Kombe la Dunia 2022: "Mashabiki wa kukodi" wanavyosherehesha kuelekea kuanza kwa michuano

"Shangwe za Kombe la Dunia tayari zinapitia mitaa ya Doha!" Hivi ndivyo Kamati kuu inayoratibu michuano Qatar, wiki moja kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, lililopangwa kufanyika Novemba 20.

Kulikuwa na batucada, bendera, wigi, kofia na kelele nyingi kutoka kwa mashabiki wanaounga mkono Ujerumani, Argentina, Brazil, Uhispania, Ufaransa, Uingereza, Mexico au Ureno. Lakini baadhi ya mashabiki kutoka nchi hizo walianza kutilia shaka ukweli wa "watani" wao huko Qatar.

Kupitia mitandao ya kijamii, walibaini kuwepo sehemu kubwa ya mashabiki wanaodaiwa kuwa na sifa zinazofanana sana na za wenyeji wa Mashariki ya Kati.

"Watu hawa, wanatoka sehemu gani ya Uhispania?" aliuliza mtumiaji wa Twitter, akionesha gwaride la Wahispania wakipuliza tarumbeta na kupiga ngoma.

Walipokuwa wakiandamana kwenye barabara ya Corniche, mojawapo ya barabara kuu za Doha, mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Argentina walivaa vinyago vya baadhi ya timu za taifa za Argentina.

Wachache waliimba kwa Kihispania wimbo wa kuhamasisha "twende, twende, Argentina...!" . Hatahivyo, wengine walionekana kujaribu tu kuendana na mazingira yake. "Je, wanalipwa kuwa mashabiki wa nchi nyingine au kuna nini?" Aliuliza mtu mmoja kwenye ukurasa wa Twitter.

Katika gwaride hilo pia kulikuwa na mashabiki kutoka Ufaransa au Uingereza ambao pia walivutia.

Kwa upande wa Wamexico, sherehe za Kombe la Dunia ilikuwa tofauti. Ubalozi wa Mexico nchini Qatar uliripoti kuwa jumuiya ya wazalendo nchini humo walikutana katika eneo tofauti ili kuhimiza ujio ujao wa Timu ya Taifa ya Mexico.

Kelele za "Mexico, Mexico!" Ziliimbwa na watu kadhaa waliohudhuria wakiwa na kofia za kawaida za Mexico na bendera yenye rangi tatu.

Kusafiri kwa ajili ya Kombe la Dunia mwaka huu kunaweza kuwa tatizo kwa mashabiki kutokana na gharama kubwa, anasema Dan Roan, mhariri wa michezo wa BBC. "Kuna kutokuwa na uhakika kuhusu uzoefu wa mashabiki nchini Qatar.

Ghorofa, vyumba vya hoteli, kambi za jangwani, majengo ya kifahari na hata vyumba kwenye meli za kitalii vimepatikana. Lakini baadhi ya mashabiki wamelalamika kuhusu chaguzi chache na za gharama kubwa za malazi." Roan anafafanua. Hili linaweza kuwa sababu inayozuia uwepo wa mashabiki kutoka nchi 32 zinazoshiriki Kombe la Dunia.