Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yasema imekamata meli mbili Hormuz baada ya meli tatu kushambuliwa

Jeshi la Wanamaji la IRGC limeonya kuwa linafuatilia kwa karibu shughuli zinazoendelea katika Mlango wa Bahari wa Hormuz na limeapa kuchukua hatua kali dhidi ya wanaokiuka sheria.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja, nakutakia usiku mwema.

  2. Maafisa 150 wa polisi wa Kenya warejea kutoka Haiti, wakihitimisha misheni ya MSS

    Kikosi cha nne cha maafisa wa polisi wa Kenya waliotumwa Haiti chini ya misheni ya Multinational Security Support (MSS) kimerejea nchini humo, kikihitimisha jukumu la Kenya katika kurejesha utulivu nchini humo wa Karibiani.

    Maafisa hao 150 wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), wakipokelewa na maafisa waandamizi wa usalama, na hivyo kufunga rasmi misheni iliyoanza mwaka 2024 baada ya kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

    Kikosi hicho kinaongozwa na Naibu Inspekta Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Utawala, Gilbert Masengeli, ambaye awali alisafiri kwenda Haiti kwa mazungumzo ya ngazi ya juu na mamlaka za nchi hiyo.

    Kenya ilipeleka takriban maafisa 980 kwa awamu ili kusaidia juhudi za kuleta utulivu, hasa katika mji mkuu, Port-au-Prince, uliokuwa umedhibitiwa na magenge yenye silaha.

    Kurejea huku kunafuatia kurejea kwa vikosi vingine mwezi Desemba 2025 na Machi 2026 baada ya kukamilika kwa jukumu la miezi 18.

    Maafisa wa serikali waliwasifu kwa taaluma, nidhamu na ujasiri wao katika mazingira magumu wakishirikiana na Polisi wa Taifa wa Haiti.

    Wakati huo huo, misheni ya MSS imebadilishwa na kuwa kikosi kipya cha Gang Suppression Force (GSF), mfumo unaoungwa mkono kimataifa ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana Haiti.

    GSF inatarajiwa kuwa na hadi wanachama 5,500, wakiwemo polisi na wanajeshi, watakaofanya kazi kwa karibu na vyombo vya usalama vya Haiti kukabiliana na magenge, kulinda miundombinu muhimu na kusaidia operesheni za kibinadamu.

    Maafisa wa Kenya walichangia pakubwa katika misheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kufungua tena barabara muhimu na kusaidia kuimarisha uwezo wa vyombo vya usalama vya ndani.

    Soma zaidi:

  3. Trump asema mazungumzo na Iran yawezekana kuanza siku chache zijazo

    Donald Trump amesema “inawezekana” duru ya pili ya mazungumzo ya amani na Iran kuanza kufikia Ijumaa, kwa mujibu wa gazeti la New York Post.

    Gazeti hilo limesema maafisa wa Pakistan waliliambia kuwa mazungumzo yanaweza kufanyika ndani ya saa 36 hadi 72 zijazo. Swali hilo lilipowasilishwa kwa Trump, alijibu kupitia ujumbe mfupi akisema: “Inawezekana! Rais DJT.”

    Jana, Trump alitangaza kuongeza muda wa usitishaji mapigano na Iran, uliokuwa umepangwa kumalizika Jumatano jioni, ili kuipa Tehran muda zaidi wa kuandaa “pendekezo la pamoja” la kumaliza vita.

    Soma zaidi:

  4. Vita vya Iran na usitishaji mapigano - tulifikaje hapa?

    Huu ni muhtasari wa jinsi usitishaji mapigano mawili katika nyanja tofauti za mgogoro wa Mashariki ya Kati ulivyofikiwa

    Marekani na Iran

    Tarehe 8 Aprili: Pakistan kama mpatanishi ilitangaza usitishaji mapigano wa muda wa wiki mbili kati ya Marekani na Iran, uliopangwa kumalizika tarehe 22 Aprili.

    Trump alisema makubaliano hayo yalifikiwa kwa sharti la kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz. Pakistan ilisema Lebanon pia ilihusishwa, jambo ambalo Iran ilikubali lakini Marekani na Israel walipinga.

    Tarehe 11 Aprili: Maafisa wakuu wa Marekani na Iran, akiwemo Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, wanakutana Pakistan. Baada ya mazungumzo ya saa 21, Washington na Tehran bado walikuwa mbali kuhusu masuala muhimu.

    Tarehe 12 Aprili: Trump anatangaza mzingiro wa usafirishaji wa meli za Iran huku Iran ikiendeleza mzingiro wake wa Hormuz baada ya mazungumzo ya Islamabad kushindwa.

    Tarehe 21 Aprili: Trump anakubali kuongeza muda wa usitishaji mapigano bila muda maalum ili mazungumzo yaendelee.

    Israel na Lebanon

    Tarehe 14 Aprili: Lebanon na Israel wanafanya mazungumzo ya kidiplomasia kwa mara ya kwanza tangu 1993, yakilenga kumaliza mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, linalofanya kazi kusini mwa Lebanon.

    Tarehe 16 Aprili: Marekani inatangaza usitishaji mapigano wa siku 10 kati ya Israel na Lebanon, uliopangwa kumalizika tarehe 26 Aprili.

    Trump alitoa wito kwa Hezbollah kuzingatia makubaliano hayo, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema wanajeshi wataendelea kuwepo kilomita 10 ndani ya kusini mwa Lebanon licha ya usitishaji mapigano.

    Soma zaidi:

  5. Iran inataka nini katika makubaliano ya kusitisha mapigano?

    Rais Donald Trump amesema makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yalifikiwa kwa sharti kwamba Tehran ifungue tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya meli za mafuta na mizigo katika Ghuba ya Uajemi.

    Iran iliruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz kwa muda wa wiki mbili, lakini hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu.

    Hata hivyo, Iran imeitaka Marekani kuondoa vikwazo vya kiuchumi, kufidia hasara zilizosababishwa na vita, na kuachia mali za Iran zilizozuiwa na Marekani.

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisafiri kwenda Pakistan kwa duru ya kwanza ya mazungumzo ya amani, lakini alirejea Washington bila mafanikio baada ya mazungumzo ya saa kadhaa.

    Kutokana na kushindwa kufikiwa kwa makubaliano mapya, Marekani ilianza kuweka mzingiro wa baharini dhidi ya Iran na kutishia kuongeza vikwazo vya kiuchumi.

    Duru ya pili ya mazungumzo ya amani pia haikuweza kufanyika wiki hii. Inaonekana Trump anajaribu kununua muda na ameongeza muda wa kusitisha mapigano bila kikomo.

  6. Ndege za kivita zagongana baada ya marubani kupiga picha wakiwa angani

    Mamlaka za Korea Kaskazini zimebaini kuwa ndege mbili za kivita ziligongana angani mwaka 2021 wakati marubani wake wakipiga picha na kurekodi video wakiwa angani.

    Ajali hiyo ilitokea wakati ndege hizo zilipokuwa katika operesheni ya ndege katika jiji la Daegu, kwa mujibu wa Tume ya Usimamizi na Uchunguzi ya Korea Kusini.

    Marubani hao hawakuumia, lakini mgongano huo uliharibu ndege hizo na kusababisha jeshi gharama ya takriban won milioni 880 (sawa na dola 596,000) kwa matengenezo.

    Mmoja wa marubani hao, ambaye baadaye aliondoka jeshini, aliamriwa kulipa faini ya won milioni 88. Inasemekana ajali hiyo ilitokea kwa sababu alitaka kupiga picha za kumbukumbu za safari yake ya mwisho akiwa na kikosi chake cha kijeshi.

    Kamati ya usimamizi iliyotoa ripoti hiyo Jumatano ilisema kupiga picha za safari muhimu za ndege kilikuwa “kitendo cha kawaida kwa marubani wakati huo.”

    Ripoti hiyo iliongeza kuwa rubani huyo alitangaza nia yake kabla ya safari, na marubani walikuwa wakitumia simu zao za mkononi kupiga picha na kurekodi video.

  7. Utawala wa Iran unaonekana kuogopa kuzuka kwa maandamano mapya

    Mamlaka nchini Iran zinaonekana kujaribu kudhibiti simulizi kwa kuzuia upatikanaji wa mtandao na kuonesha picha ya uungwaji mkono wa umma kwa upana.

    Bado haijulikani ni kiasi gani wananchi wanaweza kuvumilia chini ya shinikizo la kiuchumi linaloendelea na udhibiti wa taarifa.

    Siku moja iliyopita, muandamanaji mwingine aliyekamatwa wakati wa maandamano ya kitaifa Januari alinyongwa.

    Idara ya mahakama ya Iran ilimtambua kama Amir Ali Mirjafari, ikimshutumu kwa kuchoma moto msikiti mjini Tehran.

    Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa angalau watu 14 wameuawa katika wiki za hivi karibuni na kuripoti ongezeko la hukumu za kifo dhidi ya waandamanaji, baadhi yao wakituhumiwa kwa ujasusi.

    Mauaji hayo yanaonekana kuwa ishara ya wazi kuwa utawala huo una hofu kubwa ya uwezekano wa uasi.

    Mwezi Januari, utawala huo uliwaua makumi ya maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakidai mabadiliko.

    Viongozi wa wanamgambo wa Basij wameonekana kwenye televisheni ya taifa wakionya kuwa upinzani utashughulikiwa kwa ukali kama vile utawala unavyodai kukabiliana na maadui wa nje kama United States na Israel.

    Soma zaidi:

  8. Papa Leo ailaumu hali ya wafungwa, ataka mabadiliko Guinea ya Ekweta

    Papa Leo amelaani kile alichokiita mazingira “ya kutia wasiwasi” ya kuwashikilia wafungwa nchini Equatorial Guinea, akitaka kuheshimiwa zaidi kwa uhuru na utu wa binadamu.

    Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alitoa kauli hiyo katika Basilica ya Immaculate Conception mjini Mongomo, mji alikozaliwa Rais wa muda mrefu Teodoro Obiang Nguema.

    Katika mahubiri yake, alisisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya binadamu, akisema ni wajibu na dhamira ya kila mmoja.

    “Fikra zangu ziko kwa watu maskini zaidi, familia zinazopitia changamoto, na wafungwa ambao mara nyingi hulazimika kuishi katika mazingira ya kiafya na usafi yanayotia wasiwasi,” alisema Papa Leo.

    Kauli hiyo inakuja wakati akijiandaa kutembelea gereza katika mji wa bandari wa Bata baadaye leo, ambalo mashirika ya haki za binadamu yanasema linajulikana kwa kuwashikilia wapinzani wa kisiasa na wanaopinga serikali.

    Rais Obiang Nguema, ambaye alichukua madaraka mwaka 1979 kupitia mapinduzi, amekuwa akishutumiwa kuongoza nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa mkono wa chuma. Pia anashutumiwa kwa rushwa, huku serikali yake ikikabiliwa na madai ya kuelekeza mapato ya mafuta kwa manufaa ya tabaka la juu.

    Wakati huohuo, Papa Leo amesisitiza tena wito wake wa haki na matumizi ya rasilimali za nchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wote, si wachache waliobahatika pekee.

    “Muumba amewajalia utajiri mkubwa wa asili. Nawahimiza mshirikiane ili uwe baraka kwa wote,” alisema, akionya kuwa mustakabali wa nchi unategemea maamuzi ya wananchi wake.

    “Bwana awasaidie kuwa jamii ambayo kila mmoja, kwa mujibu wa majukumu yake, anafanya kazi zaidi kwa manufaa ya wote badala ya maslahi binafsi, na kuziba pengo kati ya waliobahatika na wasio na bahati,” aliongeza Papa huyo.

    Papa Leo amekuwa akitoa kauli kali dhidi ya ukosefu wa uadilifu katika utawala wakati wa ziara zake barani Afrika, jambo ambalo limevutia hisia za wachunguzi wa kimataifa. Mbinu yake inaonekana kama juhudi za kuendeleza uinjilisti barani humo na pia kuhimiza maadili katika jamii zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali.

    Soma zaidi:

  9. Kesi ya pamoja ya washukiwa 486 wa magenge ya uhalifu yaanza El Salvador

    Kesi ya pamoja dhidi ya washukiwa 486 wanaodhaniwa kuwa wanachama wa genge la MS-13 imeanza nchini El Salvador, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo imesema.

    Picha zilizotolewa na ofisi hiyo zinaonyesha makundi makubwa ya wanaume walioko gerezani wakishiriki kesi hiyo kupitia muunganisho wa video.

    Kundi hilo linatuhumiwa kwa pamoja kufanya zaidi ya uhalifu 47,000, ikiwemo mauaji, uhalifu wa kulazimisha watu kutoa fedha, na usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha kati ya mwaka 2012 na 2022.

    Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kesi za aina hii za pamoja “hudhoofisha haki ya utetezi na dhana ya kutokuwa na hatia kwa washtakiwa.”

    Hata hivyo, ofisi ya Mwanasheria Mkuu imesema ina ushahidi “wa kutosha” utakaowezesha kutolewa kwa “adhabu kali zaidi” kwa watakaopatikana na hatia.

    Soma zaidi:

  10. Iran yasema imekamata meli mbili Hormuz baada ya meli tatu kushambuliwa

    Vyombo vya habari vya Iran, ikiwemo kituo cha Telegram cha televisheni ya taifa ya Iran, vimechapisha taarifa ya Jeshi la Wanamaji la Islamic Revolutionary Guard Corps.

    Katika taarifa hiyo, Jeshi la Wanamaji la IRGC linasema kuwa meli mbili, MSC Francesca na Epaminondas, zimepelekwa katika maji ya Iran kwa ajili ya “ukaguzi wa mizigo, nyaraka na vitambulisho vyao.”

    Inadai kuwa meli hizo zilikuwa “zinafanya kazi bila idhini” na zilifanya “ukiukaji mara kadhaa,” huku zikishutumiwa kujaribu kuondoka katika Mlango wa Bahari wa Hormuz “kwa siri”.

    Shirika la BBC halijaweza kuthibitisha kwa kujitegemea madai hayo.

    Jeshi la Wanamaji la IRGC pia limeonya kuwa linafuatilia kwa karibu shughuli zinazoendelea katika mlango huo wa kimkakati wa Hormuz na limeapa kuchukua hatua kali dhidi ya wanaokiuka sheria.

    Katika taarifa hiyo hakukutajwa meli ya Euphoria, ambayo iliripotiwa awali kushambuliwa pia siku ya Jumatano.

    Unaweza pia Kusoma:

  11. Sudan Kusini yapanga uchaguzi Desemba huku hofu ya vita kurejea ikiongezeka

    Miaka ya ucheleweshaji, Sudan Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi mwezi Desemba mwaka huu, licha ya nchi hiyo kuwa katika hatari ya kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Wataalamu wanaonya uwezekano wa kurejea kwa vita kamili huku majeshi ya serikali chini ya Rais Salva Kiir yakipambana na makundi yanayohusishwa kwa kiwango fulani na Makamu wa Rais Riek Machar.

    Ghasia hizo zimelazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao, huku mashirika ya misaada yakishambuliwa mara kwa mara na kushindwa kutekeleza shughuli zake ipasavyo.

    Waziri wa Habari Ateny Wek Ateny aliwaambia waandishi wa habari mjini Juba kuwa serikali inafanya jitihada za kukusanya fedha kutoka mapato ya mafuta na yasiyo ya mafuta ili kufadhili uchaguzi huo.

    “Serikali ina fedha kwa sababu mafuta bado yanazalishwa, ingawa kuna changamoto,” akiongeza kuwa “mapato yasiyo ya mafuta yapo,” na kwamba uchaguzi utafadhiliwa na serikali, asema Ateny Wek Ateny.

    Makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yalimaliza vita vya mwisho kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake Riek Machar.

    Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka 2022 lakini uliahirishwa mara kadhaa.

    Hata hivyo, Waziri wa Habari amesisitiza kuwa uchaguzi lazima ufanyike mwaka huu.

    Iwapo uchaguzi utafanyika, huo utakuwa uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Sudan miaka 15 iliyopita.

    Hata hivyo, baadhi ya masharti ya makubaliano ya amani bado hayajatekelezwa, ikiwemo kuunganishwa kwa majeshi hasimu, huku nchi hiyo pia ikikabiliwa na changamoto kubwa za rushwa na umaskini.

    Soma zaidi:

  12. Rwanda yaagiza 30% ya magari ya taasisi za umma yawe ya umeme

    Serikali ya Rwanda imeziagiza taasisi zake kuhakikisha kuwa angalau asilimia 30 ya magari mapya yanayonunuliwa ni ya umeme.

    Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli pamoja na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Miundombinu, taasisi zote za serikali zinapaswa kuoanisha mipango yao ya ununuzi wa magari na sera ya taifa ya ununuzi endelevu.

    Agizo hilo limetolewa kupitia barua ya tarehe 14 Aprili iliyoandikwa na Naibu Waziri wa miundombinu, Jean de Dieu Uwihanganye.

    Hatua hii inakuja wakati bei za mafuta zikiendelea kupanda nchini humo na katika ukanda.

    Bei ya petroli imepanda hadi faranga 2,938 kwa lita kutoka 1,989 mwezi uliopita, huku dizeli ikiongezeka kutoka faranga 1,948 hadi 2,205 kwa lita.

    Wakati huo huo, matumizi ya magari ya umeme yanaongezeka kwa kasi nchini Rwanda.

    Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa hadi mwisho wa mwaka 2024, zaidi ya magari 7,000 ya umeme yalikuwa tayari yamesajiliwa.

    Ili kuhamasisha matumizi yake, serikali pia imepunguza kodi kwa magari hayo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhamia kwenye usafiri rafiki kwa mazingira.

    Soma zaidi:

  13. Kim Jong-un afichua anakotoa fedha za ujenzi wa makombora

    Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Korea Kaskazini inajipatia mamilioni ya dola kupitia fedha za mtandaoni ili kufadhili programu zake ghali za kutengeneza makombora.

    Wachunguzi wanaoshughulikia suala hilo walisema kuwa dola milioni 50 za kidijitali ziliibwa kati ya mwaka 2020 na 2021 kupitia udukuzi wa mtandaoni.

    Maafisa wanasema kuwa mbinu hii ya kuvamia mifumo ya benki ni chanzo kikubwa cha mapato kwa Korea Kaskazini, kinachotumika kufadhili silaha zake za nyuklia na makombora ya masafa marefu.

    Iliripotiwa kuwa taarifa hizo ziliwasilishwa kwa Kamati ya Vikwazo ya Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa.

    Mashambulizi hayo ya mtandaoni yalilenga angalau maeneo matatu Marekani, Ulaya na Asia.

    Ripoti hiyo pia ilinukuu utafiti uliotolewa mwezi uliopita na kampuni ya usalama ya Chainalysis, uliobaini kuwa udukuzi wa mtandaoni wa Korea Kaskazini ulisababisha upotevu wa dola milioni 400 za sarafu za kidijitali mwaka uliopita.

    Umoja wa Mataifa ulisema katika mojawapo ya ripoti zake za mwaka 2019 kuwa Korea Kaskazini ilipata dola bilioni mbili kupitia ulaghai wa mtandaoni ili kufadhili maendeleo ya silaha zake za maangamizi makubwa.

    Soma zaidi:

  14. Tangazo la Trump kusitisha mapigano 'halina maana yoyote' - Iran

    Mshauri mwandamizi wa Iran amesema kuwa tangazo la kusitisha mapigano lililotolewa na rais wa Marekani Donald Trump “halina maana yoyote” na linaonekana kuwa ni mbinu ya kuvuta muda ili kutekeleza shambulio la kushtukiza.

    Mahdi Mohammadi, ambaye ni mshauri wa spika wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwa lugha ya Kiajemi kwamba kuendelea kwa kile alichokiita “hali ya kuzingirwa” inayofanywa na Trump hakutofautiani na mashambulizi ya mabomu, na kunapaswa kujibiwa kijeshi.

    Aidha aliongeza kuwa “wakati umefika kwa Iran kuchukua hatua mapema.”

    Wakati huo huo, Jeshi la wanamaji la Marekani limekuwa likizuia eneo la Mlango Bahari wa Hormuz, na wanajeshi wake walivamia meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Iran siku ya Jumapili.

    Hii inakuja baada ya Iran kufunga kwa muda njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani kwa wiki kadhaa.

  15. Rais wa Taiwan afuta ziara yake Afrika baada ya kufungiwa anga

    Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, amefuta ziara yake katika taifa la Eswatini, akidai kuwa Beijing imeweka shinikizo kwa mataifa jirani ili kuzuia ndege yake kupita katika anga lao.

    Nchi za Seychelles, Mauritius na Madagascar zilifuta vibali vya anga kwa ndege ya Lai baada ya “shinikizo kubwa” na mbinu za kiuchumi kutoka China, kwa mujibu wa afisa wa Taiwan.

    China ilikanusha kutumia shinikizo hilo, huku ikiyasifu mataifa hayo matatu na kusema ina “thamani kubwa” kwao.

    Hii ni mara ya kwanza kufahamika hadharani ambapo kiongozi wa Taiwan amelazimika kufuta safari ya nje kutokana na kufutwa kwa vibali vya kupita anga za nchi nyingine.

    Eswatini, iliyojulikana zamani kama Swaziland, ndiyo mshirika pekee wa kidiplomasia wa Taiwan barani Afrika.

    Ni moja ya nchi 12 pekee nyingi zikiwa ndogo katika Amerika ya Kusini au Pasifiki zinazoitambua Taiwan.

  16. Matumaini ya mazungumzo ya amani Pakistan yafifia

    Donald Trump amejigamba kuhusu mabadiliko ya utawala huko Tehran lakini sasa anashughulika na kile anachokiita kupasuka kwa utawala.

    Sasa kwa kuwa viongozi wengi wakuu wa Iran wamefariki , swali la nani anayeongoza Iran kwa sasa ni halisi zaidi, jambo linalofanya jitihada za kidiplomasia kuwa ngumu zaidi.

    Huenda ni mapema kutathmini athari za hatua ya hivi karibuni ya rais, lakini dalili za awali kutoka Tehran hazionekani kuwa nzuri.

    Mshauri wa spika wa bunge na pia kiongozi wa mazungumzo, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema kuwa Trump anajaribu kuvuta muda kwa ajili ya kutekeleza shambulio jingine la kushtukiza.

    Msemaji wa jeshi alirejelea onyo kwamba Iran ilikuwa tayari kushambulia ikiwa hilo litatokea.

    Aidha Islamabad, mipango bado inaendelea kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo, huku sehemu za jiji zikiwa bado zimefungwa. Lakini matumaini ya mkutano wiki hii yanaonekana, kwa sasa, yamefifia.

  17. Iran haijaamua kushiriki duru ijayo ya mazungumzo na Marekani - Msemaji

    Kabla ya Donald Trump kutangaza kwamba ataongeza muda wa kusitisha mapigano, wizara ya mambo ya nje ya Iran iliiambia BBC kwamba Tehran bado haijaamua kama itahudhuria duru mpya ya mazungumzo ya amani na Marekani baadaye wiki hii.

    Katika mahojiano na mwandishi wa kimataifa wa BBC Lyse Doucet, msemaji Esmail Baghaei alisema Iran imeingia katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya Islamabad "kwa nia njema na hisia ya uzito, lakini kuna upande wa mazungumzo umeonyesha kukosa umakini na nia njema".

    Aidha alitaja "mapumziko yasiyo na maana, vitisho vya uhalifu wa kivita" kutoka kwa Marekani akirejelea mfululizo wa machapisho na mahojiano ya Trump kwenye mitandao ya kijamii katika siku mbili zilizopita, ambapo alitishia tena “kuharibu kila kituo cha umeme na kila daraja” ikiwa Iran haitakubali kile alichokiita pendekezo la Marekani “la haki na lenye busara sana.”

    White House ilithibitisha Jumanne usiku kuwa safari ya makamu wa rais JD Vance kwenda Pakistan kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani imefutwa.

  18. Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kwaongeza uhitaji wa mafuta Marekani - Wataalamu

    Kupitia chapisho kwenye jukwaa la mtandao wa Truth Social Jumatatu usiku, Rais Donald Trump alisema uongozi wa Iran "umelazimisha mamia ya meli" kuelekea majimbo yenye utajiri wa mafuta ya Marekani, kama vile Texas, Louisiana, na Alaska.

    Ingawa haijulikani ni aina gani ya meli alizokuwa akizirejelea, wachambuzi wa meli na biashara wanaiambia BBC Verify kwamba hatua ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz imesababisha ongezeko la uhitaji wa mafuta ghafi nchini Marekani.

    Hatua hiyo ni kikwazo kikubwa cha usafirishaji wa mafuta ya Ghuba, lakini usafirishaji umevurugika zaidi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

    Kwa kuwa hawawezi kupata mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati kupitia mlango huo, waagizaji wamelazimika kutafuta wauzaji mbadala.

    Data kutoka kwa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za bahari Kpler inaonyesha kuwa meli 71 za mafuta zinazojulikana kama Very Large Crude Carriers (VLCCs) zinaelekea Marekani kuchukua mizigo ikilinganishwa na wastani wa meli 27 kwa siku katika kipindi cha mwaka jana.

  19. Majadiliano na Marekani hayana mantiki kwa sasa – Iran

    Mahmoud Nabavian, mbunge wa Iran ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani huko Islamabad, ameeleza kupitia mtandao wa X kwamba "kuanzia sasa", kujadiliana na Marekani ni "jambo la hatari na lisilo na mantiki".

    Kando na hayo, msemaji wa makao makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, kamandi kuu ya kijeshi ya Iran, ameonya kwamba vikosi vya Iran, iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Iran, "vitashambulia maeneo yaliyopangwa awali na kutoa somo, hata kali zaidi" kwa Marekani na Israeli.

    Katika chapisho la Nabavian na taarifa ya Khatam al-Anbiya, hakukutajwa muda wa kusitisha mapigano, ingawa vyote viliripotiwa na vyombo vya habari vya Iran baada ya tangazo la Donald Trump.

    Bado Iran haijatoa kauli yoyote kupitia wizara ya mambo ya nje ya Iran au maafisa wake, au kutoka kwa msemaji mkuu wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf.

  20. Waziri mkuu wa Pakistan amshukuru Trump kwa kuongeza muda wa kusitisha mapigano

    Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amemshukuru rais wa Marekani Donald Trump baada ya kutangaza kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa muda usiojulikana muda mfupi kabla ya muda wa awali kuisha.

    "Ninamshukuru Rais Trump kwa dhati kwa kukubali ombi letu la kuongeza muda wa kusitisha mapigano ili kuruhusu juhudi zinazoendelea za kidiplomasia kuchukua mkondo wake," anasema katika taarifa ya mtandaoni.

    "Kwa imani na imani iliyopo, Pakistan itaendelea na juhudi zake za dhati za utatuzi wa migogoro kwa mazungumzo," taarifa hiyo inaongeza.

    "Ninatumai kwa dhati kwamba pande zote mbili zitaendelea kuzingatia usitishaji mapigano na kuweza kuhitimisha 'Makubaliano ya amani' kamili wakati wa duru ya pili ya mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Islamabad kwa ajili ya kukomesha kabisa mgogoro huo."