Kuongezeka kwa walowezi wa kidini wenye misimamo mikali katika Ukingo wa Magharibi

Reha Kansara na Mohanad Hashim

BBC World Service

Issa Amro amefungiwa ndani ya nyumba yake mjini Hebron, katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa na Israel.

Bustani yake ilikuwa ikiongoza hadi barabarani, lakini sasa imezungushiwa uzio. Madirisha ya nyumba yake yamefunikwa kwa matofali, hakuna mwanga wala risasi inayoweza kupita. Hizi ni hatua ambazo anasema alichukua kwa ajili ya usalama wake

Mnamo tarehe 7,Oktoba, siku ambayo Hamas ilishambulia Israel, mwanaharakati huyo wa Kipalestina anasema alichukuliwa kutoka nyumbani kwake na kuzuiliwa kwa saa 10 na kushambuliwa na wanajeshi wa Israel, ambao baadhi yao anadai ni majirani zake walowezi.

"Ninaweza kukwambia majina yao. Naweza kukuonyesha huyu anaishi hapa na yule anaishi hapa," anasema.

"Wapalestina wengi hawatoki nje kwa sababu wanaogopa."

Wakati wa mazungumzo yetu ya simu kwa njia ya video, anaelekeza kamera kwenye tundu la mlango na kuonyesha watu watano, waliovalia kile kinachoonekana kama sare za kijeshi, wakishika doria mtaani kwake wakati wa amri ya kutotoka nje usiku.

Tulielekeza madai ya Issa kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF). Msemaji mmoja aliiambia BBC kwamba dhamira yao ni "kudumisha usalama wa wakazi wote wa eneo hilo na kuchukua hatua kuzuia ugaidi na shughuli zinazohatarisha raia wa Israell" na kuongeza kwamba wanafuatilia malalamishi yake.

Tangu vita vya Gaza vianze, ghasia dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi zimeongezeka sana. Umoja wa Mataifa unasema walowezi wamewaua Wapalestina wanane na kuwajeruhi zaidi ya 84.

Kuna watu 700,000 wanaoishi katika makazi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Makazi hayo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Baadhi ya watu wanaoishi humo ni wa vuguvugu la walowezi wa Kiyahudi wenye msimamo mkali wa kidini.

Wanaamini kuwa wanachukuwa ardhi ya kibiblia ya Yudea na Samaria, Ukingo wa Magharibi wa kisasa, kwa Israel. Wito huu unaochukuliwa kuwa wa hali ya juu unawatofautisha na jumuiya nyingine za walowezi wanaohamia maeneo yanayokaliwa kimabavu kwa sababu za kiuchumi au kusaidia kuimarisha usalama wa Israel katika eneo hilo.

Lakini kile kinachowaunganisha wote ni imani kwamba wana haki, iwe wamepewa na Mungu au la, kudai ardhi katika Ukingo wa Magharibi.

Imerekodiwa sana kwamba familia za Wayahudi na Waarabu wakati mmoja ziliishi bega kwa bega mjini Jerusalem. Lakini mji huo ulipogawanywa kati ya Israel na Jordan baada ya vita vya Waarabu na Waisraeli mwaka 1948, familia za Kiyahudi zilikimbia makazi yao huko Jerusalem Mashariki huku Waarabu wakikimbia makazi yao magharibi mwa mji huo.

Harakati za kisasa za walowezi zilianza katika miongo iliyofuata, baada ya Vita vya Siku Sita mnamo 1967, wakati Israeli ilipoteka Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki kutoka kwa nchi jirani ya Jordan na washirika wake wa Kiarabu.

Miezi kadhaa baada ya vita, makao ya kwanza ya kidini, Kfar Etzion, yalianzishwa. Leo inakadiriwa watu 40,000 wanaishi katika makazi hayo kilomita nne tu kutoka mpaka kati ya Israel na Ukingo wa Magharibi.

Mwaka mmoja baadaye, kiongozi wa Kidini wa Kizayuni Moshe Levinger na wafuasi wake waliingia Hebron kusherehekea Pasaka ya likizo ya Kiyahudi, lakini hawakuondoka viunga vya mji, yeye na wafuasi wake walianzisha Kiryat Arba.

Tofauti na Kfar Etzion, ambaye aliungwa mkono na serikali, Rabi Levinger na wanafunzi wake walikaa Hebron kwa kupuuza serikali, anaeleza mwandishi na profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Montreal, Yakov Rabkin. Wanahistoria na wataalamu anachukulia matukio ya hivi punde kama sehemu ya mageuzi ya harakati ya walowezi wa kidini.

"Wao [walowezi wa kidini] walikwenda kwenye vilima na sehemu mbalimbali zilizotajwa katika Biblia, na walijaribu kuzichukua, kwa sababu wanachotaka ni kuwa na ardhi yote]iliyoangazwa katika Biblia."

Leo, idadi ya jamii za walowezi imeongezeka hadi 300 katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, kulingana na shirika lisilokuwa la kiserekali la Israel Peace Now. Linasema hii inajumuisha makazi 146 na vituo 154 vya nje. Licha ya sheria za kimataifa, Israel inachukulia makazi hayo kuwa halali, hata hivyo inafafanua vituo vya nje kuwa haramu.

Neve Gordon, profesa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu katika Chuo Kikuu cha Queen Mary mjini London anadokeza kwambamakazi yanayoanza kama vituo vya nje mara nyingi huishia kuhalalishwa na taifa la Israel.

"Wataleta nyumba nyenye muundo wa trela kisha inafuatiwa na nyingine na nyingine. Na hivyo ndivyo watapata ardhi zaidi, na familia nyingine itahamia kituo hicho. Wanajeshi wanakuja siku inayofuata na kuweka askari wanne au watano huko kulinda ardhi na kulinda vituo hivyo."

Leo Uzayuni wa Kidini umejikita katika mfumo wa kisiasa wa taifa la Israel.

Msingi wa hili ni msukumo wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia kupitia serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

"Wana mwelekeo wa kutoa kauli za uchochezi zaidi. Ni rahisi kuzitaja kama ishara za mkondo huu wa itikadi kali wa Israel ambao unaenea katika serikali nzima," anaelezea Natasha Roth-Rowland, mtafiti anayechunguza mrengo wa kulia wa Kiyahudi.

Mlowezi na kiongozi wa chama cha Kizayuni cha Kidini Bezalel Smotrich amekuwa akitoa wito wa kunyakuliwa kwa makazi zaidi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kupitia chapisho la X, ambalo zamani lilijulikana kama Twitter, alitumia lugha ya uchochezi akiwataja Wapalestina kama Wanazi.

Mwezi Novemba, kama waziri wa fedha, alitetea kuongezeka kwa uwepo wa jeshi la Israel na kutoa wito wa kupiga marufuku Wapalestina kuvuna mizeituni karibu na makazi ya Waisraeli.

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir ni jina lingine linalohusishwa sana na vuguvugu la walowezi wa kidini.

Anaishi katika makazi ya Kiryat Arba na anasimamia polisi wa ndani wa Israeli pamoja na jeshi la mpaka wa nchi hiyo katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Aliwahi kuwa mwanachama wa vuguvugu la Kach lenye uzalendo wa hali ya juu, ambalo lilianzishwa na Mmarekani Rabbi Meir Kahane na sasa limepigwa marufuku nchini Israel chini ya sheria za kupambana na ugaidi.

Ben-Gvir amewahi kuhukumiwa kwa kuchochea ubaguzi wa rangi na kuunga mkono ugaidi.

Sehemu kubwa ya vuguvugu la walowezi wa kidini, katika ngazi ya chini na katika ngazi ya kisiasa, limetiwa moyo na ushawishi wa Marekani.

Mnamo 2021, video iliyoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo ilinasa mlowezi wa Kimarekani mwenye asili ya Kiyahudi akichukua nyumba ya mwanamke wa Kipalestina katika eneo la Jerusalem Mashariki linalokaliwa kimabavu, iligonga vichwa vya habari duniani kote.

"Unaiba nyumba yangu," Muna Al-Kurd alisema.

"Kamaa sitaiba mtu mwingine ataiba," Yaakov Fauci alijibu.

Kuna mashirika ambayo huwasaidia Wayahudi wa Marekani kama Fauci kuhamia Israel na maeneo yanayokaliwa na Waisraeli. Lakini sio tu mashirika yanayofadhiliwa kibinafsi yanayoendesha harakati za walowezi.

Wakili Mmarekani mwenye asili ya Kiyahudi na balozi wa zamani wa Marekani nchini Israel David Friedman anasadikiwa kuwaunga mkono walowezi wa kidini wenye uhusiano mkubwa na makazi ya Beit El, au House of God kwa Kiingereza. Makazi, ambayo ni nyumbani kwa Mwamba wa Yakobo, ni mahali ambapo, katika Biblia, Yakobo aliota ndoto ambapo Mungu aliwaahidi ardhi Waisraeli.

Chini ya Donald Trump, David Friedman alihusika katika sera kama vile kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.

Uwiano unatolewa na historia za walowezi wa Amerika Kaskazini - Prof Neve Rabkin anasema wale wanaounga mkono vuguvugu la kidini la walowezi kutaka "kuwaondoa Wapalestina ili kuchukua makazi yao".

Prof Yakov Rabkin anakubali: "Historia ya Israel inaambatana na historia ya Marekani; tofauti pekee ni kwamba nchini Marekani waliwaangamiza wakazi wengi wa eneo hilo, na Waisraeli hawakufanya hivyo. Lakini wanajaribu."

Tangu vita vilipoanza, Peace limerekodi kuanzishwa kwa makazi sita mapya katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi Jerusalem Mashariki yanayokaliwa kimabavu. Haijulikani kama walowezi hao wana mwelekeo wa kidini au wamehamia maeneo hayo kama sehemu ya mkakati mpana wa usalama.

Vita hivyo ni "janga ambalo limebadilika kuwa fursa," anasema Prof Neve Gordon.

Shirika la Youth Against Settlements lililoanzishwa na mwanaharakati Issa Amro, ambalo linatetea kukomeshwa kwa makazi ya Waisrael katika Ukingo wa Magharibi, linasema limelazimika kusitisha shughuli zake kutokana na ghasia zinazoendelea katika mji wa Hebron, Amro anasema umekabiliwa na tishio la kutekwa nyara, kufungwa jela na kuteswa.

"Nahisi hakuna ulinzi. Nahisi hakuna usalama. Angalia jinsi ninavyoishi. Ni nani anayenilinda?"

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Lizzy Masinga