Ziara ya Putin nchini Ukraine ilikuwaje?

Akiwa anaendesha gari katika jiji hilo lililoshambuliwa sana usiku, Rais wa Urusi Vladimir Putin alifanya ziara yake ya kwanza huko Mariupol - ulioharibiwa wakati vikosi vya Urusi viliuzunguka mji huo mwanzoni mwa vita.
BBC ilifuatilia sehemu ya njia aliyopitia, ambayo ilipita karibu na maeneo kadhaa ambapo mashambulizi ya jeshi lake yalifanyika kwa miezi kadhaa. Urusi iliteka jiji hilo Mei mwaka jana.
Video zilizotolewa na vyombo vya habari vya Urusi zinaonyesha Putin akizungumza na mwenzi wake alipokuwa akielekea kwenye ukumbi wa jiji hilo. Ikulu ya Kremlin ilisema kuwa ziara hiyo ilifanyika siku ya Jumamosi na kwamba rais wa Urusi "aliamua kwa hiari" kuuzuru mji huo.
Meya wa Mariupol, Vadym Boychenko, ambaye yuko uhamishoni, aliambia BBC kwamba jiji hilo lilikuwa "moyoni " mwa Putin kwa sababu ya kile kilichotokea huko.
"Tunapaswa kuelewa kwamba Mariupol ni mahali pa mfano kwa Putin, kwa sababu ya hasira yake juu ya jiji la Mariupol. Hakuna mji mwingine ulioharibiwa kama huu. Hakuna mji mwingine ambao umezingirwa kwa muda mrefu. Hakuna mji mwingine wowote umekabiliwa na mashambulizi mengi ya mabomu.", alisema.
Kuendesha gari kupitia eneo la shambulio la Urusi.

Chanzo cha picha, Reuters
BBC imetambua baadhi ya alama kwenye njia ya kiongozi huyo wa Urusi. Putin anaonekana akiendesha gari kwenye Mtaa wa Kuprina, akigeukia Mir Prospekt Avenue na kisha Metalurhiv Avenue, ambapo Ukumbi wa Philharmonic upo, ambao picha zinaonyesha alitembelea baadaye.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ameketi karibu na mtu aliyevalia kofia nyeusi, ambaye vyombo vya habari vya Urusi vinamtambulisha kama Naibu Waziri Mkuu wa Urusi Marat Khusnullin.
Upande wao wa kushoto, wanapoendesha gari kando ya Mir Prospekt, kuna sanamu za ndege katika Uwanja wa Freedom Square Mariupol.
Zaidi upande wa kulia eneo lisiloonekana kwenye picha ni Hospitali ya Nambari Tatu ya kina mama ya Mariupol, ambayo ilishambuliwa kwa bomu katika shambulio kubwa Machi mwaka jana.
Picha za Mariana Vishegirskaya, mwenye ujauzito wa miezi tisa, uso wake ukiwa na damu, akishuka ngazi zilizojaa vifusi zilisambazwa sana huku kukiwa na hasira juu ya shambulio hilo. Alinusurika na akajifungua siku iliyofuata. Miongoni mwa wahasiriwa wa shambulio hilo pia alikuwa mwanamke mwingine mjamzito.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelitaja shambulio hilo kuwa uhalifu wa kivita, lakini ubalozi wa Urusi mjini London ulisema hospitali hiyo haitumiki tena na inatumiwa na wanachama wa Kikosi cha Azov - kundi la wanamgambo wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ukraine lililoundwa mwaka 2014 na ambao walijumuishwa katika Walinzi wa Kitaifa wa Ukraine.
Katika ziara yake huko Mariupol, Putin aligeukia Mir Prospekt kabla tu ya barabara hiyo kufika Theatre Square - eneo la mlipuko mbaya ambao unakadiriwa kuua angalau 300 na labda raia 600.
Raia walitumia jengo hilo kama kimbilio la kuzingirwa na ishara kubwa yenye neno "watoto" ilikuwa imechorwa kwa Kirusi mbele ya ukumbi wa michezo. Jengo hilo liliporomoka wakati lilipogongwa. Uchunguzi wa baadaye wa shirika la habari la Associated Press ulidai kuwa hadi watu 600 walikufa. Urusi ilikanusha kulipua ukumbi wa michezo na kulaumu Kikosi cha Azov.

Chanzo cha picha, Reuters
Jengo la Urusi huko Mariupol
Picha kutoka kwa ziara ya Putin zinaonyesha rais huyo wa Urusi akitembelea nyumba mpya ya makazi, inayosemekana kuwa katika wilaya ya Nevsky ya Mariupol.
Anaongozwa na Khusnulli, ambaye anamwonyesha baadhi ya mipango ya ujenzi mpya. Anaonekana pia akizungumza na watu ambao vyombo vya habari vya Urusi vinasema ni wenyeji, na anatembelea nyumba ambayo anaambiwa ina vyumba vitatu.
Nevsky ni wilaya mpya inayoundwa na vyumba kadhaa vya ghorofa magharibi mwa jiji. Umepewa jina la Mto Neva, ambapo St. Petersburg, mji alikozaliwa Rais Putin, uko.
Meya Boychenko alisema kuwa majengo mengi yaliyojengwa na Warusi yako nje kidogo ya jiji.
"Walijenga hili ili tu kuthibitisha kwamba haya yanayotokea huko ni ya kweli. Lakini wanadanganya! Wanadanganya kwamba walikuja kuukomboa mji, waliuharibu, mji huu haupo tena, na itachukua miaka 20. Kuujenga upya!", alisema.
Wakazi wa Mariupol waliambia BBC kuwa majengo mapya yanajengwa na baadhi ya yale yaliyoharibiwa na jeshi la Urusi yanaondolewa. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa asilimia 90 ya majengo ya makazi yaliharibiwa katika shambulio la Urusi.
Mwandishi wa habari wa Norway Morten Risberg, ambaye alitembelea Mariupol mwezi Disemba, alisema ameona "ujenzi na ukarabati mkubwa" huku kukiwa na "uharibifu kila mahali ulipotazama".
"Wanabadilisha majina ya barabarani, wanapaka rangi za Urusi juu ya rangi za Ukraine na kuweka bendera za Urusi kila mahali," aliambia BBC. Wengi wa raia waliosalia katika jiji hilo "walilenga tu kunusurika", alisema.
Kutembea kupitia ukumbi wa tamasha

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwingineko katika picha hizo, Rais Putin anaonekana akipita ndani ya ukumbi wa tamasha huko Mariupol. Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilisema ni Ukumbi wa Tamasha wa Philharmonic - na BBC imethibitisha kuwa picha hizo zinalingana na muonekano wa ndani ya ukumbi huo.
Hili ni jengo Umoja wa Mataifa ulioonya kuwa litatumika kuwahukumu askari wa Ukraine ambao walipinga vikosi vya Kirusi kwa miezi katika kiwanda kikubwa cha chuma cha Azovstal huko Mariupol. Urusi hatimaye ilipata udhibiti kamili wa Mariupol mwezi Mei baada ya walinzi wake kujisalimisha.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Agosti mwaka jana - ikiwa ni pamoja na maafisa wa Ukraine - zilionekana kuonyesha vizimba vya chuma vikijengwa jukwaani. Kulingana na Umoja wa Mataifa, kuwashtaki wafungwa wa vita (POWs) kwa kushiriki katika uhasama ni uhalifu wa kivita.
Lakini kesi hizo hazikufanyika, kwani POWs baadaye walikuwa sehemu ya kubadilishana wafungwa kwa wafungwa 55 kutoka Ukraine, akiwemo naibu wa zamani Viktor Medvedchuk.
Picha za hivi karibuni za mambo ya ndani ya ukumbi wa tamasha zinaonyesha kuwa vizimba vimeondolewa na ndani ya jengo imepambwa kwa mapambo mapya.
Wakati wa kuzingirwa, jumba la tamasha, pamoja na jumba la maigizo, lilitumiwa na raia kama kimbilio. Taasisi za kitamaduni zilikuwa "ambapo watu wangejificha kwenye vyumba vya chini na kungoja mashambulizi ya Urusi yamalizike," Boychenko alisema.
Kabla ya uvamizi huo, palikuwa mahali pa tamasha la Mariupol Classic la muziki wa zamani. Kulingana na Boychenko, tamasha hilo lilikuwa "sherehe kubwa ya muziki wa kitamaduni kwa watu wa Mariupol" ambayo ilivutia wasanii kutoka ng'ambo na kutoka sehemu zingine za Ukraine.
"Watu wengi walikusanyika kila wakati kwenye tamasha hili ili kuhisi hali ambayo ilikuwa ikitawala huko Mariupol," alisema.
Katika picha ya baadaye, Rais Putin anaonekana akitembelea kumbukumbu ya Vita vya Pili vya Dunia iitwayo Ukumbusho wa Ukombozi.










