'Ni nani aliyekupa idhini ya kumuajiri mke wangu?'

Wanawake wanaofanya kazi wanakabiliwa na vikwazo vikali

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake wanaofanya kazi wanakabiliwa na vikwazo vikali
Muda wa kusoma: Dakika 5

"Katika mahojiano ya kazi, nilitakiwa kuwasilisha idhini ya maandishi kutoka kwa mume wangu ili kuthibitisha kuwa nina idhini yake kufanya kazi," anasema Neda, ambaye ana shahada ya uzamili ya uhandisi wa katika sekta ya mafuta na gesi kutoka Iran.

Mwanamke huyo anaeleza kwamba alihisi kufedheheshwa.

"Niliwaambia kuwa mimi ni mtu mzima na ninafanya maamuzi yangu mwenyewe."

Hii ni hali ambayo huwakabili wanawake wa Iran kila siku.

Ripoti ya 2024 ya Benki ya Dunia inaorodhesha Iran miongoni mwa nchi zilizo na sheria kali dhidi ya wanawake wanaotafuta ajira.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Jukwaa la Global Gender Gap 2024, Iran ina kiwango cha chini zaidi cha ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake kati ya nchi 146 zilizofanyiwa utafiti.

Wakati wanawake ni zaidi ya 50% ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini humo, wanakadiria 12% pekee ya wafanyikazi, kulingana na data ya 2023.

Sheria za jinsia, pamoja na unyanyasaji wa kijinsia uliokithiri na mitazamo inayotilia shaka uwezo wa wanawake hufanya mazingira ya kazi kuwa magumu kwao.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na BBC katika makala hii walisema kuwa wanahisi kupuuzwa kazini.

"Vikwazo vingi vya kisheria na kitamaduni vinawaweka wanawake nje ya nguvu kazi nchini Iran," anasema Nadereh Chamlou, mshauri mkuu wa zamani wa Benki ya Dunia.

Chamlou anaongeza kuwa mambo kama vile kukosekana kwa mifumo ya kisheria na vikwazo vilivyopo vya kisheria, pamoja na pengo kubwa sana la malipo ya kijinsia, vinachangia ushiriki mdogo wa wanawake katika nguvu kazi nchini Iran.

Soma pia:

changamoto ya kisheria na kitamaduni

Wanaume wanajua kwamba wanaweza kuwazuia kisheria wake zao kufanya kazi na wengine kutumia fursa hii.

Mfanyabiashara wa Iran Saeed aliambia BBC kwamba "mume mwenye hasira aliwahi kuingia ofisini kwetu kuuliza kwa ukali: 'Ni nani aliyekupa ruhusa ya kumwajiri mke wangu?'

Anasema sasa anahakikisha anatafuta kibali cha maandishi kutoka kwa mume anapoajiri mwanamke.

Razieh, kijana mtaalamu anayefanya kazi katika kampuni ya kibinafsi, anakumbuka tukio kama hilo wakati mwanamume mwenye hasira alipoingia ofisini kwake na kumwambia Mkurugenzi Mtendaji: "Sitaki mke wangu afanye kazi hapa."

Mkurugenzi Mtendaji, Razieh anasema, ilibidi amwambie mwanamke huyo, ambaye alikuwa mhasibu, "kurudi nyumbani na kujaribu kuweka mambo sawa na mumewe, vinginevyo angelazimika kujiuzulu. Hatua ambayo hatimaye alilazimika kuchukua."

Baadhi ya makampuni hazitaki kuwaajiri wanawake vijana na kuwekeza katika mafunzo yao kwa sababu waume zao wanaweza kuwazuia kufanya kazi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya makampuni hazitaki kuwaajiri wanawake vijana na kuwekeza katika mafunzo yao kwa sababu waume zao wanaweza kuwazuia kufanya kazi.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na mshauri wa kimataifa Nadereh Chamlou, sheria hii pia inasababisha makampuni kuhofia kuwaajiri wasichana wadogo, kwani waajiri hawataki "kuwekeza katika mafunzo ya wanawake hawa ambao baadaye wanazuiliwa kufanya kazi na waume zao."

Na hata kama watapata kazi hiyo (bila kupigana kwanza na familia zao na wenzi wao), wanawake wanaingia kwenye soko la ajira ambalo ubaguzi wa ajira dhidi ya wanawake unaungwa mkono kisheria kwa kiwango fulani.

Sheria moja kama hiyo ni Kifungu cha 1105 cha Sheria ya Kiraia ya Jamhuri ya Kiislamu, ambapo mume anafafanuliwa kama kichwa cha familia na "mtegemezi mkuu."

Hii ina maana kwamba wanaume wanapewa kipaumbele katika ajira kuliko wanawake, ambao pia wanatarajiwa kufanya kazi kwa sehemu ndogo ya malipo ikilinganishwa na wenzao wa kiume ikiwa watapewa nafasi.

Raz yuko katika miaka yake ya 20 na amebadilisha kazi mara kadhaa. Anasema kuwa kila mahali ambapo amefanya kazi, kazi za wanawake ni za kwanza kutolewa kufungwa.

"Mahali pa mwisho nilifanya kazi, wakati kulikuwa na marekebisho, karibu watu wote walioachishwa kazi walikuwa wanawake," anaongeza.

Mwanamke mwingine, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, aliambia BBC kuwa aliamua kuacha kazi yake baada ya zaidi ya muongo mmoja na kubaki nyumbani "kwa sababu nilijua singepandishwa cheo kamwe".

"Mradi tu kuna wanaume wanaopatikana, hata kama walikuwa na sifa duni, singefikiriwa kamwe kuongezwa mishahara au kupandishwa cheo. Ilikuwa ni kupoteza muda," anasema.

Ukweli kwamba wanawake hawazingatiwi kisheria kuwa walezi huathiri haki yao ya kupata faida na bonasi.

Katika hali nyingi, kama watahitimu, "manufaa wanayopata kwa miaka yao ya ajira yanaweza yasitumike kwa familia zao, kama vile pensheni," Chamlou anasema.

"Kwa hiyo wanapunguza malipo ambayo wanawake wanapata kutokana na kazi zao na wanaweza kuchangia familia zao," anaongeza mshauri mkuu wa zamani wa Benki ya Dunia.

xx

Chanzo cha picha, Getty Images

Sepideh ana shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Tehran, ambapo alikuwa akifundisha na kuongoza miradi huru ya sanaa, lakini hajafanya kazi katika miaka ya hivi karibuni.

"Baada ya kuhitimu, nilifikiri ningeweza kujikimu kimaisha kama wanaume wengi niliowajua, lakini muundo wa kijamii, kisiasa na kiuchumi umeundwa kwa njia ambayo inafanya kazi inayofaa kuwa ndoto isiyoweza kufikiwa kwa wanawake," Sepideh anaambia BBC.

Sheria ya vazi la hijabu ilikuwa kitovu cha maandamano makubwa nchini Iran miaka miwili iliyopita na bado ni miongoni mwa masuala tata yanayozua na mifarakano ya kisiasa nchini humo.

Sheria pia inafanya idadi ya kazi, hasa serikalini na katika sekta ya umma, kutoweza kufikiwa na wanawake ambao hawataki kufuata sheria kali za mavazi.

Ripoti ya IMF ilionyesha kuwa ukuaji wa uchumi unahusiana na kuongezeka kwa ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake, na kukadiria kuwa ikiwa viwango vya ajira vya wanawake nchini Iran vitafikishwa katika kiwango sawa na ajira ya wanaume, pato la taifa la nchi hiyo (GDP) linaweza kuongezeka kwa takriban 40%.

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Kulingana na Nadereh Chamlou, kwa sasa hakuna "utashi wa kisiasa" kuwezesha mabadiliko ya kuiwajumuisha wanawake katika nguvu kazi.

Lakini anaamini kuwa wanawake nchini Iran wanachukua hatua mikononi mwao na kuunda biashara ndogo ndogo zinazojitegemea ili kujifungulia soko la ajira.

"Baadhi ya mawazo ya ubunifu zaidi ya biashara, kutoka kwa programu za kupikia hadi majukwaa ya rejareja ya dijiti, yameanzishwa na wanawake," anaelezea.

Anaona "sekta halisi ya kibinafsi nchini Iran" inayoundwa na makampuni mengi yanayomilikiwa na wanawake.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi