Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania katikati ya matumaini na mashaka, ikisubiri ripoti ya Oktoba 29
Tanzania kwa sasa iko katika wakati wa kipekee na wenye uzito mkubwa wa kihistoria. Ni kipindi cha kusubiri, kutafakari na kujiuliza maswali magumu kuhusu mustakabali wa taifa, wakati macho yote yakiwa yameelekezwa kwenye ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mohamed Chande, ripoti hii itakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye aliyeiunda tume hiyo, Novemba 18, 2025. Itakabidhiwa Aprili 23, 2026.
Na kabla ya ripoti kukabidhiwa Rais aligusia machache yanayohusiana na matukio ya oktoba 29; " tunaambiwa kwamba vijana walioingia barabarani walilipwa fedha kwanza ndiyo wakaingia barabarani".
Alisema pia vijana walifuata mkumbwa, hakakujua wanachokifanya. Mamia ya vijana walikamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa uhaini, kabla kusamehewa na Rais.
Sasa ripoti hii si hati ya kawaida ya kiutawala. Ni matokeo ya safari ndefu ya uchunguzi iliyogusa hisia za wananchi, taasisi za dola na wadau wa ndani na nje ya nchi. Kwa baadhi, ni nafasi ya kupata majibu yaliyosubiriwa kwa muda mrefu. Kwa wengine, ni mtihani wa ukweli, uwazi na uimara wa taasisi za taifa.
Katika hali hiyo, Tanzania imejikuta katikati ya hisia mbili kubwa: matumaini ya kupata majibu na pia mashaka kuhusu mwelekeo wa matokeo yake. Na ndio maana mjadala kuhusu ripoti hiyo umevuka mipaka ya siasa na kuwa mjadala wa kitaifa unaogusa mustakabali wa umoja wa nchi.
Oktoba 29, 2025, siku nyingine ya kihistoria Tanzania
Oktoba 29, 2025 ilianza kama siku ya kawaida ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania. Wananchi walijitokeza kupiga kura wakiwa na matarajio ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa amani na utulivu.
Hata hivyo, kadri siku ilivyoendelea, taarifa za sintofahamu zilianza kuibuka katika baadhi ya maeneo. Maandamano, vurugu na taharuki vilianza kuripotiwa, na kugeuza hali ya uchaguzi kuwa ya wasiwasi mkubwa.
Katika muda mfupi uliofuata siku hiyo na siku chache baadaye, taarifa za vifo, majeruhi na uharibifu wa mali zilianza kusambaa. Hali hiyo ilizua hofu na maswali mengi miongoni mwa wananchi kuhusu kilichotokea na chanzo chake halisi.
Kutoka hapo, mjadala wa kitaifa ulibadilika. Haukuwa tena kuhusu matokeo ya uchaguzi pekee, bali kuhusu usalama, haki, na uaminifu wa mfumo wa uchaguzi na taasisi za dola.
Kuanzia wanaharakati wa ndani, vyama vya upinzani, mpaka Jumuia za kimataifa zikaanza kuitazama Tanzania kwa jicho la kipekee.
Safari ya siku 153 za Tume ya Uchunguzi
Kufuatia matukio hayo, serikali ilianzisha Tume ya Uchunguzi yenye wajumbe tisa kuchunguza kilichotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.
Tume hiyo ilianza rasmi kazi yake tarehe 20 Novemba 2025, na Ilipewa siku 90 kuwasilisha majibu ya maswali sita muhimu: Chanzo halisi cha ghasia hizo ni nini?Nani walihusika? na kwa lengo gani?
Maswali mengine ni madhara gani yalitokea?h atua gani zilichukuliwa kukabiliana na hali hiyo? na mapendekezo gani yanapaswa kutolewa?
Katika kipindi cha takribani siku 153, tume ilifanya kazi kitaifa. Ilitembelea mikoa 11 na wilaya 21, ikikusanya ushahidi kutoka kwa wananchi wa kawaida, waathirika, viongozi wa kisiasa na vyombo vya usalama.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, wamepokea ushahidi kutoka kwa watanzania 63,603 kupitia njia mbalimbali.
"Nasubiri kw ahamu kubwa, kilichomo kwenye ripoti, idadi ya waliotoa ushahidi ni kubwa naamini hawataichakachua", anasema Aziz Charles mkazi wa Dar es salaam.
Hili la kuchakua ripoti Tume ililipinga mapema ikisema iko huru na itafanya kazi zake kwa uhuru.
Kila ushuhuda uliobebwa na tume unaongeza uzito wa kazi yake. Badala ya kuwa uchunguzi wa kawaida, unageuka kuwa safari ya kuelewa maumivu, hofu na matarajio ya wananchi, na hapo ndipo matumaini yalipo na mashaka yanapoanzia.
Matumaini na mashaka ya watanzania
Kabla ya matukio ya oktoba 29 na hata baada ya matukio yale, Tanzania hakiua inaonekana kama taifa moja kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mgawanyiko wa wazi kisiasa ulijionyesha. Sasa kadri uchunguzi ulivyoendelea wa Tume, nchi hiyo ilijikuta ikigawanyika pia kimtazamo. Wapo waliouona mchakato huo kama nafasi ya kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za dola na kujenga upya mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wadau wa kisiasa na kijamii waliendelea kueleza mashaka kuhusu uhuru na uhalali wa tume, wakihofia uwezekano wa matokeo yake kuegemea upande fulani. Vyama vya siasa vya upinzani, wanaharakati na baadhi ya Jumuia za kimataifa zimeonyesha wasiwasi wao kuhusu uhuru wa tume, ingawa tume yenyewe imesema iko huru.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia, Dennis Muchunguzi, hivi karibuni, alisisitiza umuhimu wa utulivu wa taifa akisema:
"Si sahihi kuanza kutoa hukumu au kuzusha taarifa zisizo na msingi kuhusu ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio Oktoba 29 wakati bado haijakamilika. Hadi sasa hakuna anayefahamu yaliyomo ndani ya ripoti hiyo, hivyo ni vyema jamii ikasubiri kwa utulivu matokeo rasmi."
Miongoni mwa mitazamo hiyo, mchambuzi wa kimataifa Salim Amin anaeleza kuwa hali ya sasa ndiyo inayoifanya Tanzania kuonekana iko katika "kizingiti cha historia," ambapo taifa bado halijapata simulizi rasmi la tukio hilo kubwa la kitaifa.
'Ripoti ya kusuka ama kuonyoa'
Ripoti ya Tume ya Uchunguzi imekamilika na inakabidhiwa kwa Rais Samia Aprili 23, 2026. Hii ni hatua inayotazamwa kama moja ya matukio muhimu zaidi ya kisiasa nchini Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa upande mmoja, ripoti hiyo inatarajiwa kutoa mwanga kuhusu kilichotokea na kusaidia taifa kuelekea uponyaji, uwajibikaji na kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi zao.
Kwa upande mwingine, kuna hofu kwamba matokeo yake yanaweza kufungua mjadala mpya wa kisiasa, hasa iwapo hitimisho lake halitalingana na matarajio ya makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa.
" Ripoti hii ni ya kusuka ama kunyoa, kujenga ama kubomoa, kwa sababu matarajio ni makubwa sana, nchi ikiwa katika mazingira ya aina hii, ripoti ikikidhi matakwa itajenga upaya taifa, ila ikija na matokeo tofauti, ufa utakuwa mgumu kuzibikana imani itapotea kabisa", anasema Amin
Kwa upande mwingine, kuwekwa ndani kwa Tundu Lisuu, kiongozi wa mkuu wa upinzani na mwenyekiti wa Chadema, anayetuhumiwa kwa kesi ya uhaini, kunajenga maswlai mengine, nchi itatokaje ilipo? ripoti inatarajiwa kutoa muelekeo wa maridhiano, nini mustakabali wa Lissu.
Makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche alisema, Lissu ndiye mwenye fimbo ya maridhianona mazungumzo mengine yoyote yatakayohusu mustakabali wa taifa hilo, lazima awepo nje kushiriki kama mamlaka zitaona umuhimu wa maridhiano ya kweli.
Ndiyo maana Tanzania sasa iko katika hali ya kusubiri kwa makini na kwa tahadhari si kwa sababu ya udadisi pekee wa ripoti, bali kwa sababu ya uzito wa matokeo yanayoweza kuathiri mshikamano wa taifa, athari chanya ama hasi.