Hasira dhidi ya UN yaongezeka, onyo la uhalifu wa kivita latolewa DRC
Na Emmanuel Igunza na Patrick Jackson
BBC News, Nairobi na London

Chanzo cha picha, Reuters
Polisi katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekabiliana na waandamanaji katika siku ya tatu ya maandamano ya kupinga Umoja wa Mataifa.
Takriban watu 19 wakiwemo wanajeshi watatu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa wameuawa, maafisa wanasema.
Maandamano yalizuka katika mji wa Goma huku watu wakishutumu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kudhibiti ghasia za makundi yenye silaha.
Umoja wa Mataifa unaonya mashambulizi dhidi ya ujumbe wake, kwa zaidi ya miongo miwili, yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.
Mashambulizi yalifanywa kwenye vituo vyake viwili, huko Goma na Butembo, ambapo walinda amani wawili wa India na mjumbe wa tatu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa waliuawa.
Zaidi ya watu 50 wamejeruhiwa tangu mapigano hayo yaanze siku ya Jumatatu.
Siku ya Jumatano, waandamanaji walilenga tena vituo vya Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.
Msemaji huyo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa mamlaka ya Kongo kuchunguza matukio hayo.
Hakukuwa na ushahidi wa awali kwamba walinda amani wake waliwafyatulia risasi waandamanaji, afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Umoja wa Mataifa ulilaumu ghasia na uporaji wa mali yake kwa wahalifu wanaojifanya kuwa waandamanaji.
Ilisema walikuwa wamekamata silaha kutoka kwa polisi wa eneo hilo na kufyatua risasi.
"Makundi ya watu yanarusha mawe na mabomu ya petroli, kuvunja ngome, uporaji na kuharibu, na kuchoma vituo kwa moto," Farhan Haq, naibu msemaji wa Bw Guterres, katika taarifa yake.
"Hali ni tete sana na uimarishaji unaratibiwa. Vikosi vyetu vya kukabiliana haraka viko katika hali ya tahadhari na wameshauriwa kujizuia zaidi, kwa kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji na kufyatua risasi za onyo tu wakati wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa au mali inashambuliwa."
Wanajeshi wa Congo walikuwa wakisaidia kulinda vituo vya Umoja wa Mataifa, Bw Haq aliongeza.
Polisi wa eneo hilo pia wamewashutumu baadhi ya wanachama wa makundi yenye silaha kwa kujipenyeza katika maandamano hayo ili kuchochea chuki dhidi ya walinda amani hao, ambao kikosi chao kinajulikana rasmi kwa jina la Monusco.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linapambana na kundi la waasi la M23 na Allied Democratic Force (ADF), kundi lenye mafungamano na wanaojiita Islamic State, na wanamgambo wengine wengi.
Hasira imeenea kutokana na kushindwa kwa Umoja wa Mataifa kusitisha ghasia zinazofanywa na makundi yenye silaha yanayoendesha shughuli zake katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini.
"Wanatupiga mabomu ya machozi kwa sababu tulikuja kusema kuwa Monusco haitusaidii," muandamanaji Anselme Musimbwa aliliambia shirika la habari la Reuters huko Goma Jumanne.
"Wamekuwa Congo kwa miaka 22 na hakuna kinachofanya kazi." Muandamanaji mwenzake Jack Sinzahera alisema: "Tuna polisi wetu ambao watasimamia usalama na mali zetu.
Hatutaki chochote cha kufanya na Monusco." Walinda amani wa Umoja wa Mataifa mara nyingi wamekuwa wakilengwa na waasi nchini DR Congo na mara nyingi wamekuwa wakikabiliwa na shutuma za kushindwa kuwalinda raia - ukosoaji ambao Umoja wa Mataifa umekuwa ukipuuzilia mbali kila mara.
Lakini maandamano ya hivi punde yanaleta matatizo makubwa kwa ujumbe mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa na unaofadhiliwa kwa kiasi kikubwa zaidi wa kulinda amani.












