Wachezaji 100 wakiwemo wakubwa 'watemwa' EPL

Chanzo cha picha, EPL
Baada ya msimu wa 2024/25 kukamilika, vilabu vya Ligi Kuu England (EPL) vimechapisha rasmi orodha ya wachezaji wanaoachwa huru leo Juni 30, 2025, kufuatia mikataba yao kumalizika.
Wako baadhi ya majina makubwa yakiondoka na kuachwa kama wachezaji huru (free agent), wakati baadhi tayari wameanza mipango ya maisha mapya nje ya EPL.
Miongoni mwa majina yanayovutia sana macho ya mashabiki na wachambuzi ni Kevin De Bruyne, aliyekuwa kiungo nyota wa Manchester City kwa kipindi cha miaka tisa. De Bruyne, ambaye alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya City chini ya Pep Guardiola, ameondoka rasmi baada ya mkataba wake kufikia kikomo.
Mnamo tarehe 12 Juni 2025, klabu ya Napoli ya Italia ilitangaza rasmi kumsajili kiungo huyo kwa mkataba wa miaka miwili, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. De Bruyne, ambaye alihusishwa pia na vilabu vya Saudi Arabia, MLS na baadhi ya klabu za EPL, ameona ni muda muafaka kuendelea na soka la ushindani katika Serie A na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa upande wa Thomas Partey, kiungo wa kati kutoka Ghana, naye ameondoka rasmi Arsenal baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na uongozi wa Mikel Arteta.
Partey, ambaye alijiunga na Arsenal kutoka Atletico Madrid mwaka 2020, amekuwa akisumbuliwa na majeraha na kuwa mguu ndani mguu nje katika kikosi cha kwanza. Kwa mujibu wa taarifa kutoka TBR Football, klabu ya Galatasaray ya Uturuki ipo katika mazungumzo ya kumsajili Partey, ambaye anapendelea kupata dakika za kucheza zaidi kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2026.

Chanzo cha picha, Getty Images
Galatasaray pia inahusishwa na nia ya kumnasa kiungo mwingine mwenye uzoefu mkubwa Ilkay Gündogan, ambaye kwa sasa anachezea FC Barcelona. Gündogan bado hajatangaza hadharani hatima yake, lakini ripoti zinaeleza kuwa hana uhakika wa nafasi ya kudumu chini ya kocha Hansi Flick, ambaye ameanza kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Barcelona.
Galatasaray wana matumaini ya kutumia uzoefu wa wachezaji hawa wawili katika kampeni zao za ndani na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbali na wachezaji hao, vilabu vingine vya EPL vimewaachia nyota kama Jamie Vardy wa Leicester City, ambaye anaripotiwa kuvutiwa na vilabu vya MLS na Saudi Pro League, na Victor Lindelöf wa Manchester United, anayehusishwa na Napoli na Lazio ya Italia.
Wengine ni Christian Eriksen, ambaye pia ameondoka Manchester United na kuvutia klabu za Uturuki kama Beşiktaş, na Ashley Young, aliyemaliza mkataba wake na Everton. Kiungo wa Italia, Jorginho amejiunga na klabu ya Brazil, Flamengo following his departure from Arsenal.
Kwa jumla, zaidi ya wachezaji 100 wametajwa kwenye orodha za vilabu 20 vya EPL waliomaliza mikataba yao msimu huu. Dirisha la usajili wa majira ya joto limefunguka rasmi, na ushindani wa kuwasajili mastaa hawa unaendelea kuongezeka.
Wadau wa soka wanatarajia kuona hatua zaidi katika wiki zijazo, huku dirisha la usajili likiwa wazi hadi Septemba 2025 kwa vilabu vya EPL na nchi nyingi Ulaya.















