Jinsi China inavyopanga kuwa nchi yenye nguvu kubwa zaidi kwenye misheni za anga za mbali

Chinese flag in space with the Earth in the background

Chanzo cha picha, BBC; Getty Image; Nasa

Wanaanga watatu wa China wameanza misheni ya miezi sita, kufanya kazi kwenye kituo kipya cha anga za mbali cha nchi hiyo.

Ni hatua ya hivi punde zaidi ya Uchina kuelekea kuwa nchi yenye nguvu ya anga za mbali kwa miongo kadhaa ijayo.

Kituo cha anga cha Tiangong ni nini?

Mwaka jana, China iliweka katika obiti sehemu ya kwanza ya kituo chake cha anga cha Tiangong au "Ikulu ya Mbinguni". Inapanga kuongeza sehemuzaidi, kama vile maabara ya sayansi ya Mengtian, ifikapo mwisho mwa mwaka.

Mwaka ujao, itazindua darubini ya anga, iitwayo Xuntian. Hii itaruka karibu na kituo cha anga, na kutia nanga nayo kwa ukarabati na kujaza mafuta.

Tiangong itakuwa na nguvu zake, mifumo ya kuwezesha maisha na sehemu za kuishi.

Uchina ni nchi ya tatu tu katika historia kuwaweka wanaanga wote angani na kujenga kituo cha anga za juu, baada ya Muungano wa Kisovieti (sasa Urusi) na Marekani.

Ina matarajio makubwa kwa kituo cha Tiangong na inatumai itachukua nafasi ya Kituo cha Kimataifa cha Anga za Mbali (ISS), ambacho kinapaswa kusitishwa mnamo 2031.

Wanaanga wa China hawajajumuishwa kwenye ISS kwa sababu sheria ya Marekani imepiga marufuku shirika lake la anga za mbali, Nasa, kushiriki data zake na China.

Mipango ya China kufikia Mwezi na Mars

Matarajio ya China hayaishii hapo.

Miaka michache kutoka sasa inataka kuchukua sampuli kutoka kwa asteroidi karibu na Dunia.

Kufikia 2030, inalenga kuwa na wanaanga wake wa kwanza kwenye Mwezi, na kuwa itakuwa imetuma vyombo kukusanya sampuli kutoka sayari za Mars na Jupiter.

Timeline of China's space plan
1px transparent line

Nchi zingine zinafanya nini?

China inapopanua nafasi yake katika anga za mbali, nchi nyingine kadhaa pia zinalenga kufika Mwezini.

Nasa inapanga kurejea Mwezini na wanaanga kutoka Marekani na nchi nyingine kuanzia mwaka 2025 na kuendelea na tayari imepeleka roketi yake kubwa ya SLS katika Kituo cha anga za mbali cha Kennedy,

Japani, Korea Kusini, Urusi, India, Umoja wa Falme za Kiarabu pia wanafanya kazi kwenye misheni zao za mwezi.

India imezindua misheni yake kuu ya pili ya Mwezi tayari na inataka kuwa na kituo chake cha anga ifikapo mwaka 2030.

Wakati huo huo, Shirika la Anga za mbali la Ulaya, ambalo linashirikiana na Nasa kwa misheni za mwezi, pia linapanga kupeleka satelaiti za mwezi ili kuwarahisishia wanaanga kuwasiliana na Dunia.

line

Nani anatunga sheria za anga za mbali?

  • Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Anga za mbali 1967 unasema hakuna mahali popote angani panapoweza kudaiwa na taifa lolote
  • Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mwezi wa 1979 unasema kuwa anga haipaswi kutumiwa kibiashara, lakini Marekani, China na Urusi zimekataa kutia saini.
  • Sasa, Marekani inakuza Makubaliano yake ya Artemis, ikielezea jinsi mataifa yanaweza kutumia madini ya Mwezi kwa njia ya ushirikiano.
  • Urusi na Uchina hazitatia saini Makubaliano hayo, zikisema Marekani haina haki ya kutunga sheria za anga za mbali.
line

Je, historia ya Uchina kwenye anga za mbali ni ipi?

Uchina iliweka satelaiti yake ya kwanza kwenye obiti mnamo 1970 - ilipopitia usumbufu mkubwa uliosababishwa na mabadiliko ya Utamaduni.

Mataifa mengine pekee ambayo yameingia angani kwa hatua hiyo yalikuwa ni Marekani, Umoja wa Kisovieti, Ufaransa na Japan.

Katika miaka 10 iliyopita, China imerusha zaidi ya roketi 200.

Tayari imetuma ujumbe usiokuwa na mtu kwa Mwezi, unaoitwa Chang'e 5, kukusanya na kurejesha sampuli za mawe. Ilipanda bendera ya Uchina kwenye mwezi - ambayo ilikuwa kubwa kuliko bendera za zamani za Amerika.

Kwa kuzinduliwa kwa Shenzhou 14, China sasa imeweka wanaanga 14 angani, ikilinganishwa na 340 wa Marekani na zaidi ya 130 na Umoja wa Kisovieti (sasa Urusi).

Lakini kumekuwa na vikwazo. Mnamo 2021, sehemu ya roketi ya Uchina ilianguka kutoka obiti na kuanguka kwenye Bahari ya Atlantiki na pia kurushwa mara mbili hakukufaulu mnamo 2020.

Bar chart of government spending on space programmes
1px transparent line

Ni nani anayelipia mpango wa anga za mbali wa China?

Vyombo vya habari vya serikali ya China Xinhua vilisema takriban watu 300,000 wamefanya kazi katika miradi ya anga ya juu ya Uchina - karibu mara 18 zaidi ya wanaofanya kazi sasa katika Nasa.

Mamlaka ya Kitaifa wa Anga za Mbali ya China ilianzishwa mwaka 2003 kwa bajeti ya awali ya kila mwaka ya Yuan bilioni mbili ($300m, £240m).

Hata hivyo, mwaka 2016 China ilifungua sekta yake ya anga kwa makampuni binafsi, na haya sasa yanawekeza zaidi ya yuan bilioni 10 ($1.5bn, £1.2bn) kwa mwaka, kulingana na vyombo vya habari vya China.

Graphic of China's commercial launches
1px transparent line

Kwa nini China inaenda angani?

China ina nia ya kuendeleza teknolojia yake ya satelaiti, kwa mawasiliano ya simu, usimamizi wa trafiki ya anga, utabiri wa hali ya hewa na mambo mengine.

Lakini satelaiti zake nyingi pia zina madhumuni ya kijeshi. Zinaweza kuisaidia kupeleleza nchi pinzani, na kuongoza makombora ya masafa marefu.

Lucinda King, meneja wa mradi wa anga za mbali katika Chuo Kikuu cha Portsmouth, anasema China haizingatii misheni za anga za juu tu: "Wanafanya kazi kwa wingi katika nyanja zote za anga. Wana motisha ya kisiasa na rasilimali kufadhili programu zao."

Misheni za Uchina za Mwezi huchochewa kwa kiasi na fursa za kuchimba madini adimu kutoka kwa ardhi yake, kama vile lithiamu.