Utata kuhusu vyombo vinne vya anga vilivyodunguliwa na Jeshi la Marekani mwezi huu

Jeshi la Marekani halina uhakika kuhusu vitu vitatu vilivyokuwa vinaelea katika anga la Amerika Kaskazini vilikuwa vitu gani - na kwa namna gani viwezea kuwa kwneye anga hilo.

Rais Joe Biden aliamuru kitu kingine - ambac ho ni cha nne kwa jumla mwezi huu - kuangushwa siku ya Jumapili.

Inaelezwa kitu hicho kisichofahamika mpaka sasa kilikuwa kikisafiri kwa futi 20,000 (6,100m), na kingeweza kuingilia kati usafiri wa anga (ndege za kibiashara), Marekani ilisema.

Kamanda wa kijeshi alisema kitu hicho kinaweza kuwa kama "aina ya puto" au "aina fulani ya mfumo unaofahamika kama propulsion".

Aliongeza kuwa hawezi kukataa kuwa vitu hivyo ni vya nje ya nchi.

Kitu cha hivi karibuni zaidi - kilichotunguliwa juu ya Ziwa Huron huko Michigan karibu na mpaka wa Canada - kimeelezewa na maafisa wa ulinzi kilikuwa na "muundo wa pembetatu".

Kiliangushwa na kombora lililorushwa kutoka kwenye ndege ya kivita ya F-16 saa 14:42 saa za ndani (19:42 GMT).

Tukio hilo linazua maswali zaidi kuhusu msururu wa vitu vya angani ambavyo vimedunguliwa Amerika Kaskazini mwezi huu.

Hata hivyo Kamanda wa Kamandi ya Kaskazini ya Marekani Jenerali Glen VanHerck alisema kuwa hakuna dalili ya tishio lolote.

"Sitaziainisha kama puto. Tunaziita vitu kwa sababu fulani," alisema.

"Tunachoona ni vitu vidogo sana sana," aliongeza.

Uvumi kuhusu vitu hivyo unaweza kuwa umeongezeka katika siku za hivi karibuni.

"Nitaruhusu jumuiya ya wasomi na jumuiya ya kukabiliana na ujasusi kubaini hilo," Jenerali VanHerck alisema alipoulizwa ikiwa inawezekana vitu hivyo ni vya kigeni au vya nje ya nchi.

"Sijakataza chochote kwa wakati huu."

Puto linaloshukiwa kuwa la kijasusi la China liliangushwa kwenye ufukwe wa South Carolina tarehe 4 Februari baada ya kuelea kwa siku nyingi juu ya anga la Marekani. Maafisa walisema ilianzia China na limekuwa ikitumika kufuatilia tovuti nyeti.

Uchina ilikanusha kuwa kitu hicho kilitumika kwa ujasusi na kusema kuwa ni kifaa cha kuangalia hali ya hewa ambacho kilikuwa kimepotea uelekeo. Tukio hilo - na majibizano ya hasira katika matokeo yake - yalichochea mvutano kati ya Washington na Beijing.

Lakini siku ya Jumapili, Afisa wa ulinzi alisema Marekani ilikuwa imewasiliana na Beijing kuhusu kitu cha kwanza kilichoonekana kwenye anga lake, baada ya kutopokea majibu kwa siku kadhaa. Haikuweza kufahamika mara moja kilichojadiliwa.

Tangu tukio hilo la kwanza, ndege za kivita za Marekani zimeviangusha vitu vingine vitatu kwenye anga la Marekani.

Rais Biden aliamuru kitu kingine kuangushwa kaskazini mwa Alaska siku ya Ijumaa, na siku ya Jumamosi kitu kingine kama hicho kilitunguliwa kwenye anga la Yukon kaskazini-magharibi mwa Canada.

Marekani na Canada bado zinafanyia kazi kurejesha mabaki, lakini utafutaji wa mabaki hayo huko Alaska umetatizwa na hali ya hewa.

"Vitu hivi havikufanana kwa karibu, na vilikuwa vidogo zaidi kuliko, puto la [Februari 4] na hatutavitambulisha kwa uhakika hadi tuweze kupata mabaki yake," msemaji wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu alisema.

Matukio ya vitu visivyojulikana kwenye anga la Marekani

Februari 4: Wanajeshi wa Marekani walililitungua puto linaloshukiwa kuwa la ufuatiliaji katika pwani ya Carolina Kusini. Iilikuwa linaelea kwa siku kadhaa kwenye anga la Marekani, na maafisa walisema lilitoka China na limekuwa likifuatilia tovuti nyeti.

Februari 10: Marekani yadungua kitu kingine Kaskazini mwa Alaska ambacho maafisa walisema hakina mfumo wowote wa kukiendesha au kudhibiti.

Februari 11: Ndege ya kivita ya Marekani ilikitungua "kitu cha anga cha juu" kwenye eneo la Yukon nchini Canada, takriban maili 100 (kilomita 160) kutoka mpaka wa Marekani. Ilielezewa kilikuwa kidogo kuliko puto la kwanza.

Februari 12: Ndege za Marekani zilitungua kitu cha nne kwenye anga za juu karibu na Ziwa Huron "kutokana na tahadhari nyingi".

Afisa mmoja mkuu aliiambia ABC News kwamba vitu ama vyombo vitatu vya hivi majuzi zaidi vya kuangushwa huenda vilikuwa vifaa vya hali ya hewa na si puto za uchunguzi.

Lakini hii ilionekana kupingwa na Mwanademokrasia mkuu katika Congress, ambaye hapo awali aliambia shirika la utangazaji kwamba maafisa wa ujasusi waliamini kuwa vitu hivyo ni puto za uchunguzi.

"Wanaamini lilikuwa [puto], ndio," Kiongozi wa wabunge wengi katika Seneti Chuck Schumer alisema, akiongeza kuwa vilikuwa "vidogo zaidi" kuliko kile cha kwanza kilichodunguliwa kwenye pwani ya Carolina Kusini.

Debbie Dingell wa chama cha Democrat, mmoja wa wanachama kadhaa wa Congress wa Michigan ambaye alipongeza jeshi kwa kuangusha kifaa kingine Jumapili, akitaka White House na maafisa wa ulinzi kutoa habari zaidi.

"Tunahitaji ukweli kuhusu vinatoka wapi, vina malengo gani, na kwa nini vinaongezeka," alisema.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi Ben Wallace wa Uingereza alisema nchi hiyo itafanya mapitio ya usalama kufuatia matukio ya hivi majuzi nchini Marekani na Canada.

"Maendeleo haya ni ishara nyingine ya jinsi taswira ya tishio la kimataifa inavyobadilika na kuwa mbaya," alisema.