Putin atafanya nini baada ya uasi wa Wagner? Baadhi ya maswali muhimu na majibu

Hatua za usalama za dharura bado zinaendelea kutekelezwa mjini Moscow, baada ya uasi wa mamluki wa Wagner ambao umetikisa nafasi ya rais wa Urusi.

Bado kuna maswali mengi ambayo yanahitaji kujibiwa ili kuelewa hali hiyo.

Putin atafanya nini tena?

Katika saa 24 zilizoshangaza, Vladimir Putin alikabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa mamlaka yake tangu aingie madarakani zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Ingawa hatari ambayo ingetokea mara moja inaonekana kuzuiliwa, wataalam wa Urusi wanasema Putin haonekani kuwa na nguvu, lakini amejeruhiwa vibaya.

Chuki ya Putin kutokana na usaliti ilionekana kujitokeza katika hotuba yake kali kwenye televisheni ya taifa Jumamosi asubuhi, ambapo alimshutumu kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin kwa "kutokuwa mwanaminifu" na uhaini.

Rais wa Urusi hajaonekana hadharani tangu wakati huo, na hakuna hotuba mpya ya rais iliyopangwa kwa siku za usoni. Katika mahojiano yaliyorekodiwa kwenye televisheni ya taifa siku ya Jumapili - ambayo yanaonekana kufanywa kabla ya uasi - Putin alisema ana imani na vita vinavyoendelea Ukraine.

Hatua za usalama za kupambana na ugaidi bado zinaendelea mjini Moscow, lakini haijabainika iwapo rais Putin yuko katika mji mkuu wa Urusi wakati huu.

Baadhi wanatarajia kwamba Putin ataonyesha hasira yake kwa namna fulani, ama kijeshi nchini Ukraine, au kwa wale ambao hawajaonyesha kutoa msaada ndani ya Urusi.

MEP wa Poland Radek Sikorski aliiambia BBC kwamba kiongozi wa Urusi "huenda akawaondoa wale anaowaona kuwa hawana maamuzi", kumaanisha kuwa utawala wake utakuwa "wa kimabavu zaidi na wakati huo huo wa ukatili zaidi".

Prigozhin atafanya nini huko Belarusi?

Mtu anayesemekana kutekeleza uasi, Yevgeny Prigozhin, sasa ni mtu huru. Licha ya jaribio la kupindua uongozi wa kijeshi wa Urusi, shtaka la uasi wa kutumia silaha dhidi yake lilitupiliwa mbali. Lakini hatujui maelezo yote ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Urusi na Wagner.

Na pia wachambuzi wa Kirusi hawatarajii Prigozhin kutoweka kimya tu hivyo.

Kiongozi huyo wa mamluki amekuwa mtu muhimu kwa makumi na maelfu ya wapiganaji wa Ukraine - lakini sio mwenye maamuzi ya moja kwa moja na pia amekuwa muhimu kwa Rais Putin, akifanya kazi nyuma ya pazia kwa muda mrefu.

Ametumia miaka akifanya kazi chafu kwa Kremlin, kuanzia mapigano nchini Syria hadi mapigano nchini Ukraine mwaka 2014, ilipoiteka Crimea.

Lakini baada ya kupinga mamlaka ya Putin - na wengine wakimchukulia kama mwenye kumtusi kiongozi wa Urusi - maswali yanaibuka mengi juu ya hakikisho alilopewa kwa usalama wake, na jukumu lake katika siku zijazo.

Watazamaji wanashangaa ni kiasi gani cha udhibiti wa kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko ataweka juu ya Prigozhin - ikiwa kweli ataenda Minsk - na ikiwa vikosi vya Wagner vitamfuata, vitaleta tishio gani kwa Urusi, Belarus na Ukraine.

Nini kinatokea kwa kundi la Wagner Group sasa?

Kabla ya uasi huu ulioshangaza wenye kuhusisha silaha, makumi ya maelfu ya mamluki wa Wagner walikuwa na jukumu kubwa katika vita vya Putin dhidi ya Ukraine. Lakini siku za Wagner kama jeshi huru tayari zilikuwa zikikaribia kufika mwisho.

Prigozhin na vikosi vyake wanapinga shinikizo la kuingizwa katika wizara ya ulinzi ya Urusi, na upinzani dhidi ya Wagner unaonekana kama sababu kuu ya kugeuza uhasama uliodumu kwa muda mrefu kuwa uasi.

Lakini kwa kumalizika kwa uasi wa muda mfupi - na Prigozhin sasa akionekana anaelekea uhamishoni - wengi wanajiuliza wapiganaji wake watafanya nini.

Mashtaka yanaonekana kufutwa dhidi ya waliohusika katika uasi huo. Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wanajeshi wa Wagner wakiondoka katika jiji la Rostov-on-Don, ambako walikuwa wamedhibiti kambi za kijeshi.

Gavana wa Voronezh, ambayo iko katikati ya Rostov na Moscow, alisema vikosi vya Wagner pia vinaondoka katika mkoa wake.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa sasa watashirikiana tu na kujumuika katika jeshi la kawaida la Urusi - au hata kama wanajeshi wa kawaida wa Urusi sasa watakuwa tayari kuhudumu pamoja nao kwa hiari.

Je, watarejea tu kwenye mapigano katika maeneo yenye migogoro ya Ukraine, kama vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vinavyopendekeza?

Baadhi ya wachambuzi wameibua wasiwasi kuwa huenda wapiganaji hao wakamfuata Prigozhin magharibi iwapo ataenda Belarus, eneo la karibu zaidi ambalo Urusi inaweza kushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kiev.

Hali ilivyo itaathiri vipi vita vya Ukraine?

Kundi la Wagner linajumuisha baadhi ya makomando mashuhuri wanaopigana nchini Ukraine, ingawa wapiganaji wake wengi wametolewa gerezani, wakishawishiwa na ahadi ya uhuru wa kuhudumu vitani.

Walihusika sana katika unyakuzi wa Warusi wa mji wa Bakhmut, kwa mfano.

Urusi inadai uasi huo haujaathiri kampeni yake nchini Ukraine hadi sasa.

Hata hivyo, hakuna shaka kwamba vikosi vya Urusi vimesikia kinachoendelea na habari hiyo inaweza kuwa ya kuhuzunisha.

Wengine wanapendekeza kwamba kunaweza kuwa na mapigano kati ya vitengo pinzani katika siku zijazo, kulingana na jinsi hali ilivyo nchini Urusi baada ya matukio ya Jumamosi.

Nchini Ukraine, pamoja na kuwa na wasiwasi juu ya hatari ya Urusi kuongeza uingiliaji wake, viongozi wa kijeshi watatafuta fursa kutokana na kukosekana kwa utulivu katika mpaka.

Vikosi vya Kiev vilianzisha mashambulizi ya kukabiliana na kutwaa tena ardhi iliyonyakuliwa na wavamizi na wanaamini kwamba machafuko nchini Urusi yanatoa fursa "muhimu" kwao.

Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Ukraine Bill Taylor aliiambia BBC kwamba vikosi vya Ukraine vilikuwa "vizuri" kutumia udhaifu wa kimbinu uliofichuliwa na harakati za ghafla za wapiganaji wa Wagner.

Marekani na wengine walijua nini mapema?

Huku uasi wa Prigozhin ukionekana kuishangaza Ikulu ya Urusi, mashirika ya kijasusi ya Marekani tayari yameona dalili za kwamba anapanga kuchukua hatua na yalikuwa yametoa taarifa kwa Rais Joe Biden pamoja na viongozi wakuu wa bunge mapema wiki hii, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti.

Ujasusi wa Marekani uligundua kuwa kiongozi wa kundi la mamluki alikuwa akikusanya silaha, risasi na vifaa vingine karibu na mpaka na Urusi, CNN iliripoti.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, Rais Biden amezungumza na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza juu ya wasiwasi kwamba udhibiti wa Putin wa silaha nyingi za nyuklia za Urusi unaweza kutumbukia katika machafuko.

Wakuu wa kijasusi wa Marekani walikuwa wakifuatilia uhusiano unaozidi kuzorota kati ya Prigozhin na maafisa wa ulinzi wa Urusi kwa miezi kadhaa na ujasusi ulihitimisha kuwa ni ishara kwamba vita vya Ukraine vinakwenda vibaya kwa Wagner na wanajeshi wa kawaida, gazeti hilo linasema.

Wakati huo huo, gazeti la Washington Post linasema kuwa Marekani inaweza kuwa ilijua Prigozhin anapanga kitu mapema katikati ya Juni.

Kichochezi kikuu kilikuwa amri ya Juni 10 ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi kuamuru vikundi vyote vya kujitolea - kama vile Kundi la Wagner - kutia saini mikataba na serikali, ambayo ingekuwa utekaji wa vikosi vya mamluki vya Prigozhin.

"Kulikuwa na ishara za kutosha kuweza kuuambia uongozi ... kwamba kuna jambo limetokea," maafisa waliambia gazeti hilo – uhalisia hasa wa mipango ya Prigozhin haikuwa wazi hadi muda mfupi kabla ya uasi kuanza.

Rais Putin pia aliambiwa na Ujasusi wake kwamba Prigozhin alikuwa akipanga kitu, gazeti hilo liliripoti. Lakini haikuwa wazi ni lini hasa aliambiwa hili, ila "hakika ilikuwa zaidi ya saa 24 zilizopita," gazeti hilo lilimnukuu afisa wa Marekani akisema Jumamosi.

Watu wa Urusi wanafikiria nini?

Hotuba ya Putin kwa taifa wakati mzozo huo ukiendelea inaonekana kama ishara ya jinsi anavyochukulia tishio hilo kwa uzito na hitaji la kutoa hakikisho kwa umma nchini Urusi.

"Wengi ndani ya wasomi watamlaumu Putin kwa kila kitu kilivyokwenda kufikia sasa na kwamba hakukuwa na majibu sahihi kutoka kwa rais kwa wakati," aliandika mchambuzi mashuhuri wa Urusi Tatyana Stanovaya kwenye Telegraph. Kwa hiyo, simulizi hii yote pia ni pigo kwa nafasi za Putin.

Ingawa ni vigumu kufikia hitimisho kuhusu maoni ya umma ya Kirusi kwa ujumla, viongozi wa nchi wangekuwa na wasiwasi kwa kuona watazamaji wa kiraia wakishangilia vitengo vya Wagner huko Rostov.

Majeshi ya Wagner yakiondoka katika jiji hilo yalikuwa yamedhibiti vilivyo wakati wa uasi wao, yalilakiwa na umati ulioonekana kuwaunga mkono ambao ulishangilia, kupiga makofi na kupiga picha.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba baadhi ya wakazi walikimbia kuondoka jijini kwa treni siku ya Jumamosi baada ya Wagner kuwasili.