Mwanamke ambaye picha zake zilizoibiwa zilivyotumiwa kuwalaghai wanaume maelfu ya pesa

Jenney

Chanzo cha picha, BBC/Jenny Law

Kwa zaidi ya muongo mmoja, picha zilizoibwa za nyota wa zamani zimetumiwa kuwalaghai waathiriwa maelfu ya dola. Je, unahisije kuwa uso usiojua wa matapeli wengi wa mapenzi?

Takriban kila siku, Vanessa hupokea ujumbe kutoka kwa wanaume wanaoamini kuwa wana uhusiano naye - wengine hata hufikiri kuwa ni mke wao. Wana hasira, wamechanganyikiwa na wengine wanataka kurejeshewa pesa zao - ambazo wanasema walimtuma kulipia gharama za kila siku, bili za hospitali, au kusaidia jamaa.

Lakini yote ni uwongo. Vanessa hawafahamu wanaume hawa. Badala yake, picha na video zake - zilizoondolewa kutoka kwa maisha yake ya zamani katika burudani ya watu wazima - zimetumika kama mtego katika ulaghai wa mapenzi mtandaoni kuanzia katikati ya miaka ya 2000. Waathiriwa waliibiwa pesa kupitia wasifu ghushi mtandaoni kwa kutumia jina la Vanessa au mfano wake, katika aina ya kashfa ya mapenzi inayoitwa catfishing.

Mafuriko ya jumbe zenye visa vya pesa zilizopotea na maisha yaliyoharibiwa yamewaathiri.

"Nilianza kuwa na huzuni, na kujilaumu - labda kama picha zangu hazingekuwa huko, wanaume hawa hawangetapeliwa," Vanessa anasema - hatutumii jina lake la ukoo kulinda utambulisho wake kamili.

Kwa takriban miaka minane, Vanessa alifanya kazi kama "camgirl" - ikimaanisha kutiririsha maudhui machafu moja kwa moja kwenye mtandao kupitia kamera ya wavuti. Kwa sababu alikuwa na haya kidogo alipoanza, aliamua kuunda ubinafsi ulioitwa Janessa Brazil. "Kwa kweli sio mimi, ni Janessa, kwa hivyo sitaona aibu," alisema.

Alichukua jina la ukoo Brazil sio tu kwa sababu ndiko alikozaliwa, lakini pia kwa sababu ni mojawapo ya maneno maarufu ya utafutaji kwenye mtandao. Ulikuwa uamuzi wa busara. "Nachukia jina hilo," anasema sasa. "Lakini ilinisaidia kupata umaarufu haraka."

Kwa muda, mambo yalikuwa mazuri. Vanessa alifurahia uhusiano na mashabiki wake, ambao wangelipa hadi $20 kwa dakika kutazama na kutangamana naye. "Nataka kuwafurahisha. Nataka kufurahiya nao. Na wananaswa," anasema.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kilele cha kazi yake, anasema alikuwa akipata takriban dola milioni za Kimarekani kwa mwaka. Janessa alikuwa na tovuti yake mwenyewe, chapa iliyofanikiwa na uwepo mzuri mtandaoni. Lakini mnamo 2016 wasifu wake mtandaoni uliingia giza.

Ilituchukua miezi tisa kumpata kwa ajili ya podikasti ya Upendo, Janessa. Hatimaye tulipozungumza na Vanessa katika nyumba yake ya kawaida katika pwani ya mashariki ya Marekani, alituambia kuwa sehemu ya sababu iliyomfanya aache kutengeneza maudhui ya mtandaoni ni kujaribu kuwazuia walaghai. "Sitaki tena kuwapa uwezo wa kutumia chochote changu tena," anasema.

Vanessa alianza kufahamu kwamba matapeli walikuwa wakijifanya yeye wakati mwanamume mmoja alipochapisha kwenye gumzo wakati wa kipindi cha moja kwa moja, akisisitiza kwamba yeye ni mume wake na alikuwa amemuahidi kwamba ataacha kurekodi video. Alifikiri ni mzaha, lakini akamwomba amtumie barua pepe.

Waathiriwa zaidi walijitokeza na hadithi zinazofanana, wakichapisha maoni wakati wa maonyesho yake, na kumwomba athibitishe utambulisho wake. Walaghai pia waliibuka na maombi ya ajabu kwa ajili yake - kama vile kuvaa kofia nyekundu - picha walizotumia kuwalaghai waathiriwa.

Maoni ya mara kwa mara, barua pepe na hali ya wasiwasi ilianza kuathiri biashara yake. "Ilikuwa ndoto mbaya," anasema Vanessa. "Lakini nilijisikia vibaya kwa hawa jamaa. Nifanye nini?"

Mwanzoni alijaribu kujibu kila barua pepe, ambayo ilichukua masaa kila siku. Anasema mumewe wa wakati huo, ambaye pia alikuwa meneja wake, pia alianza kufuatilia jumbe hizo. Aliwaambia waathiriwa wa kashfa kwamba yeye na Vanessa hawakuwajibikia pesa ambazo watu hao walikuwa wamepoteza.

"Kama ningepata pesa zote ambazo hawa jamaa walituma kwa matapeli hawa wote, ningekuwa bilionea leo, sio kukaa hapa kwenye nyumba yangu ndogo," anasema.

Jenny

Chanzo cha picha, BBC/Jenny Law

Vanessa anadhani ni kawaida ya wanaume wengi kutaka kutunza wanawake, jambo ambalo linaeleza kwa nini wanatuma pesa kwa mtu ambaye hawajakutana naye.

"Hata kama hawana pesa, bado wako tayari kutoa, ili tu kujisikia kupendwa," anasema.

Roberto Marini, Muitaliano katika miaka yake ya mapema ya 30, alinaswa na Janessa bandia. Ilianza na ujumbe kwenye mtandao wa Facebook kutoka kwa mwanamke mchanga anayejiita Hannah, ambaye alimpongeza kwa biashara yake ya kuanzisha - shamba endelevu katika kisiwa cha Sardinia.

Baada ya miezi mitatu ya kubadilishana picha na ujumbe wa mapenzi, alianza kuomba pesa. Ilikuwa ni kwa ajili ya mambo madogo mwanzoni, kama simu iliyovunjika, lakini siku ziliposonga alihitaji zaidi. Alimwambia alikuwa na maisha magumu - wakati hakuwa akiwatunza jamaa wagonjwa ilibidi ajitafutie burudani ya watu wazima.

Katika harakati zake za kutaka kuujua ukweli, Roberto pia alimtumia barua pepe, pamoja na watu wengine wengi ambao alifikiri wanaweza kuwa Janessa halisi. Wakati wa mahojiano yetu naye, Vanessa alitazama tena barua pepe zake na akapata ujumbe kutoka kwake kati ya maelfu ya barua pepe.

"Hujambo. Nina haja ya kuzungumza na Janessa Brazil halisi," alikuwa ameandika mwaka wa 2016. Alikuwa amejibu saa moja baadaye, "Mimi ndiye Janessa Brazil halisi."

Alimuuliza maswali machache zaidi akijaribu kujua kama walizungumza hapo awali. Ubadilishanaji huu wa barua pepe ulikuwa wa kwanza na wa pekee kuwasiliana nao.

Lakini huo haukuwa mwisho. Roberto alibaki amenaswa na matapeli. Anasema aliwatumia jumla ya $250,000 kwa muda wa miaka minne, akimaliza akiba yake na kukopa pesa kutoka kwa marafiki na familia, na pia kuchukua mikopo.

Hiyo ni ishara ya ulaghai uliofanikiwa, asema Dkt Aunshul Rege, mtaalamu wa masuala ya uhalifu kutoka Philadelphia ambaye amesomea ulaghai wa mapenzi mtandaoni.

Anasema mara nyingi jumbe hutumwa na mitandao ya wahalifu inayofanya kazi katika timu za kuwatunza wahasiriwa, kushiriki picha na habari. Amepata hata mfano wa miongozo wanayotumia - miongozo ya vitendo ambayo pia huorodhesha visingizio vya kuzuia simu ambayo inaweza kuwafichua.

Ulaghai huo hufuata mtindo - mapenzi, vitisho vya kutengana na kisha kuomba usaidizi wa kifedha, ikidaiwa kuwaruhusu wanandoa hao hatimaye kuwa pamoja. Mbinu hizo ni za kimfumo sana kiasi cha kufahamika kwa utulivu kwa mtu yeyote ambaye amekuwa akipokea, lakini zinafanya kazi.

Dk Rege anafikiri kuna uwezekano ulaghai wa Roberto uliendeshwa na kikundi kilichopangwa. Anasema kuna mitandao mikubwa inayofanya kazi duniani kote, huku idadi kubwa ikitoka Uturuki, China, UAE, Uingereza, Nigeria na Ghana.

Mojawapo ya maeneo ambayo Roberto aliombwa kutuma pesa ni Ghana, nyumbani kwa kundi la matapeli mtandaoni liitwalo Sakawa Boys. Tulifuatilia baadhi yao huko Accra. "Ofa", kijana aliyezungumza kwa upole, alituambia kuwa kuiga watu mtandaoni kunatumia wakati na kunahusisha nidhamu nyingi - ikiwa tu kufuatilia uwongo. Alikiri kazi hiyo ilimfanya "kujisikia vibaya", lakini alikuwa amepata zaidi ya $50,000.

Jenny

Chanzo cha picha, BBC/Jenny Law

Alipoonyeshwa picha za Janessa, Ofa alisema hakuwa amezitumia yeye mwenyewe, lakini alielewa kwa nini zingekuwa kipenzi kati ya matapeli. Pia alisema ili kashfa ifanye kazi, angehitaji picha mbalimbali zinazoonyesha wanawake hao katika hali za kila siku - kama vile kupika au kwenye ukumbi wa mazoezi.

Vanessa anafikiri kwamba picha zake zimetumika kwa kiasi fulani kwa sababu alishiriki matukio mengi ya wazi kutoka kwa maisha yake ya kila siku. "Nilijianika nje kabisa, kwa hivyo walikuwa na mengi ya kufanya nao kazi," anasema.

Hatimaye wimbi lisilozuilika la wahasiriwa wa kashfa lilikua "jitu kubwa" ambalo lilimtia kiwewe Vanessa.

Kulazimika kuigiza kila siku kwenye kamera kulianza kuathiri afya yake ya akili na ndoa yake. Akiwa amechoka, Vanessa alituambia alianza kunywa pombe kabla ya maonyesho yake. Anasema anachukia kutazama video kutoka wakati huo kwa sababu anaweza kuona kutokuwa na furaha kwake.

Kufikia 2016, anasema hakuweza kuvumilia tena na akaamua kuacha. Anasema alipakia gari lake, akaacha nyumba yake na mume wake, na kuelekea kwenye maisha mapya. Sasa anafanya mazoezi ya tiba, na kuandika kumbukumbu - akichukua udhibiti wa hadithi yake mwenyewe.

Vanessa hajawahi kwenda kwa mamlaka kuripoti matapeli wanaotumia sura yake. Hafikirii wangechukulia malalamiko yake kwa uzito. "Wataniangalia kama, 'Wewe ni nyota ya ponografia' na kunicheka ," anasema.

Kwa miaka mingi tangu wakati huo, amekuwa mstahimilivu zaidi. Anajua walaghai huenda wasiache kujifanya kuwa yeye, lakini anaelewa ni kwa nini waathiriwa wengine hunaswa katika mtego huo.