Vita vya Ukraine: Biden amemwambia Zelensky nchi yake haitasimama peke yake

Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwamba Marekani itashirikiana na Ukraine "kwa muda wote itachukua" katika vita vyake na Urusi.

"Hautasimama peke yako," Bw Biden alimwambia Bw Zelensky alipotembelea Ikulu ya White House katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu uvamizi wa Urusi uanze.

Bw Biden alithibitisha kifurushi kipya cha msaada wa zaidi ya $2bn (£1.7bn) kwa Ukraine na kuahidi $45bn nyingine.

Bw Zelensky alitoa shukrani zake kwa kuungwa mkono na Marekani.

Katika mkutano wa pamoja wa wanahabari siku ya Jumatano, Bw Biden aliwaambia waandishi wa habari kuwa "hana wasiwasi hata kidogo" kuhusu kufanya muungano wa kimataifa pamoja.

Huku kukiwa na wasiwasi kwamba baadhi ya washirika wanaweza kuhisi matatizo ya gharama ya mzozo huo na usumbufu wa usambazaji wa chakula na nishati duniani, rais wa Marekani alisema anajisikia "vizuri sana" kuhusu mshikamano wa kuiunga mkono Ukraine.

Bw Biden alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin "hakuwa na nia ya kusitisha vita hivi vya kikatili".

Kama mshirika muhimu zaidi wa Ukraine, Marekani tayari imetoa $50bn (£41bn) ya usaidizi wa kibinadamu, kifedha na usalama - zaidi ya nchi nyingine yoyote.

Bw Zelensky - akiwa amevalia sweta la rangi ya kijani kibichi na buti - alielezea matumaini yake kwamba Congress ingepitisha $45bn ya ziada kama msaada kwa Ukraine "kutusaidia kutetea maadili na uhuru wetu".

Republican - ambao watachukua udhibiti wa Baraza la Wawakilishi mnamo Januari - wameonya hawataandika "cheki tupu" kwa Ukraine

Lakini Bw Zelensky, ambaye alisafiri kwa ndege ya Jeshi la Wanahewa la Marekani kutoka mji wa Rzeszow nchini Poland, alisema kwamba "bila kujali mabadiliko katika Bunge la Congress", aliamini kutakuwa na uungwaji mkono wa pande mbili kwa nchi yake.

Baada ya mkutano wa White House, rais wa Ukraine mwenye umri wa miaka 44 alitoa hotuba kwenye kikao cha pamoja cha Congress, ambapo alikaribishwa kwa shangwe.

Aliwaambia wabunge wa Marekani kuwa nchi yake bado inasimama "dhidi ya uwezekano wote" na kutabiri "mabadiliko" katika mzozo huo mwaka ujao.

Huku akiihaidi Ukraine haitajisalimisha kamwe, alisema ilihitaji silaha zaidi.

"Tuna silaha, ndio, asante," aliwaambia "Inatosha? Kusema kweli, si kweli."

"Ili jeshi la Urusi kujiondoa kabisa, mizinga na makombora zaidi yanahitajika," aliongeza.

Akihitimisha hotuba yake, Bw Zelensky aliwasilisha Bunge la Congress bendera ya vita iliyotiwa saini na watetezi wa Bakhmut, jiji lililo mstari wa mbele mashariki mwa Ukraine ambalo alitembelea katika mkesha wa safari yake ya Washington.

Kifurushi cha usaidizi wa usalama kilichotangazwa na Marekani siku ya Jumatano kinajumuisha mfumo mpya wa makombora wa Patriot, ambao unatarajiwa kuisaidia Ukraine kulinda miji yake dhidi ya makombora na ndege zisizo na rubani ambazo Urusi imerusha kwenye vituo muhimu.

Tukio la nadra liliibuka katika mkutano wa wanahabari wa Jumatano wakati Bw Zelensky, mcheshi wa zamani, akijibu maswali ya wanahabari.

"Tuko kwenye vita, samahani, samahani sana," alisisitiza kwa Kiingereza, huku watazamaji katika Chumba cha Mashariki wakicheka.

Bwana Biden alicheka na kusema: "Tunaifanyia kazi."

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema uwasilishaji wa mfumo wa hali ya juu wa makombora ya kutoka ardhini hadi angani utachukuliwa kuwa hatua ya uchochezi.

Mapema Jumatano, Bw Putin alisema anaamini kuwa nchi yake haifai kulaumiwa kwa vita vya Ukraine, na kuongeza kuwa nchi zote mbili "zinashiriki katika janga hili".

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari, jeshi la Marekani linakadiria kuwa wanajeshi 100,000 wa Urusi na 100,000 wa Ukraine wameuawa au kujeruhiwa, pamoja na vifo vya raia 40,000.

Umoja wa Mataifa umerekodi watu milioni 7.8 kama wakimbizi kutoka Ukraine kote Ulaya, ikiwa ni pamoja na Urusi. Hata hivyo, idadi hiyo haijumuishi wale ambao wamelazimika kukimbia makazi yao lakini wakisalia Ukraine.