'Walifikiria kuachana na ndoa zao kwa sababu ya kupoteza hamu ya tendo la ndoa'

- Author, Na Martha Saranga
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ukiona mti umekauka ghafla, usikimbilie kukata chunguza mizizi yake. Ndivyo ilivyo kwa wanawake wengi wanapoingia kwenye kipindi cha ukomo wa hedhi. Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), mwaka 2021 wanawake waliofikisha umri wa ukomo wa hedhi hasa wa miaka 50 na zaidi walikuwa asilimia 26 ya wanawake na wasichana wote duniani.
Kufikia mwaka 2030 wanawake waliopitia ama wanaopitia ukomo wa hedhi inatarajiwa kuwa bilioni 1.2 huku wanawake zaidi ya milioni 47 wakiingia katika kipindi hiki kila mwaka.
Ngoma ya mwili huchezwa kimya kimya, lakini moshi wa moyo huonekana hata mbali. Hivyo hivyo hali ilivyo kwa wanawake wanaokabiliwa na ukomo wa hedhi, ni hatua ya maisha ambayo huja kimyakimya, lakini huacha athari kubwa katika miili yao, hisia zao, na hata mahusiano yao ya kifamilia.
Katika jamii zetu, haya mambo huzungumzwa kwa sauti ya chini au kufunikwa kabisa. Lakini sasa ni wakati wa kuvunja ukimya. Ni nani atakayempigia kengele paka? Mmoja wao ni Aloisia Shemdoe, mwanaisimu, mtafiti wa afya ya jamii na sauti ya wanawake wanaopitia mabadiliko ya ukomo wa hedhi ambaye ameamua kulisemea hili kwa uwazi, bila woga, bila aibu.
Katika kusanyiko moja la Kikristo hapa Tanzania, alipata nafasi ya kuzungumza na wanaume. Wakiwa peke yao, walifunguka. Wengi walieleza kuwa wamekuwa wakipitia changamoto katika ndoa zao. Walilalamikia wake zao kwa kuwa na hasira za mara kwa mara, kiburi, au mabadiliko ya kihisia ambayo hawakuyaelewa.
Baadaye, walipokuwa na nafasi ya kuelewa kwa kina, waligundua kuwa hawakuwa na maarifa kuhusu mabadiliko ya mwili na akili anayopitia mwanamke katika safari yake ya kuelekea ukomo wa hedhi.
"Wanaume wengi waliniambia kwamba hawakujua kuwa haya mabadiliko ni sehemu ya maisha ya mwanamke na si tabia mpya au dharau," anasema Aloisia Shemdoe, mtafiti wa afya ya jamii.
Kwa kuzingatia taaluma yake kama mwanaisimu na mtafiti wa masuala ya afya ya mama na mtoto, Aloicia Shemdoe ameandika kitabu kiitwacho "Safari ya Ukomo wa Hedhi".

Chanzo cha picha, Aloicia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kitabu hiki kimeandikwa kwa lengo la kuboresha afya ya wanawake na jamii kwa ujumla, kwa kuleta uelewa juu ya hatua hii muhimu ya maisha ya mwanamke ambayo mara nyingi hupuuzwa au kufichwa.
Kwa kweli, miiko ya kijamii imekuwa kikwazo kikubwa kwa mijadala ya wazi kuhusu afya ya uzazi wa wanawake. Katika jamii nyingi za Kiafrika, masuala yanayohusu viungo vya uzazi au mabadiliko ya mwili wa mwanamke hayazungumzwi kwa uwazi kwa hofu ya kuonekana kukosa heshima. Hii husababisha wanawake wengi kuteseka kimya kimya.
Aloisia, ambaye sasa ana zaidi ya miaka 50, anasema kuwa safari yake ya kufikia ukomo wa hedhi ilimfungua macho na kuwa chachu ya kuwaelimisha wanawake wengine.
"Leo hii, tunaona wanawake maarufu kama Michelle Obama na Oprah Winfrey wakiamua kuvunja ukimya na kuzungumzia hadharani walichopitia. Hii inatia moyo,"anasema.
Aloisia anasisitiza kuwa kila mwanamke atapitia hatua hii maishani mwake. Ingawa kawaida huanza kati ya miaka 45 hadi 55, siku hizi kuna wanawake wanaanza mabadiliko haya wakiwa hata na miaka 38. Hali hii inachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, lishe, na mtindo wa maisha.
"Mabadiliko haya huathiri siyo tu mwili bali pia afya ya akili', anasema.
'Nilianza kusahau nywila za simu na kompyuta'

Chanzo cha picha, Aloicia
Alipoanza kusoma machapisho ya kimataifa aligundua kuwa hili ni jambo muhimu, la kawaida na la kimataifa, hivyo hakupaswa kukaa kimya.
Aloisia mwenye asili ya mkoa wa Tanga aliamua kubadili mtindo wa maisha. Anasisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi, kula lishe bora, na kuepuka mazingira yanayochochea msongo wa mawazo.
"Nilijiambia, siwezi kuandika kuhusu mazoezi na mimi mwenyewe sifanyi. Lazima nianze sasa," alisema kwa msisitizo.
Mwaka 2024, wakati wa Siku ya Wanawake Duniani, alianza rasmi kufundisha jamii kuhusu ukomo wa hedhi. Aliguswa na namna wanawake walivyojitokeza kwa wingi na kushiriki ushuhuda wa hali walizokuwa wakipitia.

Wengi walimshukuru kwa elimu waliyoipata, kwani ilikuwa mara yao ya kwanza kuelewa kuwa yale waliyokuwa wakipitia siyo laana, bali ni hatua ya kawaida ya mwili wa mwanamke.
"Baadhi ya wanawake waliniambia walikuwa wameanza kufikiria kuondoka kwenye ndoa zao kwa sababu ya kupoteza hamu ya tendo la ndoa, bila kujua chanzo ni nini,"anasema.
Hii ilithibitisha umuhimu wa elimu ya ukomo wa hedhi kwa wanawake na wanaume pia.
Ukomo wa hedhi si mwisho wa maisha ya mwanamke, bali ni mwanzo wa kipindi kipya chenye changamoto na pia fursa. Elimu husaidia wanawake kuelewa mabadiliko yanayotokea katika miili yao na kuchukua hatua stahiki za kuboresha afya yao na mahusiano yao ya kifamilia.
"Usikimbie ndoa yako kwa sababu ya ukomo wa hedhi. Badala yake, tafuta uelewa na msaada," anashauri Aloisia. Wanawake wengi wa Kitanzania huficha hali zao kwa hofu au aibu, na hili huwafanya waendelee kuteseka kimya kimya.
Ni wakati wa kuvunja ukimya

Chanzo cha picha, Alocia
Ni wakati wa jamii nzima wanawake kwa wanaume kuelimika kuhusu mabadiliko haya ya kimaumbile. Kwa kufanya hivyo, tutajenga jamii yenye afya bora, maelewano, na ustawi wa pamoja.
Aloicia anasisitiza kuwa wanawake walioko kwenye kipindi cha ukomo wa hedhi wanapaswa kuwa na afya bora kwa sababu wao ni walimu wa malezi kwa watoto, washauri kwa mabinti na wale wanaojifungua.
"Wanawake hawa wanabeba hekima na uzoefu mkubwa, hivyo afya yao ni msingi wa ustawi wa familia na jamii," anasema.
Wiki iliyopita, Aloicia alialikwa mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania, ambako alifundisha wanawake kuhusu ukomo wa hedhi. Muitikio ulikuwa wa kupendeza; wanawake walijitokeza kwa wingi, wakasikiliza elimu hiyo kwa makini na kuipokea kwa moyo mmoja.
Tukio hilo lilimpa faraja na motisha ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii nzima, akiamini kwamba maarifa haya ni nguzo ya kujenga familia zenye afya na maelewano bora.
Imehaririwa na Yusuph Mazimu















