Je, Rais wa Gabon Ali Bongo yuko wapi?

Chanzo cha picha, AFP
Kundi la maafisa wakuu wa kijeshi wametangaza kwenye televisheni ya taifa nchini Gabon kwamba wametwaa mamlaka kwa sababu uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa juma haukuwa wa kuaminika.
Tangazo hilo lilikuja muda mfupi baada ya Tume ya uchaguzi kusema kuwa Rais Ali Bongo Ondimba ameshinda kwa muhula wa tatu katika uchaguzi wa Jumamosi ambao ulikuwa na utata.
Gabon sasa inaungana na Mali, Guinea Conakry, Burkina Faso na Niger ambazo zote ziko chini ya junta za kijeshi.
Jeshi limetangaza hali ya hatari katika mji mkuu Libreville, kufunga anga na kuisimamisha katiba.
Rais Ali Bongo Ondimba hajulikani aliko.
Tume ya uchaguzi ilisema Bw Bongo alishinda chini ya thuluthi mbili tu ya kura katika uchaguzi ambao upinzani ulidai kuwa ulikuwa wa udanganyifu.
Kupinduliwa kwake kutakomesha familia yake iliyodumu kwa miaka 53 madarakani nchini Gabon.
Wanajeshi 12 walionekana kwenye televisheni wakitangaza kuwa wanafuta matokeo ya uchaguzi na kuvunja "taasisi zote za jamhuri".
Mmoja wa wanajeshi hao alisema kwenye chaneli ya televisheni ya Gabon 24: "Tumeamua kulinda amani kwa kukomesha utawala uliopo." Hii, aliongeza, ilikuwa chini ya "utawala usiowajibika, usiotabirika na kusababisha kuzorota kwa uwiano wa kijamii ambao unahatarisha nchi katika machafuko".
Bw. Bongo aliingia mamlakani wakati baba yake, Omar Bongo alipofariki dunia mwaka 2009.
Mnamo 2018, alipatwa na kiharusi ambacho kilimweka nje kwa karibu mwaka mmoja na kusababisha wito wa kumtaka ajitoe. Mwaka uliofuata, jaribio la mapinduzi lililofeli lilishuhudia askari waasi wakipelekwa gerezani.
Ali Bongo ni nani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ali Bongo Ondimba alizaliwa Februari 9 mwaka 1959 mjini Brazzaville na alifahamika kama mwana wa Alain Bernard Bongo (ambaye baadaye alifahamika kama Omar Bongo Ondimba) na Josephin Kama (baadaye Patience Dabany).
Kumekuwa na mjadala ikiwa Ali Bongo ni mwana wa Omar Bongo ikizingatiwa kuwa mama yake alikuwa mja mzito miezi 18 kabla ya kuolewa madai ambayo Ali Bongo amekuwa akipinga. Aidha, wakati wa kuzaliwa kwake mamake alikuwa na miaka 15.
Baada ya kusomea uwanasheria Ali Bongo alijitosa katika siasa za Gabon ambapo alijiunga na chama PDG mwaka 1981 na muda mfupi baadae aliteuliwa katika kamati kuu ya chama mwezi Machi mwaka 1983.
Baadaye aliteuliwa kumwakilisha baba yake katika chama hicho nafasi ambayo ilimwezesha kujiunga na asasi kuu ya uongozi wa chama katika uamuzi ambao ulifikiwa katika kongamano maalum ya PDG mwaka 1986.
Ali Bongo ni mwana wa kiume wa rais Omar Bongo, ambaye aliongoza Gabon kiimla kutoka mwaka 1967 hadi alipofariki dunia mwaka 2009.
Wakati wa utawala wa baba yake Ali Bongo aliwahi kuhudumu kama waziri wa mambo ya nje wa wa Gabon kati ya mwaka 1989 na 1991.
Pia aliwahi kuhudumu kama naibu kiongozi wa bunge la kitaifa kuanzia mwaka 1991 hadi 1999.
Wakati wa uchaguzi wa uraisi wa mwaka 2005 alifanya kazi kama mshirikishi wa vijana katika kampaini ya baba yake.
Baada ya uchaguzi huo alipandishwa cheo na kuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Gabon kuanzia Januari 21 mwaka 2006 huku akiendelea kushikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi.












