Je, Wamisri walitumia 'lifti' kujenga piramidi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Piramidi za Misri zilijengwa maelfu ya miaka iliyopita, lakini jinsi yalivyojengwa imewashangaza wanasayansi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, wataalamu sasa wanafikiri huenda wamegundua siri ya jinsi piramidi hizo zilivyojengwa.
Utafiti mpya unanadharia kwamba Wamisri wa kale walitumia "lifti ya maji" ndani ya piramidi.
Kama vile vitu vilivyoyeyushwa hulipuka kutoka kwenye moyo wa dunia wakati wa volkano, kwa njia hii, mawe makubwa yanaweza kubebwa kupitia chumba.
Wataalamu wamegundua nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Piramidi ya Djoser inajulikana kama piramidi kongwe zaidi nchini Misri. Piramidi hii ilijengwa zaidi ya miaka 4500 iliyopita.
Piramidi hii, ambayo iko kusini mwa Cairo, mji mkuu wa Misri, inafikia urefu wa kuvutia wa mita 62.5 katika ngazi sita.
Sasa timu ya watafiti wa Ufaransa wanaamini kuwa wanaweza kuwa wamegundua jinsi piramidi hii kubwa ilivyojengwa.
Wataalamu wamechunguza mazingira yanayozunguka piramidi, pamoja na vichuguu na mambo ya ndani, na kusema wamepata ushahidi kwamba Wamisri wa kale wanaweza kuwa walitumia mfumo wa maji.
Kwa mujibu wa nadharia iliyopendekezwa na kikundi hiki, muundo wa mawe unaoitwa "Jasr al-Madir" uliundwa kukusanya maji kutoka maeneo ya jirani na kuhamisha ndani ya piramidi.
Baada ya maji kuingia, mfumo wa kuelea ulitumiwa kuinua kiwango cha maji, ili kuhamisha mawe mazito kutoka ndani ya piramidi hadi pale yalipohitajika.
Wamisri wa kale wanajulikana kuwa wataalamu wa ujenzi kwa ubunifu wao wa ujenzi, na wanafikiri kwamba hii inaweza kuwa imewasaidia kupata wazo hili la busara.
Kwa nini piramidi zilijengwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Piramidi za Misri ni moja ya maajabu ya ulimwengu.
Mapiramidi mengi yalijengwa kama makaburi; Mahali pa kuzikia maofisa wa kifalme wa Misri ambao, bila shaka, walichukua mali zao zote za kidunia pamoja nao.
Amri ya kujenga piramidi ilitolewa na wafalme wa jamii ya kale ya Misri, ambao waliitwa fharao.
Mafarao walipata wahandisi na wasanifu bora zaidi wa kusanifu na kujenga majengo.
Maarufu zaidi kati yao ni Piramidi Kuu ya Giza, ambayo ina urefu wa mita 147 na imetengenezwa kwa vitalu vikubwa milioni mbili na 300,000.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












