Urusi imetishia kuziharibu ndege za Poland na Slovakia zilizoahidiwa Ukraine

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Poland iliahidi Ukraine ndege nne aina ya MiG-29 siku ya Alhamisi

Ikulu ya Urusi imetishia kuharibu ndege zozote za kivita zitakazopewa Ukraine na washirika wake, baada ya nchi mbili kuahidi ndege za enzi za Usovieti.

Slovakia imekuwa nchi ya pili ya Nato kuahidi Kyiv baadhi ya ndege za MiG-29 siku ya Ijumaa, siku moja baada ya Poland.

Ndege za Slovakia zilizuiwa mwaka jana na haizitumii tena ndege hizo.

Ukraine imeziomba nchi za Magharibi kuipatia ndege za kisasa, lakini kwa sababu ya muda mrefu wa mafunzo, hatua hiyo inaonekana tu kama mpango wa muda mrefu

Inaona ndege za ziada kuwa muhimu kwa ulinzi wake na uwezekano wa mashambulizi ya kukabiliana, mwaka mmoja baada ya uvamizi wa Urusi.

Nchi nyingine za Nato zinafikiria kutuma ndege za enzi za Usovieti kama vile MiG, ambazo marubani wa Ukraine wamefunzwa kuzirusha.

Hii ni hatua nzuri kwa Ukraine - ambayo ina marubani wengi kuliko ndege - lakini haitaleta tofauti kubwa.

Raia wa Ukraine wanasema wanachohitaji sana ni ndege za kivita za F-16 zilizo tengenezwa Marekani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yuri Sak, mshauri mkuu wa ulinzi wa Ukraine, anasema wapiganaji wa kizazi cha nne wana uwezo bora zaidi.

Hilo bado linaonekana kutowezekana - angalau kwa sasa, kwani ingechukua muda kuwafunza marubani wa Ukraine kuhusu jeti za Magharibi.

Maafisa wa kijeshi wa nchi za Magharibi wanasalia na mashaka kuhusu nege za kivita za kisasa - lengo lao ni kusaidia Ukraine kushinda vita mashinani.

Mstari wa mbele wa vita umejaa mifumo ya ulinzi wa anga kwa pande zote mbili. Jeshi la anga la Urusi ni kubwa zaidi kuliko la Ukraine na halijaweza kupata udhibiti wa anga.

Habari za makabidhiano hayo zinajiri huku vyombo vya habari vya Urusi vikiripoti kwamba Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alikuwa amewapamba marubani waliohusika katika tukio la mapema wiki hii ambalo lilisababisha ndege isiyo na rubani ya Marekani kuanguka kwenye Bahari Nyeusi.

Washington imelaani kitendo cha Urusi, ambapo inasema moja ya ndege aina ya Su-27 iliigonga ndege hiyo isiyo na rubani, kama ya kutojali, lakini Moscow inasema ndege hiyo ilipata tatizo la kimitambo .

.
Maelezo ya picha, Ikulu ya Urusi imetishia kuharibu ndege zozote za kivita zitakazopewa Ukraine na washirika wake, baada ya nchi mbili kuahidi ndege za enzi za Usovieti.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amelaani mipango ya nchi za Nato, akisema kuwa ndege hiyo haitaathiri matokeo ya "operesheni maalum ya kijeshi" ya Moscow, kwenye vita, lakini badala yake "italeta masaibu ya ziada kwa Ukraine na watu wa Ukraine".

"Bila shaka, wakati wa operesheni maalum ya kijeshi, vifaa hivi vyote vitaharibiwa," aliongeza.

Mwanzoni mwa uvamizi kamili wa Urusi, Ukraine iliaminika kuwa na takriban ndege 120 zenye uwezo wa kivita - hasa MiG-29 na Su-27 zilizozeeka.

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Slovakia Eduard Heger alitweet kwamba serikali yake imeidhinisha kutuma 13 MiG-29 za nchi hiyo.

Alisema "ahadi lazima zitimizwe" na kwamba alifurahi kwamba wengine walikuwa wakijibu wito wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wa kutaka silaha zaidi.

Alisema Slovakia pia itatuma Ukraine sehemu ya mfumo wake wa ulinzi wa anga wa Kub.

Siku ya Alhamisi, Poland iliahidi MiG-29 nne, kutumwa katika siku zijazo, lakini nyingi zaidi zinatarajiwa kufuata.

Kama ilivyo kwa ahadi yake ya mizinga ya Leopard, imevunja kizuizi. Hii ilikuwa hatua ambayo hakuna mtu ambaye alikuwa tayari kuchukua mwaka mmoja uliopita.

Haijabainika ni ndege ngapi za Slovakia zinazofanya kazi.