Muuguzi aliyegeuka na kuwa mwalimu wa taekwondo nchini Nigeria

Chanzo cha picha, OTHER
Sio kawaida kabisa kwa muuguzi kutumia muda wake kupiga watu mateke na ngumi - lakini Adaeze Efobi si daktari wa kawaida.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 bado anaweza kuelekea Olimpiki kuiwakilisha Nigeria katika taekwondo.
Efobi aliipenda taekwondo alipokuwa akiitazama kwenye televisheni akiwa na umri wa miaka saba, lakini hakupata fursa ya kushindana hadi alipokuwa na umri wa miaka 22.
''Niliwaambia wazazi wangu kuwa ninavutiwa na taekwondo lakini wakati huo waliamini sanaa hii ni aina ya uhuni," Efobi aliambia BBC Sport Africa.
"Nilicheza mpira wa vikapu na mpira wa miguu na pia nilishiriki katika mbio za kutembea nikiwa katika shule ya upili."
Licha ya kuzaliwa na kukulia Lagos, ni wakati tu Efobi alipowekwa makazi katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ebonyi, ambapo alikuwa akisomea digrii ya uuguzi, ndipo aliweza kutimiza ndoto ya utotoni.
"Katika mwaka wangu wa pili, wanafunzi wenzangu walikuwa na mechi ya mpira wa miguu na darasa lingine. Nilitazama tu na kuona kundi la wanafunzi wakifanya taekwondo, wakiwa wamevalia sare zao na mikanda yao," Efobi alikumbuka.
"Nilikwenda kwenye kikao chao cha mafunzo, nikajaza makaratasi yaliyohitajika na nikaanza. Niligundua kuwa mapenzi niliyokuwa nayo nikiwa na umri wa miaka saba bado yalikuwa pale."
Sasa Efobi ambaye ni muuguzi aliyehitimu na mwalimu wa taekwondo anaamini kuwa mchezo huo umemsaidia maishani, hasa kuhusu nidhamu binafsi.
“Nilikua mtoto sikuweza kujieleza lakini nililazimika kufanyiwa mazoezi mengi ili kurekebisha hali hiyo,” alisema.
"Nilijifunza kwamba watu waliokomaa hutumia midomo yao, hawatumii mikono yao. Hiyo ni nidhamu, na nilianza kuifanya kuwa sehemu ya maisha yangu.
"Mimi ni mtu bora zaidi nikijilinganisha sasa na jinsi nilivyokuwa hapo awali. Kuvuka vikwazo hivyo, nilijiona nikifanya mambo fulani ambayo yalinishangaza mimi na familia yangu walipogundua kuwa nafanya taekwondo.'
Kuleta uuguzi katika taekwondo

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkuu wa taekwondo nchini Nigeria Ferguson Oluigbo anaamini Efobi ana fursa kubwa dhidi ya wapiganaji wenzake kutokana na historia yake ya uuguzi.
"Naangalia siku atakwenda na timu ya taifa kwenye Olimpiki - sio tu kama mfanyakazi mwenza lakini kama mtaalamu wa matibabu," Oluigbo alisema.
"Anakwenda kushindana na pia atakuwa uwanjani akisaidia timu ya madaktari. Anaelewa nini kitatokea kwa mguu wako unapofanya taekwondo - tofauti na muuguzi au daktari ambaye hajui lolote kuhusu michezo.
"Atasema 'hapana, hicho kitu unachokigusa sio maumivu, hapa ndipo maumivu yanatoka' kwa sababu anaelewa."
Oluigbo ni mkufunzi mwenye uzoefu wa mashindano ya olimpiki, akiwa miongoni mwa wakufunzi waliomsaidia Chika Chukwumerije kushinda medali ya shaba kwenye Michezo ya Beijing ya mwaka 2008.
Efobi, wakati huo huo, ameshinda mataji kadhaa ya uzito wa kati na anatarajia kuwa bingwa wa kitaifa katika kiwango chake.
Pia anashindana katika poomsae - shindano lisilo la kupigana la sanaa ya kijeshi ambapo unapitia mfululizo wa hatua na mashambulizi - na anafundisha katika shule ya Pan African Martial Arts International (Panamai), ambapo anaweza kuchanganya mambo mawili anayopenda zaidi. .
"Ninafuata ninayoyapenda, ambayo ni kuwa mwalimu wa taekwondo, lakini ninaleta uuguzi katika taekwondo – ninashughulikia majeraha wakati wa mafunzo ya taekwondo," alisema.
"Ninaamini kuwa muuguzi ni kusaidia watu na sio lazima ufanye kazi hospitalini kusaidia watu, naweza kufanya kazi kwenye kampuni, gym au mahali popote ninapotaka.
"Kama msemo unavyoenda, fanya kile kinachokufurahisha; napenda uuguzi na nina shauku kubwa ya taekwondo."
Kuokoa maisha na kujenga urithi

Chanzo cha picha, OTHER
Efobi anafanya kazi kama muuguzi anayehama na anakumbuka tukio moja ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa kwa hamu yake ya kusaidia wengine.
“Nilikuwa narudi kutoka kumtibu mtoto na kulikuwa na huyu mwendesha pikipiki ambaye alikuwa amegongwa na gari,” alisema.
“Nilishuhudia tukio hilo na nilikuwa katikati ya watu nikiwarudisha nyuma nikijaribu kuwafanya wasimguse.
"Nilikuwa nikizungumza naye, nikimtuliza, nikiangalia mifupa iliyovunjika. Alikuwa akivuja damu.
"Akili yangu ilikuwa imechanganyikiwa. Ilikuwa ni kama 'anavuja damu, sina glavu'. Lakini ilinibidi kuokoa maisha yake.
"Nilichofanya kilikuwa cha hatari. Kimsingi, nisingekuwa kigusa maji maji ya mwili bila glavu. Ilibidi nijipange, nikachukua nguo, nikairarua na kufunga jeraha.
"Alikuwa amevunjika. Niliisogeza kwa kiasi fulani ili kuunganisha miguu na mikono. Baadhi ya wapita njia na mimi tukampeleka hospitali ya karibu. Nina furaha mtu huyo aliishi kuona siku nyingine."
Efobi anatumai uzoefu wake wa maisha uliounganishwa unaweza kusikika mbali zaidi anapokutana na wagonjwa mbalimbali katika kazi yake ya uuguzi na kuwafunza watu kutoka mkanda mweupe hadi mweusi katika taekwondo.
"Mwishowe, ninataka kuwa na urithi ambapo siku moja sisi katika shule zetu za Panamai katika Afrika Magharibi tutakusanyika sote kuona wale wote ambao shirika limetoa," alisema.
"Naona tukiwa tumeketi chini na kila mtu kwenye picha. Ni jambo la kujivunia."












