Yanga: Jinsi mafanikio katika klabu ya Tanzania yalivyoibua msisimko wa kitaifa

Mashabiki wa Yanga

Chanzo cha picha, young Africans

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania

Timu ya Young Africans Sports Club almaarufu Yanga, imeshika nafasi ya pili katika Kombe la Shirikisho la Afrika (CAFCC), linaloratibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kufuatia kushindwa katika fainali ya mkondo wa pili nchini Algeria.

Yanga iliambulia medali za fedha siku ya Jumamosi Juni 3, 2023 baada ya kuifunga klabu ya USM Alger, 1-0.

Ushindi ambao haukuisaidia timu hiyo kubeba kombe kwani iliruhusu magoli mengi nyumbani katika fainali ya mkondo wa kwanza.

Katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ya Kariakoo ilifungwa 2-1 mbele ya maelfu ya mashabiki wake Mei 28, 2023. Ilitinga fainali baada ya kuitoa timu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, kwa mabao 4-1 katika michezo miwili.

Mamia ya mashabiki wa Yanga walifika katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere usiku wa jana kwa ajili ya kuipokea timu hiyo. Huku mashabiki wa timu nyingine watu wa mirengo mbalimbali ya kisiasa wakimimina pongeza.

Wanasiasa wanena

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema Freeman Mbowe amewapongeza wachezaji wa timu ya Yanga kwa kupambana bila kuchoka dhidi ya mabingwa USM Alger kupitia ukurasa wake wa Twitter.

“Mimi ni muumini wa kutokukata tamaa, ni muumini mzuri pia wa kupambania ninachokiamini kwa gharama yoyote. Na ndicho Yanga mlichokionesha jana. Asanteni kwa hili, pongezi za dhati kwa kuweka alama kwenye mashindano ya kimataifa ya CAFCC, sina shaka wakati ujao tutalibeba kabisa.”

Shabiki wa Simba Sports Club na Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Mei 18, 2028 alitoa pongezi kwa Yanga kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, baada ya timu hiyo kutinga fainali.

“Ninawapongeza sana klabu ya Yanga kwa mafanikio makubwa. Tunawaombea mafanikio zaidi kwani mafanikio ya Yanga ni mafanikio ya Tanzania.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameipongeza timu ya Yanga kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika michuano hiyo. Sanjari na kuwaalika Ikulu siku ya leo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo na mchezo wa mpira kwa ujumla.

“Historia mliyoandika katika safari yenu ya michuano hii mikubwa. Ni ya heshima kwa taifa letu, nawatakia heri katika mipango yenu ya siku zijazo,” aliandika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter.

Ni kawaida kwa mchezo wa soka nchini Tanzania kuwaleta pamoja wanasiasa, hasa timu zinapofika hatua kubwa katika mashindano na kuibeba bendera ya nchi. Timu ya Simba na Yanga zenye mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania, zina kusanya watu kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa.

Rais Samia na Soka

Rais Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Ikulu Mawasiliano

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha mafanikio katika mchezo wa soka ndani na kimataifa, zimeonekana wazi katika mashindano yote mawili; Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nilianza kwa kutoa Shilingi milioni tano kila goli, kwa timu ya Simba na Yanga, kwenye michuano hii, laki pia nikatoa shilingi milioni 10 kila goli moja ambapo bahati mbaya Simba wao wameisha njiani na kuwaacha wenzao Yanga.”

Alisema hayo wakati akizungumza katika tukio la uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya televisheni ardhini (DTT) ya kampuni ya Azam, Mei 18, siku moja tu baada ya Yanga kutinga fainali.

Itakumbukwa kwamba timu ya Simba SC ilitolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mikwaju ya penalti 4 – 3, baada ya kumaliza dakika 90 droo ya bao 1-1 katika mechi mbili za robo fainali dhidi ya timu ya Waydad ya nchini Morocco.

Uamuzi wa rais Samia kutoka mamilioni ya pesa umechangia pakubwa kuzipatia motisha timu hizo sambamba na kutangaza soka la Tanzania kimataifa. Ambapo kwa mara ya kwanza Yanga ikafuzu hatua ya fainali katika kombe la shirikisho.

Mwezi Agosti 2020, rais mstaafu Jakaya Kikwete alitoa wito kwa timu za Tanzania kufanya uwekezaji mkubwa katika timu za vijana ili kunoa vipaji vyao wenyewe. Kikwete alizungumza hilo katika Siku ya Wananchi katika uwanja wa Mkapa.

Zipo baadhi ya timu tayari zinamiliki timu za vijana, wakiendelea kuwanoa. Mchango wa Rais Samia unaweza kuwa na msaada mkubwa kwa timu ambazo zina vijana wadogo, nao kunufaika na pesa hizo.

Umaarufu wa mpira ulimwenguni

Mchezo wa mpira unabakiwa kuwa namba moja miongoni mwa michezo yenye mashabiki wengi duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali. Ukikadiriwa kuwa wa mashabiki takribani bilioni 4.

Mpira ni kama dini ya ulimwengu, kila uendapo kuna maelfu ya mashabiki wakifuatilia timu zao za ndani na zile timu za kimataifa. Mchezo wa mpira una nguvu ya kusimamisha shughuli katiika majiji na watu wakaelekea uwanjani au wakaingia barabarani kusherehekea.

Tangu timu ya kwanza kuundwa 1857, Sheffield F.C huko England. Na kombe la FA kuwa mashindano makongwe zaidi ulimwenguni ambayo bado yanafanyika hadi sasa, kutoka 1871. England na Scotland kuwa timu za taifa za kwanza kucheza Novemba 1872. Na Kombe Dunia kuchezwa Uruguay 1930. Mchezo wa soka umeendelea kukua.

Maelfu ya ligi huchezwa takribani kila nchi, na ligi na mashindano ya kimataifa hukutanisha timu na wachezaji wa mataifa mbali mbali. Mpira una ushabiki mkubwa, ushindani na biashara ya pesa nyingi.