Simulizi kuhusu barua za mapenzi zilizozuiliwa za wanawake Wahispania kwa wanaume wa Morocco

Barua na picha

Barua zilizoshikiliwa zilizoandikwa kwa wanaume wa Morocco kutoka kwa wanawake wa Uhispania miongo kadhaa iliyopita zinaonesha historia ya mambo ya miiko wakati wa ukoloni.

"Utarudi lini Uhispania?" swali la kukata tamaa lilikuwa limeandikwa kwa uangalifu kwenye ukurasa, ishara ya jinsi ilivyokuwa muhimu kwa Carmela.

"Niambie kuwa hauwatazami wanawake wengine," aliandika kutoka Granada mnamo 1944.

Lakini maneno haya yalikusudiwa kamwe kutosomwa. Barua ya mapenzi iliyosafiri kimataifa ya Carmela haikufika mahali ilipokusudiwa nchini Morocco.

Badala yake, iliishia kufichwa ndani kabisa katika hifadhi za Kihispania, katika eneo la siri kulikowekwa mamia ya ujumbe wa mahaba kati ya wanawake wa Uhispania na wanaume wa Morocco.

Walikamatwa kati ya miaka ya 1930 na 1950, wanaandika kuhusu uhusiano wa karibu uliopigwa marufuku.

Kwa miongo kadhaa, mamlaka ya kikoloni ya eneo la ulinzi la Uhispania nchini Morocco waliikamata barua hii.

Masanduku yamejaa maneno ya mapenzi: "Ninapata wazimu kwa ajili yako," anaandika mwanamke mmoja kutoka Valencia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi zina picha, kuna picha nyingi za wanawake zinazoonesha sura ya kuwakumbusha wapenzi wao wa mbali jinsi walivyo. Mmoja alituma picha yake akiendesha baiskeli, taswira ya maisha ya kila siku.

Zote ziliwekwa wazi katika bahasha na watendaji wa serikali walio makini, na kisha kusahaulika.

Ziliingia vumbi mpaka zilipopatikana na kuchapishwa na wasomi Josep LluísMateo Dieste na Nieves Muriel García.

Kila barua ina mwonekano wa kuvutia katika uhusiano mzima, lakini kila moja pia inatuambia kuhusu ukandamizaji ambao mahusiano haya yalikabili.

Maafisa wa Uhispania walijaribu kila walichoweza kufanya uhusiano huu usiwezekane.

Kama agizo moja lilivyosema mnamo 1937: "Kama sheria ya jumla, ndoa kati ya wanajeshi wa Morocco na wanawake wa Uhispania lazima zizuiwe."

Tangu 1912, Uhispania ilidai mamlaka juu ya sehemu ya Morocco kama ulinzi, ikigawanya nchi hiyo katika kanda mbili, pamoja na Ufaransa.

Wapiganaji wa jumuiya ya Waberber walipinga hili, maarufu sana katika Vita vya Rif vilivyodumu kwa muda mrefu na vya umwagaji damu kati ya 1921 na 1926, ambavyo vilishuhudia jeshi la Uhispania likiangamizwa na vikosi vilivyoongozwa na Abdelkrim al-Khattabi.

Ili kuondokana na changamoto hiyo, serikali ya Uhispania iliongeza idadi ya wanajeshi wake nchini Morocco na kuajiri maelfu ya raia wa Morocco kuhudumu katika jeshi lake.

Kufikia miaka ya 1930 ukanda mrefu kando ya kaskazini mwa nchi, kutoka pwani ya Atlantiki huko Asilah mpaka karibu na mpaka na Algeria upande wa mashariki, ulisimamiwa vilivyo na Uhispania na mji mkuu wake huko Tetouan.

Ilikuwa kutoka kwenye kambi za kijeshi katika eneo hili ambapo mnamo 1936, Jenerali Francisco Franco alianzisha mapinduzi dhidi ya serikali ya Republican, na kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Uhispania.

makazi

Vita vilipokuwa vikiendelea, ghafla maelfu ya wanaume wa Morocco walioandikishwa kujiunga na jeshi la Uhispania walitumwa kuvuka bahari hadi Uhispania kupigana pamoja na vikosi vya Franco.

Zaidi ya wanajeshi, wanafunzi, wafanyabiashara na wafanyakazi wengine pia walijiunga nao na kuishia kuishi kote nchini, katika miji na maeneo ya mbali zaidi ya vijijini.

Popote walipokwenda, wanaume wa Morocco walikutana na wanawake wa Uhispania.

Huko Salamanca, mwanamke anayeitwa Concha alikutana na Nasar, mwanajeshi wa Morocco.

Akiwa na mapenzi tele, aliandikia wakuu wake ruhusa ya kuolewa naye mwaka wa 1938. Lakini kwa wakoloni wa Uhispania, mawasiliano kama hayo yalipaswa kupigwa marufuku kabisa.

Walionesha kuchukizwa na Concha, ambaye walimdharau kama mzee, "mbaya, mnene kama kiboko na mlegevu kwa mwendo''.

Walishuku kwamba Nasar alikuwa ameonesha kupendezwa tu kwa sababu Concha alitokea kuwa na nyumba, jambo ambalo liliamsha "upendo wake uliozidi kipimo".

Maagizo rasmi yalipaswa kuweka "vigingi vingi iwezekanavyo" kuzuia uhusiano huu "bila kupiga marufuku waziwazi", kama agizo moja lilivyowekwa mnamo 1937.

Hakika, kwa vile utawala wa Franco ulitegemea uaminifu wa askari wa Morocco, hawakufanya uhusiano huo kuwa haramu waziwazi. Badala yake, walitengeneza safu nzima ya njia za kuwafanya kutowezekana kwa vitendo.

Kwa mfano, ikiwa mwanamke atagunduliwa kumwandikia mwanaume wa Morocco, watampiga marufuku kuingia Morocco.

Mara nyingi, walipiga marufuku pia mwanaume wa Morocco kuingia Uhispania, na kufanya uhusiano wao usiwezekane.

Barua

Mnamo 1948, barua ilinaswa kati ya Carmen kutoka Zaragoza kwenda kwa mpenzi wake Abdeselam huko Morocco. Wenye mamlaka katika Tetouan wawalipiga marufuku mara moja wote wawili wasivuke kwenda upande mwingine.

Katika barua hiyo, Carmen alitoa habari kuhusu binti yao, ambaye sasa angekua bila kumuona baba yake. Viongozi hawakumtilia maanani mtoto huyo.

Kwa nini walichukulia mahusiano haya kwa dharau kama hii?

Sehemu ya jibu liko katika itikadi ya udikteta.

Serikali ya Franco ilikuwa na chuki dhidi ya wanawake, ikidhibiti kwa ukali uhamaji wa wanawake na kuwazuia kupata ajira.

Pia ilijiona kama mtetezi wa Ukatoliki, na kwa sababu za kidini, wanawake walioolewa na wanaume Waislamu walionekana kama "waliopotea kwa imani".

Lakini sababu kubwa zaidi ilikuwa kile maafisa walichokiita "heshima".

Ili utawala wa kikoloni uendelee, Uhispania ilibidi ionekane kuwa bora kuliko Morocco.

Kwa vile serikali ilielewa ndoa kuwa chini ya mwanamke na mwanaume, ndoa yoyote katika mgawanyiko wa ukoloni inlimfanya mwanamke wa Kihispania kumtii mwanaume wa Morocco.

Hili likijulikana, lingedhoofisha msingi wa utawala wa kikoloni.

Ingawa hatua mbalimbali za kukatisha tamaa mahusiano haya zilitoka kwenye kutoidhinishwa hadi kupigwa marufuku moja kwa moja, kanuni ya msingi ilikuwa sawa: mahusiano kama hayo yalikuwa tishio.

Barua hizi, hata hivyo, zinafichua kwamba chini ya uso wa jamii ya kikoloni, mikutano ilikuwa ya kawaida na ilisababisha aina mbalimbali za mahusiano: urafiki, uchumba, ngono na ndoa.

Kuzifungua ni jambo la kufurahisha.Lakini pia inasikitisha, maandiko mengi hayakuwahi kufika kule yalikokusudiwa. Ni kama uvamizi wa faragha, kwani watu hawa hawakuwahi kuchagua kujumuishwa kwenye kumbukumbu hii.

Morocco ilipopata uhuru mnamo 1956, serikali ya ulinzi huko Tetouan ilifungwa na kumbukumbu zake zilisahaulika.

Ziliishia karibu na Madrid, katika hifadhi kuu ya kumbukumbu ya utawala katika mji wa chuo kikuu wa Alcala de Henares ambapo, kama historia nyingi za ukoloni wa Uhispania barani Afrika,zilisahaulika.

Lakini licha ya kuchapishwa hivi karibuni kwa baadhi ya barua hizi, hadithi zao bado hazijulikani, na kumbukumbu hii ya muda mrefu bado haijafichua siri zake zote.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa ana Ambia Hirsi