Mazoezi rahisi unayoweza kufanya na kufurahia msimu wa sikukuu

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Lizzy Masinga
- Nafasi, BBC Swahili
Kutokana na ongezeko hilo la uzito wa mwili, idadi ya magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya viungo, PCOD, ugumba imeongezeka.
Nyakati hizi, magonjwa haya sio tu kwa watu wazima zaidi , lakini pia kwa vijana watano kati ya kumi wenye umri wa miaka 20 na 25.
Si lazima uwe mkimbiaji au uwe mwanamichezo ili ufahamu manufaa ya mazoezi.
Kufanya mazoezi fulani ni bora kuliko kutofanya chochote, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge wameeleza.
Wakati huu wa mapumziko ya mwisho, unapokuwa nyumbani kuna mazoezi mepesi ambayo mtu anaweza kuyafanya na kuyafurahia vilevile kufurahia wakati huu wa mapumziko.
Kutembea
Timu ya Idara ya huduma za afya Uingereza ilitazama tafiti zilizopita kuhusu faida za kuushughulisha mwili na kuhitimisha kuwa hata kufanya nusu ya kiasi kilichoshauriwa kunaweza kuzuia kesi moja kati ya 20 za maradhi ya moyo na karibu moja kati ya kesi 30 za saratani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni, ukosefu wa mazoezi ya mwili huchangia vifo milioni 3.2 kila mwaka.
Honey Fine, mkufunzi binafsi na mwalimu wa kampuni ya kimataifa ya mazoezi ya mwili ya Barry's, anasisitiza matatizo yanayotokana na kukaa chini sana bila kufanya mazoezi.
"Inaweza kupunguza kasi ya metaboliki yako na kuathiri ukuaji wa misuli na nguvu, ambayo inaweza kusababisha maumivu," anaiambia BBC.
"Kukaa chini kwa muda mrefu kunaweza pia kusababisha aina zote za matatizo ya mgongo, tunapata hii sana kwa watu wenye kazi za ofisi, kwamba migongo yao huwekwa mara kwa mara katika hali ya mkazo ambayo husababisha matatizo mengi zaidi baadaye katika maisha."
"Kazi kama vile kusimama, kubeba, kuosha sakafu, kuzungukazunguka, kutembea kwa miguu wakati unazungumza kwenye simu ni mambo madogo madogo ambayo hutufanya tuwe watendaji zaidi ambayo hutusaidia kuchoma kalori kwa ufanisi zaidi," alisema.
Kuruka kamba

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna njia nyingine za mazoezi nyumbani ya kufurahisha kama kuruka kamba unaweza kuweka muziki na densi. Kwa dakika 15.
Si tu yanafanya kazi kwenye moyo wako tu, lakini pia yataweka tabasamu kwenye uso wako.
Haijalishi umri wako, hupunguza maumivu ya viungo na kuzuia jeraha, huongeza nguvu. Mazoezi haya husaidia kupunguza hatari ya kuanguka, na kuimarisha misuli.
Yoga

Chanzo cha picha, Getty Images
Yoga ni aina ya zamani ya mazoezi ambayo inazingatia nguvu na kuwezesha kupumua ili kuimarisha ustawi wa kimwili na kiakili.
Yoga ni zoezi la kuimarisha misuli na miongozo inasema tunapaswa kufanya kwa siku mbili au zaidi kwa wiki, kila wiki, zoezi ambalo unaweza kulifanya nyumbani kipindi hiki cha mapumziko.
Kuendesha baiskeli

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dkt. Richard Ferguson, msomi, mhadhiri na mtafiti katika Fiziolojia ya Mazoezi katika Chuo Kikuu cha Loughborough, yeye pia ni mwendesha baiskeli mahiri.
Anashauri kuwa watu wanaweza kufanya zoezi jepesi la kuendesha baiskeli.
"Kwa sababu kuendesha baiskeli husaidia kurefusha maisha ya afya. Kama vile shughuli yoyote ya mchezo, hukuruhusu kuishi na afya njema kwa muda mrefu zaidi. Unaimarika zaidi, moyo wako unakuwa na nguvu na jinsi unavyosimamia lishe yako inakuwa bora."
Wataalamu wanashauri kujaribu kutembea kwenda kwenye maduka badala ya kutumia gari, au kucheza na watoto au wajukuu zako.
Wakati huu wa mapumziko, kuwa na shughuli za kukufurahisha katika utaratibu wako wa kila wiki ndiyo njia bora ya kuongeza kiwango cha mazoezi ya mwili unayofanya, wanasema.
Uchambuzi katika Jarida la Uingereza la Sports uliangalia utafiti uliochapishwa hapo awali juu ya faida za mazoezi katika karibu tafiti 100 kubwa na karibu nakala 200 zilizopitiwa ili kupata muhtasari wa ushahidi.
Waligundua kwamba ikiwa kila mtu atatenga angalau dakika 150 za mazoezi kwa wiki, basi karibu kifo kimoja kati ya sita cha mapema kingezuiwa.
Watafiti wanasema kujijengea tabia ya kufanya mazoezi ndio jambo linalohitajika.
Imehaririwa na Yusuf Jumah












