadiliko kwa kutumia teknolojia mapema zaidi ya tulivyodhani, takriban miaka 2.75 milioni iliyopita, na huenda hata kabla yake."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












