Ndoa ya utotoni: 'Niliuzwa kwa ajili ya ndoa kwa £7 nikiwa na umri wa miaka 12'

Chanzo cha picha, YOUSEF ELDIN / BBC
Na Megha Mohan na Yousef Eldin
BBC 100 Women
Inakadiriwa kuwa msichana mmoja kati ya watano duniani kote ameolewa akiwa na umri wa miaka 18.
Hata nchi ambazo zina sheria dhidi ya ndoa za utotoni nyakati nyingine hushindwa kuzitekeleza. Lakini nchini Malawi baadhi wanaona kuna dalili za kwanza za mabadiliko.
Mara ya tatu tulipomtembelea Tamara tuliambiwa kwamba alikuwa ameondoka asubuhi na mapema kwenda kwenye mashamba ya karibu kufanya shughuli za kilimo.
Katika ujauzito wa miezi tisa, mtoto huo mwenye umri wa miaka 13 hakupumzika.
Tamara (si jina lake halisi) alikuwa amelala chini sakafuni katika kibanda kidogo cha shangazi yake kwa miezi kadhaa baada ya mumewe, mwanamume mwenye umri wa miaka 20, kutoroka.
Alikuwa amesikia kwamba maafisa wa huduma za kijamii wanakuja kumwokoa Tamara kutoka katika ndoa yao haramu na akaondoka kabla hawajafika, ikabidi atembee hadi kijijini kwa shangazi yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mengi yamebadilika katika maisha ya Tamara katika miaka michache iliyopita. Akiwa amezaliwa katika familia ya wakulima iliyopo kijijini katika wilaya ya Neno kusini mwa Malawi, familia yake iliishi chini ya mstari wa umaskini wa serikali ya Malawi, kama asilimia 65 ya watu wengine katika eneo hilo.
Vita katika nchi ya Ukraine ambayo ni mshirika wa moja kwa moja wa biashara na Malawi, viliongeza shinikizo – kusimamisha usambazaji wa ngano na mbolea na kupandisha bei.
Wazazi wa Tamara walipougua na kufariki, mmoja baada ya mwingine mtoto wao wa pekee alichukuliwa na bibi yake.
Lakini baada ya mwezi mmoja, Tamara aliporudi kutoka shuleni siku moja, nyanya (bibi) yake alikuwa na habari fulani.
"Aliniambia lazima niolewe," Tamara anasema. "Tayari alikuwa amepokea pesa kutoka kwa mwanaume."
Mwanaume ambaye Tamara hakuwahi kukutana naye alilipa Kwacha ya Malawi 15,000 kwa ajili yake - karibu $9, au £7.
Bibi yake Tamara alikuwa tayari ameishatumia pesa hizo kununulia mahindi kwa ajili ya familia na mwanamume huyo sasa hakuwa na subira. Alitaka msichana aliyemlipia aache shule na kuishi naye.
Ndoa za utotoni zimekuwa kinyume cha sheria nchini Malawi tangu mwaka 2017, lakini kwa muda mrefu imekuwa zikikubalika kitamaduni nchini humo, na bado zinaendelea katika jamii za vijijini kama vile Tamara, ambako takriban 85% ya wakazi wa Malawi wanaishi.
Zaidi ya asilimia 40 ya wasichana nchini Malawi wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Girls Not Brides.
"Maisha yalikuwa magumu kwa sababu mwanamume huyo alikuwa mzee," Tamara anasema. "Alikuwa akininyanyasa kimwili kwa kuniuma kila nilipofanya jambo baya."
Aliishi naye kwa muda wa miezi mitatu, hadi mtu alipozitahadharisha huduma za kijamii. Kisha, mipango ilipokuwa ikifanywa ili Tamara arudi shuleni, aliona jambo fulani. Alikuwa amekosa hedhi kadhaa.
Tamara alikuwa na umri wa miaka 12 na anatarajia mtoto.
Takriban kilomita 100 (maili 62) kutoka kwenye kibanda cha shangazi yake Tamara, karibu na mpaka wa Msumbiji, kuna jengo dogo la kijani kibichi lenye kelele za muziki wa pop wa Malawi. Ni ofisi ya Radio Mzati, kituo cha redio cha hapa nchini Malawi.
Kundi la wasichana warembo walio katika umri wa miaka 20 na ushee wamekusanyika katika studio ya redio, wakirekebisha maikrofoni zao na kucheka wanapojitayarisha kwenda hewani.
"Habari! Hujambo! Karibu kwenye toleo jingine la Ticheze Atsikana," mtangazaji wa Boma la Chikondi Kuphata, "kipindi ambacho ni jukwaa letu sisi wasichana warembo kujadili masuala yanayotuhusu!"
Kuphata na mwandalizi mwenza wa kipindi Lucy Morris wanatangaza kwa lugha mbili Kiingereza na Chichewa kwa pamoja - jina la kipindi linamaanisha "hebu tuzungumze" kwa lugha ya Chichewa.
Ni kipindi cha kila wiki, kinachofadhiliwa na AGE Africa, shirika lisilo la kiserikali NGO ambalo linasaidia wasichana wa vijijini na walio katika mazingira magumu kuendelea na elimu, na kinawafikia zaidi ya wasikilizaji milioni nne kote Malawi. Wengi wa watazamaji ni wanawake katika jamii za vijijini kama Tamara.

Chanzo cha picha, BBC
Mada ya leo ni ndoa za utotoni.
"Sababu kuu hapa ni umaskini," anasema Morris. “Kwa sababu familia nyingi tunazotoka ni maskini, wazazi wetu hawana uwezo wa kuwalea watoto wao, hivyo suluhisho bora ni kumpeleka mtoto wa kike kwenye ndoa.
"Wasichana huolewa na wanaume wenye umri mkubwa zaidi kuliko wao ambao wanaweza kuwanunua."
Wanawake hao huwahimiza wasikilizaji wao kutuma maoni kupitia WhatsApp, kabla ya kucheza wimbo unaoitwa Come Back. Maneno yake yana ujumbe wazi:
"Sasa unahitaji shule kwa kila kitu!
"Ni bora urudi shule!
"Ndoa ya mapema sio nzuri!"
"Wasichana wanapokuwa na elimu na kujua haki zao, wanajua wanaweza kupata msaada wa kukomesha ndoa za utotoni. Hiyo ni sehemu ya dhamira yetu, kuwafanya wasichana kuzungumza, kushirikishana hadithi zao na kujua kwamba kuna njia nyingine," Morris anasema.
Kijiji chake, Gulumba, kilichopo chini ya Mlima Mulanje, kina klabu ya kusikiliza kipindi cha wanawake pekee cha Ticheze Atsikan.
Shabiki mwingine wa kipindi hicho, ingawa hajaalikwa kwenye kundi la wasikilizaji, ni chifu Benson Kwelani. Anasema anawahimiza wasichana kubaki shuleni, na hatatoa baraka zake kwa ndoa ikiwa msichana yuko chini ya umri wa miaka 18.
Kuolewa kama watoto
- Takriban wanawake milioni 650 walio hai leo waliolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef.
- Asia Kusini ndio nndiko kuna idadi kubwa zaidi ya watoto walioolewa wakiwa na zaidi ya 40% ya jumla ya wasichana wote duniani, ikifuatiwa na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye 18%.
- Ulimwenguni kote, takriban 21% ya wasichana huolewa utotoni, kulingana na shirika la misaada la World Vision
- Viwango vya ndoa za utotoni vimepungua barani Asia na Afrika katika muongo mmoja uliopita, lakini katika Amerika ya Kusini na Karibea hakuna maendeleo kwa miaka 25, kulingana na shirika lisilo la kiserikali (NGO) la Girls Not Brides.
Wiki mbili zilizopita, baada ya Michelle Obama, Amal Clooney na Melinda French Gates kuitembelea Malawi , Rais Lazarus Chakwera alitangaza ufadhili zaidi wa mkakati wa kitaifa wa kukomesha ndoa za utotoni.
Wafadhili hao watatu wenye ushawishi mkubwa wanafanya kazi nchini, wakisaidia mashirika ya ndani yanayopigana dhidi ya ndoa za utotoni.
Muungano wa Obama's Girls Opportunity Alliance, kwa mfano, unaunga mkono shirika la AGE Africa, wakati mpango wa Clooney wa Waging Justice for Women unaunga mkono Chama cha Wanasheria Wanawake cha Malawi kuwafahamisha wasichana wa vijijini kuhusu haki zao za kisheria. Nalo shirika la French Gates hufadhili miradi inayoboresha huduma za afya kwa wanawake, ikiwa ni pamoja na wasichana wanaojifungua mapema katika ujana wao.
Bado si kawaida kwa huduma za kijamii kuhusika katika visa vya ndoa za utotoni, mashirika yasiyo ya kiserikali yanasema, lakini mitazamo inaonekana kubadilika miongoni mwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo.
Baada ya msukumo wa Mfuko wa Idadi ya Watu Duniani wa Umoja wa Mataifa mwaka 2020, zaidi ya machifu 100 wa kimila wa Malawi - kama robo ya jumla - wameahidi kupiga vita ndoa za kimila katika jamii zao. Hata hivyo wanaweza kukosa nguvu ikiwa familia zinawatoa wasichana wao kwa wanaume wakubwa zaidi.
Machifu wawili katika wilaya ya Neno, ambako Tamara anaishi, wanatuambia hawakuweza kuwa na uhakika kwamba ndoa za utotoni hazifanyiki kwa siri katika jamii zao.
"Wazazi wengine hutukaripia, lakini tunawakatisha tamaa na kukataa ndoa hizo," anasema John Juwa, mkuu wa jumuiya ya zaidi ya watu 2,000.
"Wakati mwingine wazazi wanasisitiza kuwa mtoto wao yuko tayari kwenye ndoa, lakini tunaomba kijitabu chao cha utambulisho wa afya kuthibitisha umri wao."
George Mphonda, chifu wa zaidi ya watu 1,000, anasema: "Hatusemi kwamba ndoa za utotoni hazifanyiki bali tunasema ikitokea, basi zinafichwa kwetu."
Lakini ni jukumu la nani kusitisha ndoa za siri za utotoni?
Baada ya kimya kirefu Juwa anasema: "Ni jukumu letu kama machifu, tukiungwa mkono na familia."
Tamara amejifungua mtoto wa kiume mwenye afya njema. Shirika dogo lisilo la kiserikali la Malawi lenye makazi yake katika jiji la Blantyre, liitwalo People Serving Girls At Risk, lilimlipia mwanamume aliyekuwa akiendesha baiskeli kumpeleka kwa baiskeli hadi kwenye kliniki ya afya ya eneo hilo alipopata uchungu wa uzasi. Pia wanaingia mara kwa mara pamoja naye na shangazi yake.
Matatizo yanayotokana na ujauzito na kujifungua ndiyo chanzo kikuu cha vifo vya wanawake vijana kulingana na WHO, hivyo watu walikuwa wanamjali.

Chanzo cha picha, YOUSEF ELDIN/BBC
"Tamara amerejea nyumbani na anaendelea vizuri na mwanaye mdogo, familia yake ina furaha sana kuhusu kuwasili kwake," anasema Caleb Ng'ombo, mkurugenzi mtendaji wa People Serving Girls At Risk.
"Ana msaada wa jamii na shangazi yake, lakini kazi halisi inaanza sasa. Ingekuwa bora arudi shuleni lakini pia anahitaji kumsaidia mtoto wake."
Tamara anaiambia BBC kwamba matumaini yake makubwa kwa mwanawe, Prince, ni kwamba ataweza kumaliza shule.
Shangazi yake Tamara ana kibanda cha kuuza matunda na mboga ambacho huingiza chini ya $50 (£39) kwa mwezi. Ni hatua chache kutoka kwenye kibanda chao. Tamara humsaidia anapoweza, na huwaona marafiki zake.
Katika duka hilo, idadi fulani ya wasichana wachanga wanakuja kuchukua chakula kwa ajili ya familia zao.
Mara ya mwisho tulipotembelea duka hilo, angalau wasichana wawili wajawazito kutoka kijijini - wakiwa na mikono iliyojaa mboga - walimsalimia Tamara kabla ya kurejea nyumbani.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












