Kurudi kwa wanafamilia wa Putin katika macho ya umma

    • Author, Elizaveta Fokht
    • Nafasi, BBC Russian
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwanasarakasi wa zamani katika Michezo ya Olimpiki Alina Kabaeva, hujulikana katika vyombo vya habari huru vya Urusi kama mshirika wa Rais Putin, na hilo limemfanya kuwekewa vikwazo na nchi za Magharibi.

Katika miezi ya hivi karibuni, Kabaeva amerejea katika maisha ya umma, na ameanzisha chuo chake cha sarakasi cha 'Sky Grace.'

Ana uhusiano na Putin?

Katika Michezo ya BRICS ya mwaka jana huko Kazan, hafla ya kila mwaka ya michezo inayoandaliwa na nchi za BRICS. Wana sarakasi kutoka Urusi, Belarus, Kazakhstan, Thailand, Serbia, na kwingineko, walishindana na wanasarakasi wa 'Sky Grace.'

Klabu hiyo ilianzishwa miaka miwili iliyopita na Alina Kabaeva. Ni wanasarakasi mashuhuri nchini Urusi, aliyepata mafanikio katika Olimpiki na mataji mengi ulimwenguni katika sarakasi.

Lakini umaarufu wake sio wa michezo tu, pi ni kutokana na madai ya uhusiano wake na Vladimir Putin – akitajwa kuwa ndiye mama wa watoto wawili wadogo wa Putin.

'Uhusiano huo wa karibu' ulitajwa kama chanzo cha yeye kuwekewa vikwazo na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya mwaka 2022. Putin mwenyewe hajawahi kukiri kuwa na uhusiano na mwanamke huyo.

Hata ripoti ya mwaka 2015 kuwa Kabaeva amezaa na Putin ilikanushwa vikali.

Maisha ya Putin ni ya siri

Maisha binafsi ya Putin ni ya siri sana. Kuna mabinti wawili wanaodhaniwa kuwa ni watoto wake, Maria Vorontsova na Katerina Tikhonova.

Putin na mabinti hao hawajawahi kuthibitisha kuwa na uhusiano wa kifamilia. Na wao pia wako chini ya vikwazo.

Kabaeva alihudumu kwa miaka saba kama mjumbe wa bunge la Urusi, na naadae akaongoza bodi ya wakurugenzi ya National Media Group, inayomilikiwa na mshirika wa karibu wa Putin, Yuri Kovalchuk.

Licha ya kushika nyadhifa hizo, aliepuka kuonekana hadharani na kutojihusisha na vyombo vya habari. Magazeti ya Glossy yalimtaja kama mtu asiyeweza 'kufikiwa' kupata habari.

Lakini mambo yalibadilika ghafla katika msimu wa vuli wa 2022, baada ya vita vikubwa nchini Ukraine kupamba moto. Kabaeva alitangaza kuunda 'Sky Grace,' chama cha kimataifa cha vilabu vya sarakasi.

Muda mfupi baadaye, akademia ya Sky Grace ilifunguliwa. Machi 2023, akademia hiyo mpya iliripotiwa kupewa zawadi ya jengo lenye thamani ya zaidi ya rubles bilioni mbili ($20.4m) na shirika linalohusika na gesi asilia la Gazprom.

Klabu mpya ya Kabaeva pia ina hadhi ambayo shirika jingine lolote la michezo nchini Urusi halina. Inaweza kuchagua na kuidhinisha kalenda ya michezo, kuchagua sheria inapoandaa michezo - kando na zile zilizoanzishwa kwa muda mrefu nyumbani na nje ya nchi.

Zaidi ya hayo, wanasarakasi wa Kabaeva walisafiri kushiriki michezo iliofanyika Ulaya mwaka jana. Ingawa walishindana bila kuwa na utaifa. Na hakuna klabu nyingine ya sarakasi kutoka vilabu vingine vya Urusi iliyopewa fursa hiyo.

Kwenye mitandao

Sky Grace iko hai kwenye mitandao ya kijamii. Akaunti ya Telegram ya akademia hiyo inaweka video kadhaa za wanafunzi wanaofanya mazoezi wakifunzwa na Kabaeva.

"Hakuna picha au video ya Alina Kabaeva inayowekwa mtandaoni bila yeye kujua na kutoa idhini. Haiwezekani mtu kurekodi kwa siri na kisha kuichapisha," ananambia mwandishi wa habari. "Alina anaidhinisha kila kitu, kuanzia pembe ya kamera inapotakiwa ikae, mwangaza, hadi marekebisho ya video."

Uamuzi wa ghafla wa kuanza kuonekana unakuja wakati akiwa na vikwazo baada ya vita nchini Ukraine vilivyoanzishwa na Urusi.

Na wale wanaodhaniwa kuwa mabinti wa Putin, Maria Vorontsova na Katerina Tikhonova, wameanza kuonekana mbele ya umma, walijitokeza kwenye Kongamano la Uwekezaji la St Petersburg mwaka jana. Tukio hilo limepoteza mvuto wake kwa wageni tangu vita kuanza, lakini bado ni hafla inayoonyesha nguvu za Vladimir Putin na kivutio kwa wale ambao watanufaika.

Kwa kuzingatia kazi ya vyombo huru vya habari kufichua utambulisho wa watu hawa, na ukweli kwamba tayari wameekewa vikwazo, inamaanisha hakuna tena na sababu ya msingi ya kuficha utambulisho wao.

Moja ya athari za vita vya Ukraine ni kuwafichua watu wa karibu wa Putin. Usiri hauna tena maana. Kabaeva, pamoja na jamaa wengine wanaodhaniwa kuwa wa karibu na Putin, huenda wana mipango yao wenyewe binafsi. Ukaribu wao na rais wa Urusi pengine utavutia watu wengine wenye mipango kama ya kwao.

Kabaeva amewekeza katika maendeleo ya akademia yake.

Kabaeva amewekeza katika maendeleo ya akademia yake. Sky Grace sasa inapigiwa upatu kama chama cha kimataifa. Mashindano makubwa yaliyofanyika Qatar mwishoni mwa Novemba, Alina Kabaeva mwenyewe alikuwa sehemu ya waandaaji.

Mashindano hayo yalitangazwa sana katika vyombo vya habari vya Urusi. Kituo kikuu cha michezo cha nchi hiyo kilituma mmoja wa wachambuzi wake wakuu wa michezo.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi