Sayari ya 2023 DZ2 inayoweza kusambaratisha jiji itapita kwenye anga ya dunia leo usiku
Ben Morris, BBC News

Chanzo cha picha, Getty Images
Sayari kubwa ya kutosha kuharibu jiji kwa mfano Dar es Salaam ama Nairobi iwapo itaanguka, itapita kati ya mizunguko ya Dunia na Mwezi mwishoni mwa wiki hii.
Sayari hiyo iliyopewa jina la 2023 DZ2, iligunduliwa mwezi mmoja uliopita.
Saa 19:49 GMT sawa na saa 4:49 usiku kwa saa za Afrika Mashariki siku ya Jumamosi (Machi 25,2023), itapita umbali wa kilomita 175,000 kutoka Duniani baada ya kuruka karibu na Mwezi.
Ni nadra kwa sayari kubwa kama hii - inayokadiriwa kuwa na kipenyo kati ya mita 40 na 90 - kuja karibu sana na sayari ya dunia.

Chanzo cha picha, GIANLUCA MASI, THE VIRTUAL TELESCOPE PROJECT
Wataalamu wameeleza kuwa ni tukio la mara moja baada ya muongo mmoja.
Kulingana na NASA, ni fursa muhimu kwa wanaastronomia kuongeza ujuzi wao kuhusu sayari ndogondogo (asteroidi), endapo kitu hatari kimegunduliwa chenye uwezo wa kuigonga Dunia.
"Hakuna nafasi ya 'muuaji wa jiji' kugonga Dunia, lakini mbinu yake ya kuja karibu inatoa fursa nzuri ya uchunguzi," alisema mkuu wa ulinzi wa sayari wa Shirika la Anga la Ulaya, Richard Moissl.
Bw Moissl alisema data ya awali iliyoonyesha 2023 DZ2 ilikuwa "kitu cha kuvutia kisayansi".
Lakini aliongeza kuwa data zaidi inahitajika ili kubaini muundo wa sayari hiyo.
Kwa njia hiyo ya karibu ya Dunia, asteroidi inaweza kuonekana kupitia darubini kubwa na darubini ndogo kote ulimwenguni.
Matangazo ya moja kwa moja ya wavuti ya mbinu yake yatatolewa na Mradi wa The Virtual Telescope.
Kitu hicho kinaonekana kurudi kwenye mzunguko wa Dunia mnamo 2026, lakini wanasayansi wamesema hakina tishio kwa dunia.
Mapema mwezi huu, sayari nyingine yenye ukubwa sawa, 2023 DW, ilipewa kwa kifupi nafasi moja kati ya 432 ya kugonga Dunia Siku ya Wapendanao 2046.














