Je, mgogoro wa Sudan unaathiri vipi nchi za Afrika Mashariki?
Na Rashid Abdallah

Chanzo cha picha, Getty Images
Sudan; taifa la Kaskazini-mashariki mwa bara la Afrika, lenye wakaazi takribani milioni 45.66 kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2021. Kwa miongo mitatu na nusu liliongozwa na rais Omar Hassan Ahmad al-Bashir kutoka Oktoba 1993 hadi Aprili 2019.
Al-Bashir ambaye anakabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), aliondolewa madarakani kwa nguvu na jeshi la nchi hiyo, baada ya msururu wa maandamano ya kiraia dhidi ya utawala wake. Kuondolewa kwake kulitoa matumaini kwa wengi kwamba utakuwa mwanzo wa kuzaliwa Sudan mpya.
Mchakato wa kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia ulikumbwa na mkwamo. Kwa takribani miaka minne Sudan ilikuwa katika danadana za kisiasa kati ya upande wa Jeshi na wale waliotaka kusimikwa haraka serikali ya kiraia.
Serikali haikuundwa na ilipofika Jumamosi ya Aprili 15, 2023, mapigano ya kuwania madaraka yalizuka kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF), wakiongozwa na mkuu wa majeshi Abdel Fattah Al Burhan, na kikosi cha Msaada wa Dharura (RSF), kikiongozwa na naibu wake, Mohammed Hamdan Dagalo.
Milio ya risasi, mirindimo ya makombora na ndege za kivita ndizo sauti zinazosikika usiku na mchana katika mji mkuu wa taifa hilo – Khartoum. Mapigano yanazidi kuenea. Watu zaidi ya mia mbili wamesha uawa na zaidi ya elfu wamesha jeruhiwa. Je, mgogoro huu uta-ziathiri vipi nchi za Afrika Mashariki?
Mgogoro mpya na athari zake kwa Afrika Mashariki
Takribani Wakenya 3,000 wamekwama nchini Sudan, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nje wa taifa hilo, Dkt. Alfred Mutua. Serikali ya Kenya imedhamiria kuwaondoa raia wake ikiwa mapigano yatazidi kushika kasi.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda mwenye dhamana ya ushirikiano wa kikanda, John Mulimba, ameeleza kupitia ukumbi wa Bunge la nchi hiyo, juu ya uwepo wa Waganda takribani 300 ambao wamekwama Sudan.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakiwemo mahujaji waliokuwa wakielekea Saudi Arabia kwa ajili ya ibada. Wengine ni wafanya kazi na wanafunzi, wagonjwa waliokwenda kwa matibabu na watembezi. Serikali ya Uganda imeeleza kuwa inashirikiana na Umoja wa Mataifa kutafuta uwezekano wa kuwaondoa raia wake.
Mwanafunzi raia wa Burundi akizungumza na BBC Swahili, siku ya Jumanne, alieleza, “siku mapigano yanaanza nilikuwa naenda kufanya mtihani lakini haikuwezekana na mtihani ulisitishwa, na vipindi vyote vya masomo vimesitishwa, tunasubiri kama patapatikana usalama. Ila hatujui ni muda gani.”
Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Stergomena Tax amesema nchi hiyo inaendelea kuufuatilia kwa ukaribu mzozo huo. Alisema watanzania 210 wanaoishi nchini humo ambao kati yao 171 ni wanafunzi na wengine ni maofisa wa ubalozi na raia wengine wako salama.Pia, amewataka raia wa nchi hiyo walioko Sudan kuchukua tahadhari wakati serikali ikitafakari juu ya mustakbali wao.
Juhudi za Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Mgogoro wa Sudan umekuja wakati ambao nchi za Afrika Mashariki kama zilivyo nchi nyingine duniani, zinapitia hali mbaya ya mdororo wa kiuchumi utokanao na msururu wa mambo; ikiwemo janga la Uviko 19, mabadiliko ya tabia nchi yaliyochangia ukame na kubwa zaidi ni vita nchini Ukraine.
Mbali na hilo, Jumuiya ya Afrika Mashariki iko katika mchakato wa kumaliza migogoro ambayo wanachama wake wanakabiliana nayo. Moja wapo, ni ule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao unaathiri nchi wanachama Rwanda, Burundi, Uganda na Congo yenyewe.
Vilevile, nchi za Afrika Mashariki zimepakana na nchi kadhaa zenye migogoro. Kenya imepakana na Somalia yenye vita vya muda mrefu. Kenya na Sudan Kusini zimepakana na Ethiopia ambayo mgogoro wake katika jimbo la Tigray ndio kwanza unaonekana kutulia.
Wakati Sudan Kusini ikiwa ndio mwanachama pekee wa Jumuiya kupakana na Sudan katika mpaka wake wa kaskazini - kuendelea kwa mgogoro huo kutaathiri shughuli za watu Afrika Mashariki hasa wale walio katika taifa hilo. Pia, kuathiri shughuli za kibiashara hasa ile ya usafiri.
Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao makuu yake Arusha, Tanzania, siku ya Jumanne ilieleza umuhimu wa kufanyika mazungumzo ili kumaliza mkwamo unaendelea Sudan na kuzitaka pande zinazokwaruzana kutumia jumuiya ya kikanda kama njia ya muafaka ili kutuliza hali ya mambo.
Fauka ya hayo, Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika (IGAD), limetua viongozi watatu watakao elekea Sudan kwa ajili ya kwenda kutafuta suluhu. Rais wa Kenya, William Ruto, rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, na rais wa Djibout Ismail Omar Guelleh.
Historia ya migogoro Sudan

Chanzo cha picha, Getty Images
Migogoro inayohusisha uasi na mapambano ya mtutu wa bunduki siyo kitu kipya kwa taifa la Sudan. Yalishamiri wakati Sudan ya sasa na ile ya Kusini zikiwa ni nchi moja. Tudurusi walau kwa uchache, migogoro ya wenyewe kwa wenyewe wakati nchi hiyo ikijumuisha na Sudan Kusini.
Vita vya kwanza vya yenyewe kwa wenyewe, vilivyodumu kwa miaka 17, vilitokea kati ya 1955 na 1972. Vilivyohusisha majimbo ya upande wa Kusini na yale ya upande wa Kaskazini. Makubaliano ya Addis Ababa ya 1972 ndiyo yaliyomaliza vita hivyo vinavyokadiriwa kuua watu laki tano.
Vita vya pili vya wenyewe ni vililipuka tena kati ya 1983 hadi 2005, baada ya makubaliano ya Addis Ababa kuvunjwa na Rais wa wakati huo Jaafar Mohammed an-Nimeiry. Inakadiriwa watu milioni mbili waliuawa.
Msururu wa vikao vilivyokuwa vikifanyika Kenya vya kutafuta muafaka. Vilifikia tamati Januari 2005 baada ya makubaliano ya mwisho kusainiwa Naivasha kati ya serikali ya Khartoum na Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLM).
Wakati wa vita, ukame na maradhi vilichangia pia idadi ya vifo kuwa kubwa. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilipokewa maelfu ya wakimbizi wakati wa vita vyote viwili. Hadi sasa nchi hizo bado zinahifadhi wakimbizi kutoka Sudan, ambao kwa sasa ni wa Sudan Kusini.
Baada ya kura ya maoni ya Julai 2011 iliyopelekea kuzaliwa Sudan ya Kusini, mji mkuu wake Juba. Mambo katika taifa hilo changa bado hayajatengemaa, kuna mivutano ya kisiasa na wakati mwingine mapigano ya wenyewe kwa wenyewe huzuka.
Lakini vurugu za sasa za Sudan ya Khartoum hazihusishi tena Wasudan Kusini. Makundi yote mawili yanayopigana yanatoka Sudan ya Kaskazini. Ni kati ya Jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha Msaada wa Dharura ambacho ni mabaki ya wana mgambo wa Janjaweed waliohusika katika vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe.












