Waridi wa BBC: 'Tulipishana miaka 40 na mume wangu lakini nilimpenda'

ddd

Chanzo cha picha, Doreen Kimbi

    • Author, Veronica Mapunda
    • Nafasi, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kuolewa na aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa mambo ya ndani, Mgombea Urais katika uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1995 na kushika nafasi ya pili na kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Augustino Lyatonga Mrema. Ndoa ilikuwa Machi 2022.

Jina lake lilitawala vyombo vya habari na mitandao ya kijamii huku kukiwa na kauli mchangayiko ikiwemo zinazombeza kama vile 'Kaolewa na mzee' kafuata mali na nyingine nyingi.

"Watu wengi walidhani nimefuata mali, sikuwaza kabisa kuhusu mali na baada ya kufariki mitandao ilinishambulia sana amefuata mali, atamuua huyu mzee, wakawa wanatuma picha zangu mbaya mbaya lakini nilimuomba Mungu akanipa ujasiri"

Doreen Kimbi, 40 ni mfanyabiashara na mjasiriamali wa masuala ya utalii katika mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania na pia anajihusisha na kusaidia wazee.

Shughuli zake za biashara alizianza kabla hata ya kuolewa na Mrema.

dd

Chanzo cha picha, Doreen Kimbi

Ndoa yake ilidumu kwa muda wa miezi mitano tu, kabla ya mume wake mpenzi kufaririki dunia na kuzua mjadala mkubwa nchini Tanzania.

Mjadala wa kwanza ulijiegemeza kwenye utofauti mkubwa umri kati yake na Mrema. Walitofautiana miaka 40, ambao unatosha kuwa mjukuu wake.

"Nilimpenda na bado nampenda"

Doreen anasema upendo ndio uliomsukuma kuolewa na Mrema, na sio mali, umaarufu ama cheo chake.

"Ni upendo nilichokuwa nataka, ni mapenzi alininipenda na nilimpenda na bado nampenda," alisema kwa hisia.

Alikiri kwamba umri wake ulikuwa tofauti na wa mume wake, lakini hakuwahi kuona kuwa ni tatizo.

"Umri ni namba tu kwangu, haikuwa tatizo, ila kwa watu wengine ndio ilikuwa changamoto," aliongeza Doreen.

ddd

Chanzo cha picha, Doreen Kimbi

'Tulikutana Kanisani'

Doreen anapenda Wazee. Amekuwa akiishi nao na kuwatunza. mapenzi yake kwa wazee, ilijenga urahisi hata alipokutana na Mzee Mrema.

Alikuwa akimjua tangu akiwa mtoto, kwa kumuona na kumsikia kupitia vyombo vya habari, Lakini kwa mara ya kwanza alikutana nae Kanisani.

"Tulikutana kanisani, nilikuwa namjua zamani nikiwa mtoto namuona, lakini wakati huo nilikuwa naye kabisa," alisema Doreen

Alikaa kwenye uhusiano na Mrema miezi mitatu kabla hajaamua kumtakia kuwa anataka kufunga naye ndoa.

"Siku ananiambia nilishtuka alitumia Padri kuniambia, nikasema kumbe anamaanisha, lakini nikawa nafikiria umri wake," alieleza Doreen.

Hata hivyo, Doreen anasema aligundua kuwa Mrema alikuwa na mapenzi ya kweli hivyo hakuwa na budi kukubaliana naye na kuanzisha uhusiano naye.

ggg

Chanzo cha picha, Doreen Kimbi

"Aolewa na Mzee"

Baada ya ndoa yake, jina la Doreen lilitawala vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, huku vichwa vya habari vikisema "aolewa na mzee" na wengine wakiandika kuwa alifunga ndoa kwa ajili ya mali.

Doreen alisema kuwa familia yake ilijua ukweli na alisisitiza kuwa hakuwa na nia ya kutafuta mali, bali aliolewa kwa upendo.

"Watu wengi waliandika hivyo, lakini hata sikufikiria kuhusu mali zake wala sikujua kama ana mali, kwani tayari alikuwa na watoto wakubwa. Mimi nilikuwa najua tu napendwa," alisema Doreen kwa msisitizo.

"Sikuwa na Changamoto kwenye ndoa yangu"

Doreen alikiri kuwa maisha ya ndoa yalikuwa mazuri na kwamba hakukuwa na changamoto kubwa. Alijivunia kuwa mama, mke, na bibi katika familia yake.

"Nilikuwa namuuguza alipoumwa," alisema kwa furaha, akielezea jinsi alivyomtunza mumewe hadi mauti yalipomfika.

Maisha baada ya Kifo cha Mrema

Baada ya kifo cha Mrema, Doreen alikumbana na mashambulizi makali kutoka kwa watu mitandaoni.

Alielezea jinsi alivyoshambuliwa na picha na maneno mabaya yaliyoenezwa kwenye mitandao, akisema kuwa hali hiyo iliumiza sana.

"Nilishambuliwa zaidi wakati nikiwa nimefiwa, niliachana na mitandao, nilinyang'anywa simu na ndugu zangu," alisema Doreen, huku akionyesha huzuni kwa namna alivyovurugwa na mitandao ya kijamii.

Aliongeza kuwa familia yake ilimsaidia sana katika kipindi hicho kigumu, na watoto wake walihitaji msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na mashambulizi hayo.

"Mtoto wangu alikuwa anasoma shule ya kimataifa huko Moshi ambapo walikuwa huru kuangalia tv, kuwa na simu na hata magazeti hivyo alikuwa anaona kila kitu, na ilikuwa inamuumiza sana"

ggg

Chanzo cha picha, Doreen Kimbi

"Maisha yangu yamebadilika, Lakini Sijawahi Kumsahau Mrema"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya changamoto hizo, Doreen aliendelea kuishi maisha ya furaha, akijivunia familia yake na miradi yake mwenyewe.

Alisema kuwa kuolewa na Mrema haikuwa kwa bahati mbaya, kwani alikusudia kuendelea kusaidia wazee, jambo ambalo alikuwa akilifanya hata kabla ya kuolewa na Mrema.

"Wakati namuuguza aliniambia Doreen, naomba nikufie mikononi mwako, usiniache." Alisema kuwa alitimiza ombi hilo na kumshika mumewe hadi alipofariki na alifariki akiwa mikononi mwake.

Doreen alisema kuwa tangu kifo cha mumewe, hajawahi kuwa sawa kabisa. "Nashindwa kueleza, bado kuna vitu nakumbuka, na mpaka leo sijaamua kuwa na mtu mwingine. Ninasali sana," alisema huku machozi yakimtoka.

Doreen anaendelea kuishi na kumbukumbu za mumewe na anajivunia kuwa na familia yake na miradi ambayo inamsaidia kuendelea kufanya kazi ya kusaidia wazee.

Aliwapenda wazee kabla ya kukutana na Mzee Mrema na anawapenda hata baada ya kifo cha Mrema, na sasa anazindua Kituo chake cha kusaidia wazee alichokipa jina la mumewe, Agustine Lyatonga Mrema, ili kumuenzi na kuenzi wazee anaowapenda sana.