Wachezaji 7 maarufu duniani waliowahi kushitakiwa kwa ubakaji

- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Tarehe 4 Julai 2025 iligeuka kuwa siku nyingine ya kihistoria kwa mashabiki wa soka Afrika na duniani kwa ujumla baada ya Jeshi la Polisi la Uingereza kumfungulia mashtaka kiungo wa zamani wa klabu ya Arsenal, Mghana, Thomas Partey.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 anakabiliwa na mashtaka matano ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake watatu.
Kesi hizo, zinazohusisha matukio yaliyodaiwa kutokea kati ya 2021 na 2022, zinaangaliwa kwa jicho la karibu sana na mashabiki wa soka na vyombo vya habari. Pertey amekana mashataka hayo, kwa mujibu wa mwanasheria wake na kesi yake imepangwa kuendelea Agosti 2025.
Akiwa hana klabu baada ya mkataba wake na Arsenal kumalizika Juni 2025, Partey sasa anakabiliana na hali ngumu ndani na nje ya uwanja.
Hii si mara ya kwanza kwa jina kubwa kwenye soka kuhusishwa na tuhuma nzito kama hizi. Hapa ni orodha ya wachezaji wengine saba mashuhuri waliowahi kutuhumiwa na au kushtakiwa kwa ubakaji au unyanyasaji wa kingono, baadhi yao wakisafishwa na wengine wakiadhibiwa.
1. Cristiano Ronaldo - Ureno

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2009, mwanamke mmoja aitwaye Kathryn Mayorga, wakati huo mwenye umri wa miaka 24 alimtuhumu Cristiano Ronaldo, kwa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia katika chumba kimoja cha kulala wageni cha hoteli huko Las Vegas, Marekani.
Nyota huyo wa Ureno alikanusha vikali kupitia timu yake ya wanasheria akielekeza kilichotokea kwenye chumba hicho kilikuwa kitendo cha makubaliano. Ilibainika baadaye kwamba mwaka 2010 alimlipa kimya kimya kiasi cha $375,000 ili kutofungua kesi ya msingi Mahakamani.
Hata hivyo, mwaka 2018 madai hayo yaliibuka tena hadhara Mayorga akienda Mahakamani kuomba kuongezwa kwa malipo haya akitaka zaidi ya dola milioni 25 kutokana na kile alichoeleza kuchafuliwa jina kwa kashfa , udanganyifu na kuvunjwa kwa makubaliano yake na Ronaldo. Wazo hilo lilikataliwa na Jaji Jennifer Dorsey mnamo Juni 2022.
Ronaldo hakuwahi kushtakiwa rasmi kisheria kwa kosa la jinai la ubakaji , kutokana ushahidi mdogo wa tuhuma , na hadi leo anaendelea na majukumu yake kisoka soka akiwa na klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia.
2. Benjamin Mendy - Man City & Ufaransa

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliyekuwa beki wa Manchester City na timu ya taifa ya Ufaransa, Benjamin Mendy, alikumbwa na kesi ya kushangaza na kushtua ulimwengu wa soka kati ya mwaka 2021 na 2023. Alishtakiwa kwa makosa manane ya ubakaji, moja la jaribio la ubakaji, na moja la unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake kadhaa.
Mendy alikamatwa mwaka 2021 na kusimamishwa kucheza soka na klabu yake. Kesi yake ilianza rasmi Agosti 2022, na baada ya vikao virefu vya mahakama, alisafishwa na jopo la majaji Januari 2023. Baada ya kusafishwa, Mendy alijiunga na FC Lorient, na baadaye kuhamia FC Zurich. Ingawa amerudi uwanjani, kivuli cha kesi hiyo bado kinamfuata.
Kesi ya Mendy ilifuatiliwa kama tamthilia ya kweli: ushahidi wa video, ushuhuda wa waathiriwa, na ulinzi mkali wa mawakili wake vilizua mjadala mkubwa kuhusu maisha ya mastaa na maadili yao nje ya uwanja.
Baadaye beki huyo aliishtaki kalbu yake ya Manchester City Benjamin kwa kumsimamisha na kutomlipa mshahara wake tangu Septemba 2021 mpaka mkataba wake ulipomlizika Juni 2023.
Alishinda kesi na City ililazimika kumlipa mishahara yake yote zaidi ya pauni milioni 11 ($14.2 milioni).
3. Robinho - AC Milan & Brazil

Chanzo cha picha, Getty Images
Robinho, nyota wa zamani wa Brazil na klabu ya AC Milan, alihukumiwa na mahakama ya Italia mwaka 2017 kwa kosa la ubakaji wa mwanamke raia wa Albania katika klabu moja usiku jijini Milan mwaka 2013. Mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka tisa jela.
Hata hivyo, Robinho hakuhudhuria kesi hiyo na alikimbilia Brazil, nchi ambayo hairuhusu raia wake kutumikia nje ya nchi kwa mashitaka ya nje. Mnamo 2023, Mahakama ya Juu ya Italia ilithibitisha hukumu hiyo. Licha ya hayo, Robinho aliendelea kuwa huru nchini Brazil, ingawa heshima yake kama mchezaji imeporomoka vibaya.
Mwaka 2024 Mchezaji alikamatwa katika nyumba yake katika jiji la nyumbani la Santos ili kutumikia kifungo hicho cha miaka tisa jela kwa kosa la ubakaji lililohusisha genge la watu kadhaa dhidi ya mwanamke wa Kialbania.
Serikali ya Italia ilikuwa imeomba atumikie kifungo chake nchini Brazil baada ya kushindwa kumrejesha Italia alikoshitakiwa.
Mahakama nchini Brazili iliunga mkono uamuzi huo na pia iliamua kwamba anapaswa kutumikia kifungo chake jela badala ya kifungo cha nyumbani.
Wengi nchini Brazil walisifu mfumo wa haki wa Brazili ambao walihofia kwamba Robinho angekwepa haki kutokana na umaarufu wake na utajiri wake.
Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil, ambaye ameichezea nchi yake mechi 100, alikuwa akiichezea AC Milan wakati wa uhalifu huo. Baada ya kupatikana na hatia, alikata rufaa na kushindwa 2020 kabla ya Mahakama ya juu zaidi ya Italia kuidhinisha hukumu yake mnamo 2022.
Waendesha mashtaka wa Italia kisha wakatoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake.
Pamoja na hukumu yake Mwanasoka huyo, ambaye aliichezea Manchester City, kwa miaka miwili alikana kuhusika na ubakaji huo akisema ngono aliyoshiriki ilikuwa "ya makubaliano".
4. Dani Alves - Barcelona & Brazil

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji wa zamani wa FC Barcelona na Brazil, Dani Alves, alihukumiwa Februari 2024 kifungo cha miaka minne na nusu kwa kosa la ubakaji aliotekeleza katika klabu moja ya usiku huko Barcelona usiku wa kuamkia mwaka mpya 2022.
Hata hivyo, mnamo Machi 2025, Mahakama ya Rufaa ya Catalonia ilifuta hukumu hiyo, ikitaja mapungufu ya ushahidi na kutokuwepo kwa uthibitisho wa nia ya kingono isiyokuwa na ridhaa. Alves aliachiliwa kwa dhamana ya €1 milioni
Kesi hiyo ilivuta hisia za kimataifa, hasa kwa sababu ya hadhi ya Alves kama mmoja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa zaidi ya kutwaa makombe duniani. Mbrazil huyo amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya soka duniani kufikisha mataji 44 baada ya kushinda Olimpiki mwaka 2021.
Alves mara nyingi huchukuliwa kama mmoja wa mabeki bora zaidi wa wakati wote, alishinda sehemu kubwa ya mataji yake huko Hispania akiwa na Sevilla na kisha Barcelona. Baadaye alifurahia mafanikio nchini Italia akiwa na Juventus na kwa wababe wa Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG).
5. Mason Greenwood - Man Utd & England

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota wa zamani wa Manchester United, Mason Greenwood, alikumbwa na mashtaka mazito mwaka 2022 ya jaribio la ubakaji, na unyanyasaji wa kimwili dhidi ya mpenzi wake, yaliyosambaa kwa kasi kupitia sauti na video mitandaoni.
Hata hivyo, Februari 2023 mashtaka yote yalifutwa rasmi na CPS (Crown Prosecution Service) kwa kukosekana kwa ushahidi wa kutosha na mashahidi waliokataa kutoa ushirikiano.
Shahidi muhimu kabisa katika kesi hiyo, aliacha kutoa ushirikiano kwa Polisi waliokuwa wanafanya uchunguzi mwezi April 2022, hata hivyo waendesha mashataka waliendelea na kesi kwa muda kutokana na mvuto wa kesi hiyo kutokana na umaarufu wa Greenwood.
Baada ya muda wa sintofahamu, Mnamo Agosti 2023, Greenwood ilitolewa kwa mkopo kwenda Getafe kwa msimu wa 2023-24 wa ligi kuu Hispania (La Liga). Mnamo Julai 2024, aliondoka Manchester United kwa mkataba wa kudumu na kujiunga na klabu ya Ufaransa ya Marseille anakocheza mpaka sasa. Alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu Ufaransa (Ligue 1) msimu ulioisha wa 2024-25, akilingana mabao, 21 na mshambuliaji wa PSG, Ousmane Dembele.
6. Adam Johnson - Sunderland & England

Chanzo cha picha, Getty Images
Adam Johnson, aliyekuwa mchezaji wa Sunderland na timu ya taifa ya England, alikumbwa na kashfa nzito mwaka 2016 baada ya kukiri kosa la kushiriki vitendo vya kingono na msichana mwenye umri wa miaka 15. Pia alikiri kosa la kumshawishi mtoto kwa nia ya kushiriki ngono.
Alifungwa miaka sita jela, lakini aliachiwa kwa msamaha baada ya kutumikia nusu ya kifungo mwaka 2019. Tangu hapo, hajarudi tena kwenye soka ya ushindani na maisha yake yamekuwa ya faragha, yakitawaliwa na fedheha.
Tukio hilo liliathiri vibaya taswira ya soka ya Kiingereza, hasa ikizingatiwa kuwa Johnson alikuwa kipenzi cha mashabiki na mmoja wa vijana waliotegemewa na timu ya taifa ya England, Three Lions.
Baada ya kuachiliwa, juhudi zake za kurejea kwenye jamii zimekuwa za kusuasua, huku wengi wakimtazama kama mfano wa mchezaji aliyeharibu maisha yake kwa tamaa za kimwili.
7. David Goodwillie - Dundee & Scotland

Chanzo cha picha, SNS
Mwaka 2011, mshambuliaji wa zamani David Goodwillie na mwenzake David Robertson wakati huo wakiichezea Dundee United ya Scotland, walihusishwa na kesi ya ubakaji wa mwanamke mmoja huko Scotland, aliyeitwa Denise Clair.
Bi Clair alidai Robertson na Goodwillie walimbaka katika nyumba moja huko Armadale, West Lothian, baada ya mapumziko ya usiku huko Bathgate mnamo Januari 2011.
Ofisi ya Mwendesha ilifuta mashtaka ya ubakaji dhidi ya wanasoka hao baadaye mwaka huo baada ya kusema "hakuna ushahidi wa kutosha" wa kuwafungulia mashtaka.
Timu ya wanasheria ya Bi Clair iliendelea kuchukua hatua ya kiraia, ambayo walishinda mwaka wa 2017, licha ya Goodwillie kupinga kutokuwa na hatia.
Hata hivyo katika kesi hiyo ya kiraia ambalo ni jambo la nadra kwa mchezaji kuhukumiwa kwenye kesi ya kiraia kwa ubakaji, Jaji aliwaamuru wanasoka hao kulipa fidia ya £100,000 kwa Bi Clair.
Goodwillie kwa sasa anachezea Glasgow United inayoshiriki Ligi ya Magharibi ya Scotland, ligi ya hadhi ya daraja la tatu nchini Scotland.
Imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali












