Mtego wa Mapenzi wa Bhagwa: Mtindo mpya kwenye mitandao ya India unaowadhuru watu
Na Shruti Menon
BBC , Delhi

Chanzo cha picha, Twitter
Nadharia yenye utata ambayo baadhi ya makundi ya Kihindu huiita "Love Jihad" - ambayo inadai kuwa wanaume wengi Waislamu wanashiriki katika njama ya kuwatongoza wanawake wa Kihindu na kuwabadilisha - imeenea nchini India kwa miaka mingi, licha ya kukosekana kwa ushahidi. Sasa nadharia ambayo ni kinyume - kwamba wanaume wa Kihindu wanajaribu kwa makusudi kuwatongoza wanawake wa Kiislamu - inaenea mtandaoni. Unaitwa ‘’Bhagwa Love Trap’’ au "Mtego wa Mapenzi wa Bhagwa."
Ushahidi wa madai hayo ni mdogo, Lakini hilo halijayazuia madai hayo kusabisha kuenea kwa vurugu katika jamii halisi ya Wahindi.
"Ilikuwa mbaya sana. Sikuamini macho yangu," anasema Maryam, mwanamke Muislamu kutoka kaskazini mwa India, akikumbuka msururu wa jumbe za matusi alizopokea mtandaoni.
Maryam - sio jina lake halisi - ndiye aliyelengwa na shambulio la kufichuliwa kwa , maelezo ya utambulisho wake binafsi mtandaoni.
Picha zake akiwa amesimama kando ya wanaume wa Kihindu zilinakiliwa kutoka kwa akaunti za mitandao ya kijamii ya umma, na zilitumiwa kudai kwamba alijihusisha na mahusiano ya dini tofauti - mwiko mkubwa kwa wale wanaomshambulia mtandaoni. Madai hayo hayakuwa ya kweli.
Wanaume katika picha hizo walikuwa marafiki, si wapenzi wa kimapenzi, lakini hilo haikuwazuia waliomtuhumu kutoa madai ya uongo. "Walisema nalala na wanaume wa Kihindu. Walikuwa wakiwanyanyasa wazazi wangu, na kuhoji malezi yangu," anasema.
Mahusiano ya dini mbalimbali bado ni mwiko mkubwa miongoni mwa familia za kihafidhina za Kihindi.
Kulingana na utambulisho wa baadhi ya akaunti zilizomkashifu, Maryam anaamini wanaume Waislamu walikuwa nyuma shambulio hilo la "Mtego wa Mapenzi wa Bhagwa".

Chanzo cha picha, YOUTUBE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Bhagwa" inamaanisha zafarani, rangi ambayo imekuja kuhusishwa na Hindutva. Hindutva ni itikadi ambayo - kwa wakosoaji wake - inakuza aina ya utaifa wa Kihindu uliokithiri. Katika muktadha huu neno, "Bhagwa" linatumika kama alama ya Hindutva.
Nadharia ya "Bhagwa Love Trap" inaelezea kwamba wanaume wanaoamini katika Hindutva wanajaribu kuwatongoza wanawake wa Kiislamu, na kuwavuta mbali na jamii zao. Wazo hilo kimsingi linasukumwa na wanaume Waislamu, ambao wengi wao wanahofia kuwa kitendo hicho kinafanyika.
BBC ilizungumza na wamiliki wa akaunti zinazotetea nadharia hii na kutathmini mifano iliyotolewa nao. Hatukupata ushahidi wa kuonyesha ukweli halisi wa njama hii inayoendelea kutekelezwa kichini chini.
Lakini kampeni hiyo imeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii – msemo huo umetumika zaidi ya mara 200,000 tangu Machi mwaka huu.
Athari za kampeni hiyo imeleta athari katika maisha halisi ya watu.
Mnamo Mei, video iliyorekodiwa huko Madhya Pradesh ilichapishwa mtandaoni ikionyesha wanafunzi wawili wa udaktari, mwanamke Muislamu na mwanamume Mhindu, wakiteembea kuelekea katika chuo chao cha skuta.
Katika video hiyouUmati wa wanaume wanaoonekana kuwa Waislamu umewazunguka, na mwanamke huyo anakaripiwa kwa kuaibisha dini yake. "Hakuna mtu atakayekuruhusu kuuangusha Uislamu," mmoja wao anapiga kelele, huku wengine wakimshambulia Mhindu.

Chanzo cha picha, Twitter
BBC imeona video zadi 15 za makabiliano kutoka maeneo mbali mbali ya India ambayo yanafuata kampeni hiyo.
Video zinazodai nadharia hiyo ni ya kweli, zikijumuisha matukio haya na mengine, zimetazamwa zaidi ya mara milioni 10 kwenye YouTube, Instagram na X, zikiambatana na alama ya reli #BhagwaLoveTrap.
Nadharia hiyo inakwenda kinyume na ile ya zamani, iliyojulikana zaidi kama "jihadi ya mapenzi".
Inaendeleza dhana kuwa wanaume Waislamu wanajaribu kuwatongoza wanawake wa Kihindu, na imekuwa ikisukumwa mtandaoni na wazalendo wa Kihindu kwa miaka mingi. Kama vile nadharia ya "Bhagwa Love Trap", madai haya yameenea bila uthibitisho na yamesababisha vurugu halisi miongoni mwa jamii.
Ndoa za dini tofauti bado ni nadra nchini India, huku watu wengi wakichagua ndoa za kupanga.
Uchunguzi huru wa mashirika mawili ya habari ya India haukuweza kupata ushahidi wa kuunga mkono nadharia hiyo.
Licha ya hayo, kile kinachojulikana kama "jihadi ya mapenzi" kimekuwa mhimili thabiti katika mjadala wa kisiasa wa India.
Imejadiliwa hadharani na wanasiasa kutoka chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi, BJP, na baadhi ya wanachama wake ambao wanajiunga na itikadi ya Hindutva.
Nadharia ya "Bhagwa Love Trap" imechangiwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, mara nyingi na akaunti zisizojulikana, lakini baadhi ya viongozi wa juu wa Kiislamu wameikuza nadharia hiyo pia.
Shoaib Jamai, mwanazuoni wa Kiislamu na mchambuzi wa mara kwa mara wa vituo vya habari vya India, anajisifu kwa kueneza wazo hilo katika vyombo vya habari vya kitaifa, lakini anasema haungi mkono madhara yake ambayo mwelekeo wa kampeni hiyo umesababisha.
"Siungi mkono watu kutoka jamii ya Kiislamu ambao wanajaribu kuchukua sheria mkononi. Nchi hii inaendeshwa kwa sheria," anasema.
Lakini juu ya ukweli wa nadharia yenyewe, Bw. Jamai hana shaka. Vijana wa Kihindu "wanatiwa akili" na "kikosi cha Hindutva," anadai, "kuwavuta wanawake wa Kiislamu kwenye mitego".
Bw Jamai na wafuasi wengine wa nadharia hiyo wanatoa madai yao kwa kutumia mfano wa video halisi zinazosambaa mtandaoni, ambazo zinaonyesha viongozi wa Hindutva wakiwahimiza wanaume wa Kihindu kuwafuatilia kimaisha wanawake Waislamu - kama vile nadharia ya "Bhagwa Love Trap" inavyopendekeza.
Mmoja wao anamuonyesha mwanachama wa chama tawala nchini India cha BJP akizungumza katika mkutano wa kisiasa mwaka 2007Yogi Adityanath akisema: Ikiwa Waislamu "watamchukua msichana mmoja wa Kihindu," anasema, "tunapaswa kuchukua wasichana mia wa Kiislamu". Umati unashangilia.

Chanzo cha picha, HINDUTVA WATCH
Bw Adityanath tangu wakati huo amepanda cheo na kuwa waziri mkuu wa Uttar Pradesh. BBC ilimuuliza ikiwa bado anashikilia msimamo wa kauli hiyo aliyoitoa, lakini hakujibu.
Tulichunguza mifano 10 mahususi tuliyoshirikishwa na Bw Jamai na wafuasi wengine wa nadharia ya "Bhagwa Love Trap" ili kuunga mkono imani yao kwamba jambo hilo ni la kweli.
Haya yalikuwa ni matukio ya wanaume wa Kihindu ambao, wafuasi wa nadharia hiyo walisema, waliingia kimakusudi mahusiano au ndoa na wanawake wa Kiislamu ili kuwabadili na kuwadhuru kwa sababu ya utambulisho wao wa kidini.
Ingawa mifano yote iliyotajwa kwetu ilihusisha uhusiano kati ya wanaume wa Kihindu na wanawake wa Kiislamu, katika visa viwili, lakini wanawake hawakubadili dini.
Katika matukio sita ambapo ilidaiwa kuwa wanaume hao wa Kihindu waliwaua wenzi wao kwa sababu ya utambulisho wao wa kidini, kesi nne kati ya hizo zilihusiana na migogoro ya kifedha au ya kinyumbani iliyosababisha mauaji, kulingana na taarifa za polisi.
Sababu za vurugu katika kesi nyingine nne hazikuweza kuthibitishwa kupitia habari au ripoti za polisi, lakini hapakuwa na uthibitisho kwamba nadharia ya ‘’Bhagwa Love Trap’’ ilikuwa na uhusiano wowote na matukio hayo.
Msururu mwingine wa video zinazoangazia madai kuhusu "Bhagwa Love Trap", zimekanushwa na tovuti ya India ya kuangalia ukweli ya Boom Live .
Vikundi vya Hindutva vinakanusha kuwepo kwa ‘’mtego wa mapenzi’’.
"Hakuna ushahidi kabisa wa mtego kama huo kuendeshwa na Wahindu," anasema Alok Kumar, mkuu wa Vishwa Hindu Parishad, shirika la Hindutva. Madai
Labda kwa kutabirika, Bw Kumar anaamini "jihad ya upendo" ni ya kweli. "Kuna sehemu kubwa ya wanaume Waislamu… ambao huwavuta wanawake wa Kihindu kwenye mtego wao," anasema.
"Jihad ya Mapenzi ina uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa," anasema Fatima Khan, mmoja wa waandishi wa habari wa kwanza kuandika kuhusu Bhagwa Love Trap, akionyesha uungwaji mkono wake miongoni mwa wanachama wa chama tawala cha India.
"Kwa upande mwingine, Bhagwa Love Trap ni nadharia mpya ya njama. Ni kitu ambacho hakina uungwaji mkono wa kisiasa hata kidogo."
Sawa na mijadala mingi nchini, suala hilo limegubikwa na upendeleo wa kisiasa - lakini ni jambo linaloonekana wazi. Mgawanyiko wa kidini nchini India unathibitisha kuwa msingi mzuri wa nadharia kama hizi kustawi mtandaoni, na kusambaa kwa madhara halisi miongoni mwa jamii.
Maryam, mwanamke wa Kiislamu ambaye alilengwa katika shambulio la kutangazwa kwa taarifa za kibinafsi za utambulisho wake ni ushahidi wa wazo hilo. Alihuzunishwa sana na jumbe alizokuwa akipokea, alichukua muda wa mapumziko ili kuepuka makabiliano yanayoweza kutokea.
"Kwa mara ya kwanza nilijihisi siko salama katika jamii yangu. Nilikuwa nimechanganyikiwa sana na niliogopa kutoka," anasema: "Unadai kwamba unalinda wanawake, kwa kuharibu kimsingi maisha yao."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












