Kwanini imani kwa viongozi wanawake inapungua?

Chanzo cha picha, Getty Images
Imani kwa viongozi wanawake inashuka huku idadi yao katika nyadhifa za uongozi ikiongezeka. Je ni kwanini?
Wanawake zaidi sasa wanaongoza kampuni kubwa zaidi duniani kuliko ilivyowahi kutokea katika nyakati zilizopita, lakini utafiti unaonyesha kuwa kuongezeka kwa uwakilishi wao kumekuwa kukiambatana na kushuka kwa Imani kwa viongozi wa kike.
Hii inaonyesha picha mbaya kwa wale walioweza kupenya na kuingia katika uongozi.
Mwezi Novemba, data mpya kutoka katika Reykjavik Index, utafiti wa mwaka ambao unalinganisha jinsi wanaume na wanawake wanavyotazamwa inapokuja katika suala la kufaa kwao katika nafasi za mamlaka, ulionyesha kuwa imani kwa viongozi wanawake imeshuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi chote cha mwaka.
Katika nchi zote wanachama wa G7 ( nchi zilizostawi zaidi kiviwanda) – mkiwemo Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani, chache kuliko chini ya nusu (47%) walisema kuwa “‘wanahisi vyema sana ” kuwa na mwanamke kama Mkurugenzi mkuu wa kampuni kubwa katika nchi zao, kiwango hiki kikiwa ni chini ya 54% yam waka uliotangulia.
Ingawa watu wengi hawajakata tamaa, wasomi na wataalamu wa uongozi na jinsia kwa ujumla hawashangazwi na matokeo ya utafiti, na wana nadharia tofauti kuhusu ni kwanini imani kwa viongozi wanawake inafifia.
Wote wanaonya hatahivyo kwamba kuziba pengo ni muhimu ili kumaliza upendeleo unaoruhusiwa katika kila viwango vya makampuni na taasisi.
Hali halisi ya utamaduni

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya wataalmu wanadai kwamba unyanyasaji wa wanawake katika taasisi na ubaguzi wa kijinsia vimekuwa vikichochewa na hali ya kisiasa na janga la corona kwa pamoja.
Danna Greenberg, profesa wa masuala ya tabia na mienendo ya mashirika katika taasisi ya Babson College iliyopo Massachusetts, Marekani, anaamini kuwa wanawake waliacha kazi ya malipo na kuchukua jukumu la kulea watoto na kazi nyingine za nyumbani kutokana na Covid-19 na hivyo kusababisha “ugumu katika shana za kitamaduni” kuhusu nafasi ya mwanamke katika kazi na katika nyumba.
Katika nchi fulani, baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa , kunaweza kuwa na sababu za kisiasa zinazosababisha kuwepo kwa mitizamo fulani kuhusu mabadiliko ya uongozi wa kike.
“Iwapo utakuwa na mazungumzo ya kitaifa kuhusu iwapo wanawake wanapaswa hata kuruhusiwa kuchukua udhibiti wa afya yao wenyewe, sasa unatarajia nini?” anasema Michelle Harrison, Mkurugenzi mkuu wa duniani wa Kantar Public, akitoa mfano wa uamuazi wa Mahakama ya juu zaidi ya Marekani wa mwezi Juni kuhusu kubatilishwa kwa hukumu ya kesi ya Roev Wade.
Kwa maneno mengine, kama kitu cha siri kama vile haki ya mwanamke ya uzazi kinahojiwa hadharani, hiyo inaonyesha kuwa haki yake ya kufanya chochote maishani inafaa kuwa mjadala wa watu wote.
Kama kiongozi mwenye mamlaka anafanya mambo kwa njia hiyo, hilo pia linaweza kuchukuliwa kama uidhinishwaji wa tabia fulani, anasema Greenberg.
Ukosefu wa maudhui ya wanawake mtandaoni na uhamasishaji dhidi ya wanawake umepelekea kuwepo kwa ubaguzi wa jinsia katika maisha ya kila siku, anasema Laura Bates, mwandishi Muingereza, mwanaharakati na mtafiti, aliandika katika kitabu chake cha 2020 alichokiita Men who Hate Women (Wanaume wanaowachukia wanawake).
Sehemu ya utamaduni
Nadharia nyingine juu ya kushuka kwa imani kwa viongozi wanawake ni kwamba mitizamo hasi kwa wanawake viongozi imekuwa ikiongezeka kwasababu tu wanawake zaidi wamekuwa wakichukua nafasi za juu za mamlaka, jambo ambalo limebadilisha hali halisi ya utamaduni.
“Kihistonia, eneo la kazi na serikali zimekuwa zikitawaliwa na wanaume, na tamaduni imekuwa ikibuniwa na wanaume.
Hii ina maana kwamba kitu chochote tofauti na kawaida hakitaaminiwa,” anasema Allyson Zimmermann, mkurugenzi mkuu wa Ulaya, Masharika ya Kati na Afrika katika Catalyst, shirika la kimataifa linalofanya kazi na wakurugenzi wakuu na viongozi wa makampuni kujenga mahala pa kazi panapowafaa wanawake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Julie Castro Abrams, Mkurugenzi mkuu na mweneyekiti wa How Women Lead, Mtandao wa Marekani wa wanawake zaidi ya 13,000 wanaojitolea kuongeza idadi ya sauti mbali mbali za wanawake na viongozi, anaamini jambo lingine ni jinsi jamii inavyowakubali viongozi wanawake .
“Tunapenda kuwatendea maovu wanawake. Ni sehemu ya utamaduni wetu,” anasema “wakati tunapowapata wanawake zaidi katika uongozi , tabia hiyo inaanza kujitokeza, kwasababu uongozi wa wanawake unakwenda kinyume na mtazamo ambao sote tulijifunza.
Na watu hupenda kuwaona wanawake wakishindwa kwasababu mwanamke anayefanikiwa haendani na mitizamo ambayo sote tumekuwa tukifunzwa.”
Utafiti pia umeonyesha kuwa wanawake wana uwezekano mkubwa kuteuliwa kuchukua nyadhifa za juu wakati nchi au kampuni inapokuwa mashakani au inapokuwa katika hatari ya kuporomoka.
Labda mfano mzuri zaidi ni pale Waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss alipohudumu kwa muda mfupi kama Waziri mkuu wa Uingereza – alipoteuliwa wakati uchumi wa nchi ulipokuwa katika hali ya kuyumba na taifa likikabiliwa na msukosuko wa kisiasa.
Sababu chache za kuwa matumaini
Katika tamaduni nyingi na maeneo ya kazi, ubaguzi wa jinsia umeshamiri na kwa hiyo ni mbaya, ikimaanisha kuwa suluhu ya haraka ya kuumaliza haitawahi kuwepo.
Ikizingatiwa kongezeka kwa taratibu lakini kunako imarika kwa uwakilishaji wa wanawake katika vyeo vya juu vya makampuni, imani kwa viongozi wanawake litaendelea kuwa tatizo, lakini bila shaka idadi ya wanawake viongozi itaendelea kuongezeka.
Mageuzi ya mazingira ya kisiasa, uchumi na jamii, wanasema wataalamu, huenda vikaamua kiwango cha imami kwa wanawake viongozi katika miaka ijayo, wanasema wataalamu.
Kitu muhimu cha kukumbuka, anasema Harrison, ni kwamba hili halihusiani na nafasi ya watu binafsi wa jinsia fulani.
“Hii sio kuhusu kuwasaidia wanawake na sio kuhusu kuwasaidia wanaume ,” anasema “ bali ni kuhusu kubadilisha tamaduni ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi ndani ya jamii zetu. Na sasa hivi, tamaduni hizo hizo bado zipo .”













