Je, unaweza kumpa mbwa wako ale nyama iliyotengenezwa kwenye maabara?

Chanzo cha picha, NICOLA
Nicola Wordsworth anasema mbwa wake Tibetan Terrier Bertie anashiriki lishe yake.
"Mimi ni mtu wa kubadilisha badilisha mlo wa mboga mboga au vyakula visivyo vya nyama. Situmii maziwa na mara chache huwa nakula nyama," anasema Nicola mwenye umri wa miaka 54 kutoka Kent.
"Bertie huwa anakula mbogamboga pia. Na anapokuwa na nyama kwenye chakula chake, ninahakikisha ina ubora mzuri, sawa na chakula changu."
Mapema mwaka huu, Utafiti wa Uingereza uligundua kuwa 61% ya wamiliki wa wanyama wa nyumbani sasa wanataka kujua kuhusu athari za mazingira ya chakula wanachonunua kwa wanyama wao. Kwa kuzingatia nyayo za tasnia ya chakula cha wanyama, hii inaweza kuwa jambo zuri.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sekta ya chakula cha wanyama wa nyumbani duniani inatoa gesi joto zaidi kuliko mataifa kama Msumbiji na Ufilipino, kulingana na ripoti moja.
Utafiti huo pia uliainisha kwamba kila mwaka eneo la ukubwa wa Uingereza mara mbili hutumiwa kutengeneza chakula cha paka na mbwa, bila kusema chochote juu ya vyakula vya maji maji.
Wakati huo huo, uchunguzi tofauti wa Marekani ulisema kuwa chakula cha paka na mbwa kinachangia hadi 30% katika athari za mazingira za uzalishaji wa nyama.
Hivyo ni wakati wa kuchukua hatua ya kubadilisha mlo wa nyama ya kawaida wanayopewa wanyama wetu wa nyumbani, na kuwa na mbadala endelevu zaidi, kama vile vyakula vya mbogamboga, wadudu, na hata nyama iliyokuzwa kwenye maabara?
Nyama nyingine inayojulikana kama nyama ya Good Dog Food yenye makao yake London inatarajiwa kuletwa sokoni katika miaka michache ijayo.
Ina ubia kati ya kampuni mbili za kibayoteki, Agronomics na Roslin Technologies, timu yake ya utafiti tayari inakuza kuku waliotengenezwa maabara.

Chanzo cha picha, JACQUI MATTHEWS
Mchakato wa utengenezaji wa nyama iliyokuzwa kwenye maabara huanza na seli shina, kwa kawaida huchukuliwa kutoka kwa kiinitete, lakini pia kutoka kwa wanyama wazima, ambao hukuzwa katika maabara. Kwa njia inayofanana na kile kinachotokea ndani ya mwili wa mnyama, hulishwa virutubishi kama vile asidi, glukosi na vitamini.
Mbinu hiyo inazalisha nyama bila mifugo, bila ya haja ya kufuga na kuchinja wanyama. Na timu ya Chakula Bora cha Mbwa inasema hakuna haja ya kupata seli za ziada kwa sababu "inazitengeneza upya kabisa".
"Nyama ya kutengenezwa hutoa fursa ya kulisha paka na mbwa vyakula vinavyotokana na wanyama bila athari za kimaadili na kimazingira zinazohusiana na kuwalisha nyama ya asili," anasema Prof Jacqui Matthews, afisa mkuu wa zamani wa kisayansi wa Roslin Technologies.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kwa kulinganisha, chakula cha wanyama wa nyumbani kisichokuwa na nyama kinaweza kuwa na virutubisho vilivyoongezwa. Kuna ushahidi mdogo wa kuonesha kwamba hii ni chaguo salama, la muda mrefu."
Owen Ensor, mtendaji mkuu wa Chakula Bora cha Mbwa, anasema nyama iliyotengenezwa kwenye maabara hutumia ardhi kidogo, maji, na umeme, na inapunguza uchafuzi wa mazingira unaohusiana na kilimo, ukataji miti na upoteaji wa viumbe hai. Inatarajiwa pia kuwa uzalishaji hautahitaji matumizi ya antibiotics yoyote.
"Kwa kuwa hatuli nyama tumetatizika kukubaliana na hilo kwani tunammiliki mnyama mmoja nyumbani na kuna gharama ya kimazingira. Hivyo tunatumaini Chakula Bora cha Mbwa kinaweza kutatua hilo."

Chanzo cha picha, OMNI
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kidogo, bidhaa moja kama hiyo, nyama ya kuku inayotengenezwa kwenye maabara, tayari imekuwa ikiuzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu nchini Singapore. Na huko Marekani, wakala wa udhibiti wa Utawala wa Chakula na Dawa mwezi uliopita uliidhinisha kuanza kutengeneza kuku sawa na kuku kwa ajili ya wanadamu.
Mtaalamu wa lishe ya mbwa Alyssa Ralph anasema sio kawaida kwa mmiliki kutumia chaguo lake la chakula kwa mnyama wake.
"Mlo wa chakula cha wanyama wa nyumbani mara nyingi hufuata mielekeo ya chakula cha binadamu kwa karibu sana," anasema mtaalamu wa lishe ya mbwa, Alyssa Ralph.
"Hivi majuzi, tumeona hali hii na lishe ya wasiotumia nyama."
Chapa moja ya chakula cha mbwa inayotokana na mimea, Omni yenye makao yake London, inasema imeona ukuaji zaidi ya mara sita katika mauzo tangu Septemba 2021 na kuuza zaidi ya milo 90,000 ya mbwa wasio na nyama hadi sasa.
Mwanzilishi wake mwenza, Guy Sandelowsky, pia ni daktari wa wanyama wadogo wa nyumbani. Anasema kujaribu kulisha wanyama kwa nyama ambayo babu zao wa mwitu wangekula sio lazima.
"Tunajua wanahitaji protini lakini inawezekana kuwapa mbwa protini zote wanazohitaji kutoka kwa vyakula vinavyotokana na mimea."

Chanzo cha picha, GUY SANDELOWSKY
Tuwalishe mbwa wetu kile ambacho watangulizi wao wangekula porini ni mada yenye utata.
"Hoja kuu ni kwamba tunapaswa kuwalisha mbwa wetu wa nyumbani chakula cha mababu zao, kulingana na kile mbwa mwitu wa kisasa hutumia," asema Bi Ralph.
"Hata hivyo, wakati mbwa wetu na mbwa mwitu wa kijivu wanashiriki babu moja, tulianza kufuga mbwa kati ya miaka 15,000 na 40,000 iliyopita, na baadhi ya mbwa wa kwanza wa nyumbani walitoka kwa mbwa mwitu wakionekana hadi miaka 100,000 iliyopita."
Wakati huo huo, utafiti wa 2013 uligundua kuwa mbwa wa nyumbani wamebadilika kijenetiki ili kukabiliana na chakula cha kabohaidreti. Paka, kwa upande mwingine, ni wanyama wanaokula nyama bila shaka.
Nicole Paley, naibu mtendaji mkuu wa Chama cha Watengenezaji Chakula cha wanyama wa nyumbani, anadokeza kuwa tasnia ya chakula hicho inasifika kwa kupunguza taka kutoka kwa msururu wa chakula cha binadamu.
"Hata hivyo," anaongeza Bi Paley, "wakati mikazo ya rasilimali na upatikanaji wa chakula inavyoendelea, tumejitolea kutafuta suluhu zaidi."
Bi Paley anaelezea ubunifu wa hivi karibuni katika vyanzo vya protini, ikijumuisha kutoka kwa mwani, mimea ya majini, nzi na nyama iliyokuzwa kwenye maabara.
Hata hivyo, huko Kent, Nicola Wordsworth anasema angehisi kuwa"mnyonge" kidogo akila nyama iliyotengenezwa, au kumpa Bertie. Badala yake anasema kwamba wote wawili watashikamana na kula vyakula vya mimea zaidi. "Anafurahia. Ana furaha na afya."












