Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Bomu lilipoanguka nilimwambia mwanangu kuwa ni filamu ya kivita'
- Author, Anne Soy
- Nafasi, BBC News Nairobi
Makabiliano makali ya hivi majuzi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan yalienea katika maeneo mapya ya nchi hiyo na kusababisha hofu ya kutokea maafa mapya ya kibinadamu huku mamilioni ya watu wakinaswa katikati ya mzozo huo ambao hauangaziwi tena sana kutokana na kuibuka kwa mizozo mingine duniani.
Mtoto wa Rasha Amin mwenye umri wa miaka mitano sasa anakojoa kitandani usiku kwa hofu baada ya nyumba ya jirani yake katika mji mkuu, Khartoum, kushambuliwa na kombora mwezi Oktoba.
“Anaamka usiku akilia kwa sababu aliota ndoto mbaya au anaogopa,” anasema mama huyo wa watoto wawili.
Kipande cha chuma chenye ukubwa wa mpira wa gofu kilikuwa kimetoboa tundu kwenye ukuta wake kupitia kiyoyozi na kumkosa mtoto mwingine wa Rasha, aliye na umri wa miezi 20, ambaye alikuwa amelala kitandani.
Kikosi cha wanamgambo kilichokuwa kimewekwa na jirani ndicho kilikuwa kinakusudiwa kulengwa na maelezo ya Rasha kwa mtoto wake mkubwa kuwa watu walikuwa wakirekodi filamu hayakumshawishi kwa muda mrefu.
Mwalimu huyo wa shule aliye na umri wa miaka 31 na familia yake waliponea chupuchupu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi minane ambavyo vimesababisha vifo takriban watu 10,000.
Watu wengine milioni saba wameyakimbia makazi yao lakini baadhi yao, kama vile Rasha na familia yake, walioamua kubaki wamenaswa katikati ya mapigano na kuumizwa kila wakati makabiliano yanapotokea.
Nyumba yake bado imeharibiwa vibaya.
Kwa kutumia simu yake anaonyesha BBC, nyufa kwenye ukuta, madirisha na milango ambayo haipo.
"Bado tunaogopa. Inabidi tuweke magodoro yetu kwenye sakafu mbali na madirisha," anasema kuhusu juhudi zake za kuweka familia yake salama. "Pia tunakaa karibu na jokofu ilikujikinga endapo paa litaanguka."
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na mshirika wake wa zamani, Rapid Support Forces (RSF), yalizuka mwezi Aprili baada ya mzozo kati ya majenerali wanaoongoza makundi hayo mawili.
Tangu wakati huo jeshi limejitahidi kudhibiti maeneo makubwa ya nchi, na kupoteza sehemu kubwa ya mji mkuu na eneo la magharibi la Darfur huku mapigano yakizidi.
Sasa iko nyuma ya Sudan ya kati baada ya RSF hivi karibuni kuchukua udhibiti Wad Madani, mji mkuu wa jimbo la Gezira, ambao ulionekana kuwa kimbilio salama kutokana na mapigano.
Watu ambao walikuwa wametafuta usalama kutoka Khartoum sasa wanalazimika kukimbia kwa mara ya pili. Kufikia sasa takriban watu 250,000 wamekimbia kutoka Gezira, kulingana na UN.
Eneo hilo linachukuliwa kuwa ghala la chakula la Sudan, likizalisha asilimia 70 ya ngano yake, na hivyo kuzusha hofu kwamba mgogoro huo unaweza kusababisha uhaba mkubwa wa chakula na "janga la njaa", kwa mujibu wa msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Rasha na familia yake walijaribu kukimbia vita vilipoanza lakini hawakufanikiwa. Mume wake na watoto wote ni raia wa Uingereza, na alitumai familia nzima ingestahiki kuhamishwa.
Familia hiyo ililipa "fedha nyingi" ili kusafirishwa hadi kituo cha kijeshi ambapo raia wa kigeni kutoka mataifa ya Magharibi walipaswa kuchukuliwa. Wakiwa njiani walishuhudia maafa ya vita - maiti zikiwa kando ya barabara, viwanda vikiungua, watu wakipora maduka yaliyotelekezwa.
Lakini matumaini yao ya kutoka nje yalididimia walipofika. Maafisa walimwambia kwamba mume wake mzaliwa wa London na watoto wao wanaweza kuhamishwa, lakini sio Rasha.
"Tulijaribu kuwaambia ni vigumu kumtenganisha mtoto anayenyonya na mama yake na kwamba tungeweza kulipia visa tukifika," anasema, huku akilia sana.
Familia haikuwa na budi ila kurudi nyumbani, anasema mumewe Mohammed Said ambaye anaamini kuwa lilikuwa "jambo la busara kufanya".
Tangu wakati huo ameomba usaidizi kutoka kwa serikali ya Uingereza ili kuhakikisha familia yake na watu wa mataifa mchanganyiko wanaweza kuhamishwa na kupelekwa nchini Uingereza.
Alipoulizwa kuhusu hali ya familia kama ya Rasha, Waziri wa masuala ya Afrika wa Uingereza Andrew Mitchell aliiambia BBC: "Tulipuuza baadhi ya sheria katika baadhi ya matukio kujaribu kusaidia familia ambazo zilipatikana katika hali hiyo", na akashauri kwamba familia "iendelee kuwasiliana." na Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza".
Rasha na mumewe wameandika barua pepe kwa Ofisi ya Mambo ya Nje na mbunge ambaye waliamua kutomtaja, lakini wanasema kwamba walipokea majibu ya kupitia mashine na sio mtu halisi.
"Bila shaka tunahisi kutelekezwa," anasema Mohammed, huku akikiri ugumu wa kumfikia mtu yeyote aliyenaswa katika eneo la vita.
Wakati huo huo familia bado imekwama huko Khartoum, imezungukwa na watu wenye silaha wanaozurura mitaani huku wahangaika kwa kukatikiwa na umeme kila siku na ukosefu wa huduma za kimsingi.
Juhudi za kujaribu kupata suluhu la kisiasa kwa mzozo unaoongozwa na majirani wa Sudan - kupitia jumuiya ya IGAD - na Saudi Arabia mpaka sasa hazijafanikiwa.
Majenerali wanaozozana - mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na Mohammed Hamdan Dagalo wa RSF - bado hawajakubali kukutana ana kwa ana. Matarajio ya kuwaleta kwenye meza ya mazungumzo yalizidi kuwa mbali zaidi katika wiki za hivi karibuni baada ya Jenerali Burhan kupinga tangazo la Igad la mafanikio na kuapa kupigana "kufa au kupona".
Serikali za Marekani na Uingereza zimesema pande zote mbili zimefanya uhalifu wa kivita. RSF imeshutumiwa zaidi kwa kufanya mauaji ya kikabila katika eneo la magharibi la Darfur.
Katika miezi ya hivi karibuni, jamii ambazo sio za Kiarabu nchini Sudan, hususan Masalit, zimekuwa zikilengwa, vijiji vyao kuchomwa moto na kumekuwa na ripoti za ubakaji mkubwa.
"Tutafanya kila tuwezalo pamoja na washirika wetu na watu wenye nia njema kuwawajibisha wale wanaotekeleza aina yoyote ya ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu," Bw Mitchell, waziri wa Uingereza, aliambia BBC.
Hali ya chakula nchini Sudan tayari ilikuwa mbaya kabla ya vita lakini hali inazidi kuwa mbaya huku mashirika ya misaada yakihangaika kusambaza misaada.
"Tumeweza kufika Khartoum kwa msaada wa chakula mara moja tu katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne iliyopita," Leni Kinzli, msemaji wa WFP wa Sudan alisema.
Uwezo wa nchi wa kulisha wakazi wake utajaribiwa vikali "Hakuna mtu anayejisikia salama popote nchini tena kwa sababu hali inaendelea kwa kasi... Njoo Mei, tunaangalia janga la njaa," Bi Kinzli aliambia BBC.
Mjini Khartoum, Rahsa na familia yake wanategemea msaada kutoka kwa jamaa zao.
Anamtuma kaka yake kununua chochote anachoweza kupata. Ikibahatika, anaweza kununua vijiko viwili vya maziwa ya unga na nepi mbili au tatu kwa wakati mmoja.
"Hakuna uwezekano wa kula nyama au kuku," anasema Rasha, akiongeza kuwa sasa wanaishi kwa maharagwe na mboga. Watoto "wamekonda sana" anasema, "na sasa suruali zao haziwatoshi tena".
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Maryam Dodo Abdalla