'Maiti zimetapakaa kila mahali' - wanakijiji wanaomboleza vifo vya watoto waliodondoshewa makombora

xx

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma / BBC

    • Author, Azeezat Olaoluwa
    • Nafasi, BBC News, Tudunbiri
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Maalim wa madrassa ,Masud Abdulrasheed, anatafuta faraja ili kukabiliana na kifo cha binti yake mwenye umri wa miaka saba ,Habeebah, aliyeuawa kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na wanajeshi wa Nigeria wakati wa sherehe za kidini katika kijiji chao kikubwa ambacho hakina watu wengi mwaka mmoja uliopita.

Jeshi hilo lilisema kuwa mashambulizi haya yalitokea kutokana na''kutokuelewana kwa taarifa,'' ambapo jeshi hilo lilifikiria sherehe hiyo ya wazi ya Tudunbiri ni mkusanyiko wa wapiganaji wa jihad.

''Shambulio la tarehe tatu Disemba mwaka 2023, lilikuwa janga kubwa ambalo halikupaswa kutokea,'' alisema msemaji wa jeshi, meja jenerali Edwars Buba alipoongea na BBC.

''Jeshi linajuta kwa tukio hilo. Na kama tungeweza kurudisha maisha ya walioangamia, tungelifanya hivyo ''

Tahadhari: Taarifa hii ina maelezo ya picha ambayo baadhi ya wasomaji watayapata ni ya kuhuzunisha.

Takriban watu 85 walipoteza maisha, ikiwa ni pamoja na binti ya Abdulrasheed, Habeebah, baada ya ndege zisizo na rubani kutupa mabomu mawili kwenye kijiji kilichopo kaskazini mwa jimbo la Kaduna.

“Bomu la kwanza lilidondoshwa majira ya saa nne usiku, karibu na mti ambapo wanawake na watoto walikuwa wamekaa,” alikumbuka Abdulrasheed. “Tulikimbia kutafuta usalama, lakini baada ya muda mfupi, tulikusanyika ili kuwasaidia wahanga na pia kutoa msaada, lakini bomu la pili lilitulipukia na kuua watu wengi zaidi.”

Abdulrasheed anamkumbuka mwanawe Habeebah kama “mwenye upendo zaidi kati ya watoto wangu.” “Alikuwa akinipatia zawadi zote alizozipokea, hata kama sikuzihitaji,” aliiambia BBC.

Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 36 alikuwa mmoja wa waandalizi wa sherehe za kila mwaka, zinazojulikana kama Maulidi, ambazo hufanyika kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad {S.A.W}

Wengi wa wanafunzi wake walikufa katika janga hilo.

“Tuliona maiti kila mahali kama vile walikuwa wamelala. Viungo vya miili vilikuwa vimetawanyika kwenye matawi ya miti na paa za nyumba. Ilibidi tuiweke kwenye magunia na kuzika maiti wote kwenye kaburi la pamoja.”

“Hakuna kitu kinachoumiza zaidi kuliko kuona watu uliowaalika kwa sherehe wakikufa mbele yako. Nimevunjika moyo kabisa,” alisema Abdulrasheed.

Wakati baba huyo wa watoto wanne alipokuwa akizungumza na BBC, alikaa akiwa na binti yake wa pili, Zaharau, aliyekuwa pembeni mwake kwenye mkeka nje ya nyumba yao. Aliinua shati la Zaharau na kutuonyesha jeraha lililokuwa tumboni mwake.

Masud Abdulrasheed anasema hospitali zimesitisha kumpa bintiye huduma za matibabu bila malipo

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma / BBC

Maelezo ya picha, Masud Abdulrasheed anasema hospitali zimesitisha kumpa bintiye huduma za matibabu bila malipo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zaharau ambaye wakati huo alikuwa na miaka 4 aligongwa na kitu chenye ncha kali.

Na ilichukua familia yake muda wa saa nzima kuwakimbiza hospitalini manusura katika mji jirani wa Kaduna.

Ingawa alifanyiwa upasuaji Zaharau bado kidonda chake hakijapona .

"Binti yangu pamoja na wengine waliopata majeraha walipelekwa hospitalini ,walihudumiwa na tushukuru serikali kwa hilo.

"Lakini mambo yalibadilika baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya matibabu ya dharura miezi kadhaa baadaye. Hospitali zimekataa kutuendelezea matibabu bila malipo .Wanatuhadaa kwa mengi."

Ukitembelea kila familia katika kijiji cha Tudunbiri, kila familia imesalia na makovu ya siku hiyo ikiwa na manusura .

Tunakutana na Aisha Buhari ,mwenye umri wa miaka 20 alipoteza kaka zake watatu usiku huo.

Alinusurika kifo lakini anauguza jeraha la mkono wa kushoto ambalo kufikia sasa halijapona.

Akiwa amekalia kiti ,alibubujikwa na machozi na kuyafuta na mtandio aliouvaa akivuta kumbukumbu dakika za mwisho za kaka zake watatu.

"Usiku huo ,nilikuwa nimemaliza kuongea na wao na nikaondoka kidogo baada ya mlipuko wa kwanza ,sekunde moja badaye nikaona miili yao imetapakaa ,''Buhari anaeleza

"Waliponikimbiza hospitalini sikufikiria chochote bali ni kaka zangu niliowaona wakiwa wamekufa.nililia sana."

Akiendelea kutusimulia kisa hicho cha kusikitisha alisita kidogo kupangusa usaha uliokuwa ukitirirka kutoka kwa kidonda.

"Kulikuwa hakuna majukumu ya nyumba au shambani ambayo singefanya kabla ya janga hilo .Lakini sasa nategemea watu wanisaidie kwa hali kama vile kunifulia nguo,''anasema

Aisha Buhari alipoteza kaka zake watatu katika shambulizi hilo la bomu

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma / BBC

Maelezo ya picha, Aisha Buhari alipoteza kaka zake watatu katika shambulizi hilo la bomu

Gavana wa jimbo la Kaduna, Uba Sani, aliiambia BBC kwamba atachukua hatua kutatua shida ya wakazi wa kijiji hiki kama Bi Buhari.

“Asanteni BBC kwa taarifa hii. Nitakwenda mwenyewe Tudunbiri, na ikiwa nitakutana na watu wanaohitaji matibabu, nitahakikisha wanapata huduma,” aliahidi. “Amri niliyotoa ni kwamba wote walioumia wanapaswa kutibiwa, na hakuna mtu atakayekubalika kuondolewa hospitalini hadi apone kikamilifu,” aliongeza.

Mkasa huo wa kushtua haujawatia uoga mwaka huu wamesherehekea sherehe hizo za maulidi lakini walifanya miezi miwili mapema.

Sherehe hiyo pia kulizinduliwa msikiti mpya uliojengwa na mamlaka katika eneo bomu hilo lililipukia kama njia moja ya kuwafidia.

Kwa sasa Abdulrasheed anafanya kazi kama imamu wa msikiti huo, baada ya imamu wa awali kuuawa katika mashambulizi hayo ya makombora.

“Tunafurahi kujengewa msikiti mpya, lakini hatuwezi kamwe kusahau kilichotokea,” alisema Abdulrasheed kwa BBC.

“Kila ninapokuja hapa, kila mara nakumbuka siku ile, na nahisi huzuni. Tunapoadhimisha Maulidi ya mwaka huu, pia tunakumbuka wale walioangamia.”

Kwa miaka mingi, jeshi la Nigeria limekuwa likipigana na wapiganaji wa jihadi na wahalifu, ambao hufanya mashambulizi katika vijiji na kuteka nyara watu kwa ajili ya fidia katika maeneo ya kaskazini.

Hali hii imesababisha ongezeko la mashambulizi ya anga yaliyolenga kundi hilo.

Jeshi la Anga la Nigeria limepata “idadi kubwa” ya ndege mpya, aliiambia BBC mkuu wa ulinzi wa Web,Guy Martin.

Hii ni pamoja na ndege zisizo na rubani zilizoundwa na China, ambazo kawaida huitwa drones.

"Ndege zisizo na rubani kutoka China ni za bei nafuu , jambo linalozifanya zipatikane kwa urahisi zaidi. Karibu theluthi moja ya nchi za Afrika zimepata ndege zisizo na rubani , nyingi kutoka Uturuki na China,” alisema Martin, akiongeza kwamba mashambulizi yaliyosababisha janga la Tudunbiri yalifanywa na ndege zisizo na rubani.

“Kukosekana kwa taarifa sahihi, kutokuwa na mpangilio, na mafunzo finyu kwa waendeshaji ndege zisizo na rubani ni baadhi ya sababu za mashambulizi ya kimakosa.

Kuletwa haraka kwa teknolojia ya ndege zisizo na rubani mara nyingi kunazidi maendeleo ya mafunzo na taratibu za ushiriki kwa wanajeshi,” aliongeza Martin.

Meja-Jenerali Buba aliiambia BBC kwamba jeshi limejipata likifanya kazi katika mazingira ya “changamoto na ugumu.” “Lakini tumejijenga katika umiliki wa vifaa na katika upelekwaji wa makamanda na wanajeshi wazoefu,” alisema.

Kwa mujibu wa kampuni ya ushauri ya SBM Intelligence, Jeshi la Anga la Nigeria lilifanya mashambulizi ya angani 17 yasiyokusudiwa kati ya Januari 2017 na Septemba 2024, yakisababisha vifo vya zaidi ya watu 500.

Masud Abdulrasheed anahudumu kama imamu wa msikiti mpya uliojengwa baada ya awali kulipuliwa

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma / BBC

"Kosa moja ni funzo tosha; lakini tukiona mamia ya watu wanauawa katika mashambulizi makubwa,tunapaswa kuwa na wasiwasi,''mtafiti wa Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch (HRW) nchini Nigeria Anietie Ewang anasema.

Akijibu wasiwasi ulioibuliwa na shirika hilo Meja jenerali Buba anasema ''mashirika ya haki yanapaswa kutuhongera kwa kuwa tuko wazi na tunashirikiana na watu na tunawajibikia makosa yetu kama vile ilivyofanyika katika mkasa wa Tudunbiri ,''

"tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha shambulizi kama hilo halitatokea siku za usoni," Maj-Gen Buba anasema.

Aliweka wazi kuwa maafisa wawili wa jeshi walifikishwa katika mahakama ya kijeshi kutokana na shambulizi hilo huku uchunguzi ukiendelea waliachishwa kazi na kuenguliwa madaraka yao.

Serikali kuu na za majimbo zimeanzisha miradi ya maendeleo kama njia moja ya kuwafidia wanakijiji waliopoteza wapendwa wao ,Sani akiiambia BBC kwamba ujenzi wa hospitali na kituo chakujifunzia ujuzi zinakaribia kumalizika kujengwa.

"Tumekuwa tukiwasaidia wakaazi wa Tudunbiri,natutaendelea naushirikiano huo ,''anasema.

"Ni watu wangu wa karibu ," Gavana anaongezea.

Lakini cha kutamausha na kinaya zaidi ni kuwa zaidi ya wanakijiji 20 wameripoti kuwa mashamba yao yamenyakuliwa ili kutumika kujenga miradi hiyo ya maendeleo.

Ikiwemo Hashim Abdullahi mwenye umri wa miaka hamsini ambaye aliongea na BBC :''sina raha kwani hospitali hii imechukua kitega uchumi changu na sikufidiwa chochote.Sina kazi wala bazi na familia yangu inanitegemea nashindwa kuimudu.''

Akijibu lalama hizo Sani anasema:''Kwa watu ambao wanamiliki mashamba kihalali,idara ya Kaduna inafanya kazi na viongozi wa jamii kuhakikisha watu walioathirika wamefidiwa bila ubaguzi. ''

Makamu wa rais nchini Nigeria Kashim Shettima alizuru kijiji hicho baada ya mauaji ya halaiki ,akiwaahidi akishirikiana na serikali kuu haki na fidia kwa familia zilizoathirika.

Watu waliambiwa watapatiwa milioni 2.5 za Nigeria kwa kila mmoja aliyeuawa katika familia,na wale waliojeruhiwa wakiahidiwa naira 750,000.

"Ni tofauti kwamba mamalaka zimefanya fidia,lakini kuna hisia kwamba imekuwa ya kiholela,''alisema Bi Ewang.

''Tunahitaji kuona mamlaka zikichukua hatua muhimu kupata haki ,kuwajibishwa kwa idara husika na fidia kwa wahanga wa mashambulizi ya anga yote ambapo wamekubali kuwa ilikuwa ni makosa,''aliongeza.

Bi Buhari aliiambia BBC kwamba familia yake ilipokea milioni 7.5 za naira kwa ajili ya kaka zake watatu waliouawa, na alipokea 750,000 za naira kwa majeraha yake - ingawa hii haikuwa ya kutosha.

Aisha Buhari anateseka kutumia mkono wake wa kushoto baada ya kujeruhiwa katika shambulizi la bomu

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma / BBC

Maelezo ya picha, Aisha Buhari anateseka kutumia mkono wake wa kushoto baada ya kujeruhiwa katika shambulizi la bomu

“Mara nyingi hununua dawa katika duka la dawa kutibu jeraha kwa sababu hicho pekee ndicho ninachoweza kumudu sasa. Hospitali haitutunzi tena. Wakati mwingine maumivu huwa makali sana kwa wiki,” alisema.

“Tunatumai serikali itatusaidia tena ili nipate matibabu bora kwa mkono wangu. Nina hamu ya kurejelea kazi zangu za mikoni,” aliongeza Bi Buhari.

Bwana Abdulrasheed aliiambia BBC kuwa hajapokea fidia ya kifedha kwa majeraha aliyoyapata binti yake wa miaka minne.

“kila Mara ninahisi wasiwasi ninapoitazama hali yake,” alisema.

Alisema amepokea fidia kamili kwa kifo cha binti yake wa miaka saba, lakini hakuna kiasi chochote cha fedha kinachoweza kumrudisha bintiye.

“Kila wakati ninapozuru kaburi lao, nakumbuka wale tulioishi nao lakini sasa hawapo tena. Nawakosa wote. Namkosa binti yangu.”

Maelezo ya ziada na Yusuf Akinpelu .

Mada zinazofanana

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla