Je, uvamizi wa ardhini wa Israel dhidi ya Rafah utaathiri vipi mkataba wa amani kati ya Misri na Israel?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, By Attia Nabil
- Nafasi, BBC Arabic, Cairo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry amekariri tena kujitolea kwa nchi yake kwa makubaliano ya amani ya 1979 na Israel.
Hii ilifuatia ripoti za vyombo vya habari vya Israel na Marekani kwamba Cairo ilikuwa ikitishia kusitisha mkataba huo iwapo Israel itaanzisha mashambulizi katika mji wa Palestina wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi kama haya yanaweza kuwasukuma maelfu ya Wapalestina kuvuka mpaka hadi kwenye Rasi ya Sinai nchini Misri, na kuwalazimisha kutoka katika nchi yao.
Bw Shoukry alipuuza ripoti hizo kwa kusema kwamba "maoni yoyote yaliyotolewa na watu binafsi yanaweza kupotoshwa".
Hata hivyo, chanzo cha ngazi ya juu nchini Misri kiliiambia Idhaa ya Habari ya Al-Qahera (Cairo) kwamba Misri inafuatilia kwa karibu hali mjini Rafah, na iko tayari kukabiliana na matukio yoyote, bila kutoa maelezo zaidi.
Masharti kuu ya mkataba ni yapi?
Misri na Israel zimewahi kupigana, vita vya hivi karibuni zaidi vikiwa vya mwaka 1973.
Marekani ilisaidia kufikiwa kwa mapatano ya amani kati ya nchi hizo mbili mwishoni mwa miaka ya 1970 katika hatua ambayo ilirejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuweka mipaka ya kijeshi katika pande zote za mpaka.
Itifaki iliyoambatanishwa na makubaliano ya 1979 iliweka mipaka kati ya nchi hizo mbili na kuzigawanya katika kanda kuu nne.
Kanda tatu ziko katika Rasi ya Sinai nchini Misri. Ya nne iko ndani ya Israel na inaitwa Zone D.

Chanzo cha picha, Getty Images
Zone D
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkataba huo unaruhusu kuwepo kwa kikosi kidogo cha kijeshi cha Israel ardhini katika Zone D. Inaundwa na vikosi vinne vya askari wanaotembea kwa miguu, kinajumuisha hadi wanajeshi 4,000, na ngome ndogo za uwanjani pamoja na waangalizi wa UN.
Kwa mujibu wa mkataba huo, vikosi vya Israel katika eneo hilo havipaswi kujumuisha vifaru vyovyote, mizinga au makombora ya kudungulia ndege, isipokuwa makombora yanayorushwa kutoka ardhini hadi angani.
Zone D ni 2.5km (maili 1.5) ndani ya mpaka wa Israel na Misri. Inajumuisha mpaka kati ya Ukanda wa Gaza na Misri, anasema mkuu wa Arab Strategic Foundation, Samir Ragheb, ambaye yuko Cairo.
Vikosi vya Israel vilikuwa vinadhibiti mpaka na Misri ndani ya Gaza, ikijumuisha eneo la urefu wa kilomita 14 karibu na mpaka wa Misri unaojulikana kama ukanda wa Philadelphi (pia unajulikana kama mhimili wa Salah El-Din), hadi kuondoka kwake kwa upande mmoja kutoka Ukanda huo mnamo 2005.
Baadaye Israel ilifikia makubaliano na Misri yaliyofahamika kama Maafikiano ya Philadelphi ambayo waliiambatanisha na makubaliano ya amani. Hii iliruhusu Misri kupeleka wanajeshi 750 katika eneo linalojulikana kama Zone C kando ya mpaka wake na Gaza na kando ya Zone D. Haikuwa vikosi vya kijeshi, bali ni jeshi la polisi ambalo kazi yake ni kupambana na ugaidi na upenyezaji wa mipaka.
Makubaliano ya awali ya mwaka 1979 yalizuia kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya Misri katika Kanda C na kuzuia uwepo wa usalama huko kwa vikosi vya kimataifa, waangalizi, na wanachama wa polisi wa kiraia wa Misri waliokuwa na silaha nyepesi.
Lakini Kiambatisho cha I cha mkataba wa amani kinaruhusu marekebisho ya mikataba ya usalama kwa ombi la mmoja wa wahusika, na kwa makubaliano yao.
Mnamo mwaka wa 2021, Misri na Israel zilitangaza kuimarishwa kwa uwepo wa jeshi la Misri katika Kanda C na kupelekwa kwa vifaru, magari ya kivita na kubeba wafanyikazi ili kupambana na ugaidi na kukabiliana na vitisho vinavyoletwa na wapiganaji wa Islamic State huko Sinai Kaskazini.
'Operesheni ya Rafah inaweza kuwa ukiukaji wa mkataba'
Dk Ayman Salameh, mhadhiri wa sheria za kimataifa na mjumbe wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Misri, anasema Israel haina haki ya kupeleka wanajeshi wa ziada katika Kanda D bila kibali kutoka Misri, hata kwa madhumuni ya kulinda usalama wa kitaifa wa nchi hizo mbili.
Hatua ya Israel ya kupeleka vikosi vyake vya kijeshi kwenye mpaka wa kimataifa na Misri, hata bila ya mapigano yoyote au operesheni za kijeshi, inapaswa kuchukuliwa kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya amani na vipengele vyake vya usalama, anaongeza Dk Salameh. Alisema itakuwa "kitendo cha uadui" ambacho kinatishia usalama wa taifa wa Misri.
Misri ina haki, katika mazingira ya kipekee au ya kulazimisha ambayo yanawakilisha tishio kwa usalama wa taifa, kupitia au kusimamisha makubaliano na Israel, alisema.
Hii inatokana na Mkataba wa Vienna wa Sheria ya Mikataba ya 1969, ambayo inaruhusu upande wowote katika mkataba wa kimataifa kuufuta au kuuzuia, kwa ujumla au kwa sehemu, ikiwa kuna tishio la moja kwa moja kwa uhuru wa kitaifa au uhuru wa serikali kutoka kwa mshiriki wa mkataba huo.
Misri imepinga kauli zilizotolewa na maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Israel kuhusu nia yao ya kuanzisha operesheni ya kijeshi katika mji wa Rafah, ikionya kuhusu "athari mbaya" ya hatua hiyo.
Haya yanajiri huku jamii ya kimataifa na jumuiya za mataifa ya Uarabuni zikihofia "hali ya janga huko Gaza" ikiwa Israel itaendelea na mipango yake.
Misri inahofia kuwa maelfu ya Wapalestina huenda wakavuka mpaka wake iwapo hali itazidi kuzorota katika mji huo ambao sasa una Wapalestina takriban milioni 1.4.

Mtazamo tofauti nchini Israel
Yohanan Tzoreff, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Taifa nchini Israel, anasema mkataba wa amani wa Misri na Israel hauizuii Israel kupata haki ya kulinda usalama wake na usalama wa mipaka yake.
Anasisitiza umuhimu wa mkataba huo kwa nchi zote mbili na anapuuza wasiwasi wa Misri kuhusu uwezekano wa operesheni ya kijeshi ndani ya Rafah, akisema kuna majaribio ya Israel ya kushirikiana na Misri kuhusu hali hiyo.
Cairo inatarajiwa kuwa mwenyeji wa duru ya mazungumzo ambayo yatajumuisha Mkurugenzi wa CIA William Burns na ujumbe wa ngazi ya juu wa usalama wa Israel kujadili mipango ya Israel kwa uwezekano wa operesheni hiyo huko Rafah.
Pia watajadili hatua ya hivi punde katika juhudi ya kusitisha mapigano, pamoja na kubadilishana mateka na wafungwa kati ya Israel na Hamas, ripoti za vyombo vya habari zinasema.
Je kuna ushirikiano kati ya Misri na Israel?
Misri imekanusha mara kwa mara kuwepo kwa ushirikiano wowote kati ya Misri na Israel kuhusiana na operesheni za kijeshi zinazofanyika sasa ndani ya Ukanda wa Gaza, haswa katika ukanda wa Philadelphi au Zone D.
Katika wiki za hivi karibuni, tofauti kati ya Misri na Israel zimeibuka, huku maafisa wa Israel wakitangaza uwezekano wa kufanya operesheni ya kijeshi huko Rafah, na uwezekano wa kuchukua udhibiti wa ukanda wa Philadelphi, wakiishutumu Cairo kwa kushindwa kuwazuia Hamas kusafirisha silaha kimagendo hadi Gaza.
Misri imepinga shutuma hizo, ikisisitiza uwezo wake wa kudhibiti kikamilifu mipaka yake. Pia imekanusha kuwepo kwa mahandaki, au usafirishaji silaha kimagendo kutoka eneo la Misri hadi Ukanda wa Gaza.
Pia ilionya kuhusu kile ilichoeleza kuwa ni "juhudi za Israel za kuunda uhalali wa kukalia kwa mabavu ukanda wa Philadelphi", ikisema kwamba itasababisha "madhara makubwa kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili".
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












