Madai ya uongo yasambaa kuwa kituo cha utafiti cha Marekani kilisababisha tetemeko la ardhi Uturuki, Syria

Chanzo cha picha, Reuters
Tangu tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 liikumbe Uturuki na Syria tarehe 6 Februari, na kuua zaidi ya watu 44,000, kumekuwa na mamilioni ya machapisho kwenye Twitter yakishiriki habari, picha na video za maafa hayo.
Lakini BBC imegundua kwamba baadhi ya machapisho hayo yameilaumu kwa njia isiyo sahihi HAARP, kisambaza data chenye nguvu kilichoko Alaska, Marekani, kwa kusababisha tetemeko la ardhi.
HAARP Ilianzishwa na jeshi la Marekani mnamo 1990 na imekuwa ikiendeshwa na Chuo Kikuu cha Alaska Fairbanks tangu 2014.
Habari potofu kuhusu HAARP
Kufuatia tetemeko la ardhi kulikuwa na ongezeko la idadi ya akaunti zinazochapisha kuhusu HAARP kwenye Twitter. Utafiti wa BBC uligundua kuwa ilitajwa zaidi ya mara 550,000.
Katika moja ya machapisho, mwandishi aliuliza: "Ni nini hasa kilitokea Uturuki... Walitumia urekebishaji wa hali ya hewa ya Geo-engineering HAARP!"
Mtumiaji mwingine alishiriki video ya ndege na kusema kwamba wanyama walikuwa "wakitenda vitu vya ajabu" kabla ya tetemeko la ardhi, kisha akauliza ikiwa Uturuki "ilishambuliwa na HAARP?"
Watu pia walikuwa wakichapisha picha za mawingu, wakidai kuwa zilionekana Uturuki kabla ya tetemeko la ardhi na zilitengenezwa na HAARP.
Jessica Matthews, meneja wa programu wa HAARP aliiambia BBC: "Vifaa vya utafiti kwenye tovuti ya HAARP haviwezi kuunda au kukuza majanga ya asili."
Aaron Ridley, profesa wa sayansi ya hali ya hewa na anga katika Chuo Kikuu cha Michigan anakubali: "Hakuna ushahidi wa kisayansi wowote kwamba HAARP inaweza kudhibiti hali ya hewa."
Si mara ya kwanza HAARP kulaumiwa kwa uwongo kwa kuzua majanga ya asili.
''Mpango wa HAARP umetajwa mara kwa mara kama sababu kuu ya majanga mengi ya asili, licha ya ukweli kwamba madai kama hayo yamepuuzwa na wanasayansi na wataalamu," anaeleza mwandishi wa habari wa BBC Disinformation Shayan Sardarizadeh.
HAARP hufanya nini?
HAARP ilianzishwa awali ili kutafiti athari za tabaka la angahewa ya dunia ambayo ina mkusanyiko mkubwa wa ayoni na elektroni na ina uwezo wa kuakisi mawimbi ya redio (ionosphere) kwenye mawasiliano ya kijeshi na kiraia na mifumo ya urambazaji.
Usumbufu unaotokea kwa kawaida katika ionosphere unaweza kuvuruga mawimbi ya redio yanayopitishwa kutoka duniani, ambayo ni muhimu kwa aina nyingi za teknolojia ya kisasa, ikiwa ni pamoja na satelaiti za GPS, mifumo ya Wi-Fi na vyombo vya anga na mawasiliano ya redio.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Katika ionosphere unaweza kupata misukosuko... ambayo inaweza kunyonya mawimbi ya redio na mawasiliano yasiwezekane tena, mawimbi ya redio hupotea katika ionosphere," Prof Ridley alisema.
Misukosuko hii ni ngumu kutabiri kwa hivyo wanasayansi katika HAARP hutumia visambazaji vya redio vya masafa ya juu ili kupasha joto sehemu ndogo za ionosphere na kuunda hali sawa na zile zinazotokea katika maumbile ili ziweze kuchunguzwa.
Jessica Matthews anasema mchakato huu hausababishi matukio ya hali ya hewa, "Mawimbi ya redio katika masafa ambayo HAARP hupitisha hayajaingizwa katika viwango viwili vya angahewa vinavyozalisha hali ya hewa ya Dunia."
David Hysell, profesa wa Sayansi ya Dunia na anga katika Chuo Kikuu cha Cornell anakubali kwamba HAARP haiwezi kuwa na ushawishi juu ya hali ya hewa.
"Vitu hivi havina uhusiano wowote," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
"Nadharia za njama zinaingia kupita kiasi kwenye mitandao ya kijamii baada ya maafa," mwandishi wa BBC Shayan Sardarizadeh alisema.
Mnamo 2022, mafuriko yalipopiga jiji la Bulgaria la Karlovo, kulikuwa na madai ya uongo kwenye mitandao ya kijamii kuwa mvua hiyo kubwa ilisababishwa na HAARP.
HAARP pia ililaumiwa kwa mafuriko mabaya nchini China na moto mkubwa wa misitu nchini Uturuki mnamo 2021.
Baada ya Kimbunga Ian kupiga Karibea na kusini-mashariki mwa Marekani mwaka wa 2022, madai zaidi ya uongo kuhusu HAARP yalifurika kwenye mitandao ya kijamii.
Tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria lilikuwa kichochezi cha hivi punde zaidi cha madai hayo ya uwongo, lakini pengine sio ya mwisho.
"Nadharia za zamani mara nyingi hutunzwa tena kama ushahidi zaidi kwa simulizi ambayo tayari imekanushwa ili kuimarisha maoni ya wale wanaoziamini na kuleta wafuasi wapya," Sardarizadeh alisema.















