Utafiti unaonyesha kuwa 'moyo' wa Dunia umepunguza kasi yake

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiini au 'moyo' wa Dunia ni mojawapo ya vipengele vya ajabu vya sayari yetu na uchunguzi wa kushangaza mara nyingi huonekana.
Wa mwisho ni kwamba inaonekana kuwa kimepunguza kasi na inawezekana kwamba kinazunguka kwa mwelekeo tofauti na uso wa dunia.
Hii sio harbinger ya apocalypse, lakini inaweza kuathiri kasi ambayo Dunia inazunguka, mabadiliko kidogo katika urefu wa siku zake na tabia yake ya sumaku, ingawa tafiti zaidi zinahitajika ili kudhibitisha hili.
"Tunaona ushahidi wa kutosha kwamba kiini cha Dunia kimekuwa kikizunguka kwa kasi zaidi kuliko uso wa dunia, lakini mwaka 2009 kilisimama," anasema mwanajiofizikia Song Xiaodong wa Chuo Kikuu cha Peking nchini China, mmoja wa waandishi wa utafiti mpya uliochapishwa Januari katika jarida la Nature Geoscience.
Kiini cha Dunia kimeundwa kwa vyuma na nikeli yenye radius ya kilomita 1,221. Ni eneo lenye joto sana katika nyuzi 5,400 °C na hulinganishwa na joto la Jua (5,700 °C).
Na kimezungukwa na safu nene ya vyuma vya majimaji kama msingi wa nje.
Kuelewa jinsi inavyozunguka imekuwa mada ya mjadala kati ya wanasayansi kwa miongo kadhaa.
Utafiti mpya unasema nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiini cha Dunia kimeelezewa kama aina ya "sayari ndani ya sayari". Kwa sababu inaelea kwenye safu nene ya unyevunyevu, inaweza kuzunguka kwa kujitegemea.
Ni vigumu kukielewa kiini hicho kwa usahihi. Kiko zaidi ya kilomita 5,000 chini ya miguu yetu. Kile kidogo tunachojua hupatikana kutokana na kupima tofauti ndogo ndogo za mawimbi ya tetemeko la ardhi yanayotokana na matetemeko ya ardhi na milipuko ya nyuklia.
Waandishi wa utafiti mpya, Song Xiaodong na Yang Yi, walilinganisha mitetemo hii na uchambuzi wa matetemeko tofauti ya ardhi katika miongo sita iliyopita.
Nadharia yao sio tu kwamba inabishana kwamba "kiini cha ndani huzunguka kutoka upande mmoja hadi mwingine kama swing", lakini pia hii hufanyika katika mizunguko ya miongo saba, na mabadiliko katika mwelekeo wa mzunguko kila baada ya miaka 35, kulingana na kile walichoelezea Shirika la habari la AFP.
Kulingana na matokeo yao, mara ya mwisho ilibadilisha mwelekeo ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 na mabadiliko yaliyofuata yangetokea katikati ya miaka ya 2040.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa maneno mengine, halitakuwa jambo jipya.
Watafiti walisema mzunguko huu unakaribiana na mabadiliko ya urefu wa siku, ambayo ni tofauti ndogo ya wakati halisi Dunia ianchukua kuzunguka kwenye mhimili wake.
Maoni tofauti
Hadi sasa hakuna ushahidi mwingi juu ya ushawishi wa tabia ya kiini hicho kwenye uso wa dunia, ingawa watafiti wanaamini kuwa kuna viungo vya tabaka zote za Dunia.
Yang na Song wanatumai kuwa matokeo yao "yatawahamasisha watafiti kuunda mifano ya majaribio ambayo huchukulia Dunia kama mfumo wa nguvu uliojumuishwa," wanasema.
Wataalamu wengine, hata hivyo, wanahofia utafiti huo mpya, wakitaja nadharia zingine na kuonya juu ya mafumbo mengi yanayoendelea kuhusu eneo hilo la kati la dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mojawapo ya maswali makubwa ambayo yamesalia ni jinsi ya kupatanisha kushuka kulikoelezewa na Yang na Song na mabadiliko ya haraka yaliyoripotiwa katika masomo mengine.
John Vidale, mtaalam wa matetemeko katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa California, alichapisha utafiti mwaka jana ukionyesha kwamba kiini cha Dunia huzunguka kwa kasi zaidi, kubadilisha mwelekeo kila baada ya miaka sita au zaidi.
Kwa upande wake hali hiyo ilitokana na mawimbi ya tetemeko la ardhi yaliyosababishwa na milipuko miwili ya nyuklia katika miaka ya 1970.
Hrvoje Tkalcic, mwanajiofizikia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, amechapisha utafiti mwingine unaopendekeza kuwa mizunguko ya kiini cha Dunia hudumu kati ya miaka 20 au 30 badala ya 70.
Kwa kuzingatia tofauti katika mifano, Vidale anatabiri "mshangao zaidi" kuhusu moyo wa ajabu wa sayari yetu.












